Wajasiriamali walia mikopo umiza inasababisha afya ya akili

Mwanza. Baadhi ya wajasiriamali jijini Mwanza wamesimulia namna mikopo umiza inavyowasababishia kupata tatizo la afya ya akili.

Wamesema hayo kwa nyakati tofauti jana Ijumaa Agosti 23, 2024 wakati wa semina ya elimu ya fedha, utunzaji wa kumbukumbu za biashara na afya ya akili kwa wajasiriamali yaliyoandaliwa na Shirika la Patrice Global Mission (PGM) kwa kushirikiana na Benki ya Absa.

Wamesema mbali na mikopo umiza kuwa na riba kubwa, hata namna wanavyodaiwa huwasababishia muda wote kuwa na hofu ya kushindwa kufanya mambo mengine na kujikuta wakiuza mali zao bila kupenda.

“Hii imewahi kuniathiri mpaka nikauza ng’ombe zangu, nilikopa fedha Sh300,000 na ilibidi nirejeshe Sh600,000 kwa kipindi cha miezi mitatu kwa maana riba ilikuwa ni Sh300,000 na mimi wakati nakopa nilikuwa na shida sana lakini masharti yalikuwa magumu sana ila sikuwa na namna,” amesema Obadia Emmanuel dereva wa bodaboda, eneo la Malimbe jijini Mwanza.

“Nilijikuta mwisho wa siku nakuja kulipa Sh1.2 milioni baada ya miezi sita kwa sababu ilizalisha zaidi japo kuwa nililipa kwa shida sana lakini nilijikuta nimepata hasara kubwa sana kwa kipindi hicho, nilikuwa na msongo wa mawazo mkubwa sana mpaka kuna muda nikakosa namna ya kufanya ndiyo nikaamua kujifilisi,” amesema.

Kwa upande wake, mjasiriamali wa viungo vya chai jijini humo, Salome Kusekwa amesema kipindi anamsomesha mtoto wake chuo alichukua mikopo hadi kufikia hatua ya kujificha ndani huku akiogopa kushika simu kwa lengo la kuwakwepa wadai wake.

“Nimewahi kukopa wakati nasomesha mtoto wangu chuoni nilikuwa na madeni mengi kiasi ambacho hata simu nilikuwa naogopa kushika na hata ilipokuwa ikiita hofu ilikuwa ikitanda mpaka kuna wakati nilikuwa najifungia ndani naogopa kutoka nje kwa kuwakwepa wanao nidai,” amesema.

Mkurugenzi wa Afya na Mafunzo Shirika la PGM ambaye pia ni Mtaalamu wa Afya ya Akili, Dk Nuru Ndomondo akitoa elimu kwa wajasiliamali jijini Mwanza kwenye semina iliyofanyika jana Agosti 23, 2024. Picha na Anania Kajuni

“Shida iliyopo kwenye mikopo ya Serikali kuna milolongo mingi sana kwa sababu nahitaji kupata fedha leo, lakini ukifuatilia unachukua zaidi ya mwezi sasa hiyo shida yako si inakuwa imeisha ndio maana tunakimbilia kwenye mikopo umiza hivyo niombe Serikali labda ijaribu kupunguza milolongo ya upataji mikopo,” amesema Kusekwa.

Mfanyabiashara katika eneo la Kilimahewa wilayani Ilemela mkoani humo, Lydia Josephat ametoa wito kwa wananchi hasa wanawake kuachana na tabia ya kujiunga kwenye vikundi vingi vya kuchangishana fedha kwa kuwa ndio sababu ya kukimbilia mikopo umiza na kupata tatizo la afya ya akili

“Niwaambie wanawake na wanaume punguza vikundi sio sifa kuwa na vikundi vingi angali huna uwezo ni bora kuwa na kikundi kimoja au viwili kwa sababu ukiwa navyo vingi utajikuta unaenda kukopa mikopo ya kausha damu ili upate fedha ya mchezo,” amesema Lydia.

Mkurugenzi Mtendaji katika Shirika la PGM, Boni Nyabweta ametoa wito kwa wajasiriamali na wananchi kuachana na mikopo ya mtaani yenye riba kubwa badala yake wajikite kuomba mikopo inayotolewa na Serikali au kwenye taasisi za fedha zenye riba ndogo.

“Ili kukabiliana na changamoto hiyo kwanza ni kuwa na uelewa wa mikopo yenye masharti nafuu na mingi inatolewa na Serikali mfano mikopo ya asilimia 10 lakini pia kuna Sh18 bilioni ambayo imetengwa kwa ajili ya mikopo kwa wajasiriamali wadogo, kwa hiyo wajielekeze kule badala ya kuendelea kuumizwa na mikopo umiza,” amesema Nyabweta.

Mkurugenzi wa Afya na Mafunzo wa Shirika la PGM ambaye pia ni Mtaalamu wa Afya ya Akili, Dk Nuru Ndomondo amewashauri wajasiriamali kuwaona wataalamu wa fedha na wanasaikolojia pindi wanapokutana na changamoto ya afya ya akili inayotokana na mikopo umiza kwa ajili ya kuwapa ushauri na kusaidiwa.

“Ukiona imetokea hali kama hiyo ya kusumbuliwa na mikopo umiza basi nenda ukawaone wataalamu wa fedha na afya ya akili pale anapoona dalili za kuwa na tatizo hilo na huko watamsaidia au kumuelekeza wapi akapate msaada,” amesema Dk Ndomondo.

Related Posts