Tamko la Polisi kwa anayetajwa kuwa ‘afande’

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa kina umefanyika na jalada limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) kuhusu Fatuma Kigondo anayetajwa kuwa ni afande na kudaiwa kuwatuma vijana waliombaka kwa kundi na kumlawiti binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam.

“Jeshi la Polisi lingependa kutoa taarifa juu ya Ofisa wa Polisi anayetajwa kwa jina la Fatuma Kigondo kwamba uchunguzi wa kina ulishafanyika ikiwa ni pamoja na kupata maelezo ya watu mbalimbali pamoja na ya kwake na jalada limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka,” inaeleza taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime iliyotolewa kwa umma leo Jumamosi Agosti 24, 2024.

Taarifa ya polisi imetolewa zikiwa zimepita siku 20 tangu kusambaa kwenye mitandao ya kijamii picha jongefu (video) ikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumwingilia binti kinyume cha maumbile.

Kupitia video hiyo vijana, hao walimtaka binti huyo aliyejitambulisha kuwa mkazi wa Yombo Dovya kumuomba msahama ‘afande’ kwa kosa la kutembea na mume wake.

Video hizo zilisambaa Jumapili ya Agosti 4, 2024 na kuzua taharuki kwenye jamii, wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu wakipaza sauti wakitaka hatua kali zichukuliwe kwa wote waliohusika ikiwemo aliyetambuliwa kwa jina la ‘Afande.’

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts