Ukaguzi kuboresha miundombinu Ngorongoro kuanza Agosti 27 

Arusha. Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, imesema inatarajia kuanza kukagua, kubainisha vituo vya kupigia kura na kufanya maandalizi mengine kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Mahakama Kuu kuzuia tamko la Serikali la kufuta kata, vijiji na vitongoji vikiwamo vya wilayani Ngorongoro na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuondolewa vikwazo kwa wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ngorongoro, Murtallah Mbillu, amesema hayo leo Jumamosi Agosti 24, 2024 alipozungumza na Mwananchi.

Amesema kuanzia Agosti 27, 2024 atakwenda Tarafa ya Ngorongoro kutembelea vituo vya afya, shule na maeneo mengine ambayo yatatumika kwa ajili ya kupigia kura.

“Kuanzia Jumanne nitaenda kwenye Tarafa ya Ngorongoro kutembelea shule, vituo vya afya na kuainisha vituo vya kupiga kura, ili kuendelea na maandalizi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa,” amesema.

Kuhusu maagizo ya kurejeshwa huduma za kijamii zikiwamo za maji, afya na elimu, amesema kuanzia wiki ijapo mbali na kukagua vituo vya kupigia kura, ataenda na mhandisi ambaye ataainisha miundombinu ya shule, maji na vituo vya afya inayotakiwa kuboreshwa.

“Tutakuwa na mhandisi na kuna Sh350 milioni zilizotolewa na mamlaka (Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro -NCAA), tutazitumia kwa ajili ya kukarabati miundombinu ambayo imeharibika ikiwemo ya vyoo katika shule,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kurejeshwa kwa huduma za kijamii, kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuondolewa vikwazo kwa wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro.

Maagizo hayo yalitolewa baada ya wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro kuandamana na kukusanyika kwa siku tano mfululizo wakipinga kufutwa vitongoji 96, vijiji 25 na kata 11, amri ambayo kimsingi ilikuwa inawakosesha haki ya kupiga kura.

Maagizo ya Rais Samia yalitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliyeambatana na viongozi wengine kuzungumza na wananchi wa kata 11, katika eneo la Oloirobi lililopo Kata ya Ngorongoro.

Agosti 22, 2024 Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ilitoa zuio la utekelezaji wa tangazo la Serikali namba 673 la Agosti 2, 2024.

Tangazo hilo chini ya kifungu cha 30 cha Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), lililotoa tamko la kufuta vijiji, kata na vitongoji kutoka wilaya za Ngorongoro, Bahi, Chemba, Kasulu, Kakonko, Hai na Rombo.

Uamuzi wa Mahakama ulitolewa na Jaji Ayoub Mwenda, aliyesikiliza maombi madogo ya zuio yaliyowasilishwa na mmoja wa wananchi wa Ngorongoro, Isaya Ole Pose kupitia wakili Peter Njau. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Jaji aliridhia zuio hilo. Maombi ya msingi yatasikilizwa Septemba 26, 2024.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Kanali Wilson Sakulo, amesema hali ya ulinzi na usalama wilayani humo ni shwari na wananchi waliokuwa wamekusanyika katika makundi mawili, waliondoka jana Agosti 23 usiku baada ya tamko la Serikali.

Mbunge wa Ngorongoro, Emanuel Ole Shangai, amesema wananchi waliokuwa wamekusanyika walianza kuondoka kurejea makwao jana.

Related Posts