Yanga yafanya maangamizi kwa Vital’O

TIMU ya Yanga imetinga hatua ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 6-0, dhidi ya Vital’O ya Burundi katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.

Yanga imepata bao la mapema tu dakika ya 13 kupitia kwa nyota wa kikosi hicho, Pacome Zouzoua kwa mkwaju wa penalti baada ya kuupia mpira langoni mwa Vital’O’ na kumfanya beki wa timu hiyo, Amedee Ndavyutse, kuudaka eneo la hatari kisha kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Yanga imeandika bao la pili dakika ya 48, kupitia kwa nyota wa timu hiyo, Clement Mzize dakika ya 48, kisha Clatous Chama akitupia la tatu dakika ya 50, huku Prince Dube aliyeingia kipindi cha pili akaendeleza moto wake baada ya kutupia la nne dakika ya 72.

Mabao mengine ya Yanga yamefungwa na Aziz Ki, huku lile la sita akifunga Mudathir Yahya.

MCHEZO WA UPANDE MMOJA
Kitendo cha beki wa timu ya Vital’O’, Amedee Ndavyutse kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 12 baada ya kuushika mpira eneo la hatari, kiliifanya Yanga kuutawala mchezo kwa kushambulia lango la wapinzani wao ambao walijilinda huku wakishambulia kwa kushtukiza.

Hata hivyo, licha ya Yanga kutengeneza nafasi nyingi kupitia kwa viungo wake washambuliaji, Clatous Chama na Pacome Zouzoua aliyefunga bao la utangulizi, ila bado eneo la mwisho la umaliziaji lililokuwa linaongozwa na Kennedy Musonda na Clement Mzize lilikosa utulivu wa kutumia vyema nafasi za kufunga mabao zaidi dakika 45, za kwanza.

Kipindi cha pili Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amefanya mabadiliko ya mapema kwa kumtoa Aziz Andambwile na nafasi yake kuchukuliwa na Stephane Aziz KI Ili kuongeza mashambulizi zaidi.

Mabadiliko hayo yameanza kuonyesha manufaa mapema tu kwani dakika mbili za kipindi cha pili kwa maana ya 48 na 50 yalizaa mabao mawili yaliyofungwa na Clement Mzize na Clatous Chama.

YAFUZU KIBABE
Yanga imefuzu kibabe katika hatua ya pili ya michuano hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-0, baada ya mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa pia kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi Agosti 17 jijini Dar es Salaam kushinda mabao 4-0.

Katika mchezo huo wa kwanza, mabao ya Yanga yalifungwa na Prince Dube, Clatous Chota Chama, Clement Mzize na Stephane Aziz KI, ikiwa ni muendelezo wa kiwango bora cha timu hiyo tangu ilipotwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii msimu huu baada ya ushindi wa mabao 4-1, dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC.

MABADILIKO SABA
Kuonyesha Yanga ina ukubwa wa kikosi katika mchezo huo Gamondi amefanya mabadiliko ya wachezaji saba wapya walioanza tofauti na mechi ya kwanza iliyopigwa Agosti 17, kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Maeneo yaliyofanyiwa mabadiliko ni kuanzia eneo la beki wa kati ambapo Dickson Job alianza akichukua nafasi ya Ibrahim Hamad ‘Bacca’ ambaye hakuwa kabisa sehemu ya mchezo huo wa jana.

Gamondi amefanya pia mabadiliko eneo la kiungo ambapo Jonas Mkude na Aziz Andambwile walianza sambamba na Duke Abuya huku Maxi Mpia Nzengeli, Khalid Aucho, Mudathir Yahya na Stephane Aziz KI wakianzia benchi.

Clatous Chama aliendelea kuanza katika kikosi cha kwanza sawa na Pacome Zouzoua ambaye mchezo uliopita alianzia benchi kisha kuingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Maxi Nzengeli.

Mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Prince Dube ameanzia benchi katika mchezo wa jana huku Kennedy Musonda na Clement Mzize wakiongoza safu ya ushambuliaji.

YAVUNA MILIONI 40
Jumla ya mabao 10-0, iliyoyapata Yanga katika michezo yote miwili ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, imeifanya timu hiyo kuvuna kiasi cha Sh35 milioni ikiwa ni kampeni ya ‘Goli la Mama’ inayotolewa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kama motisha ya klabu zetu kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

Katika michuano ya kimataifa msimu huu, Rais, Samia alitangaza kutoa kiasi cha Sh5 milioni kwa kila bao litakalofungwa ikiwa ni muendelezo wa kutoa hamasa kwa klabu zote hapa nchini zinazoshiriki mashindano hayo.

MIKONONI MWA WAHABESHI
Ushindi huu wa Yanga unaifanya kwa sasa kukutana na timu ya Commercial Bank ya Ethiopia katika mchezo wa raundi ya pili kusaka tiketi ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Yanga inakutana na Commercial ambayo imefika hatua hiyo baada ya kuitoa SC Villa ya Uganda kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya kuanza na ushindi ugenini jijini Kampala wa mabao 2-1, huku mchezo wa marudiano uliopigwa pia jana jijini Addis Ababa Ethiopia kulazimishwa sare ya kufungana kwa bao 1-1.

Katika hatua hiyo ya raundi ya pili kusaka tiketi ya kufuzu makundi, Yanga itaanzia ugenini Ethiopia kwenye mchezo wa kwanza utakaopigwa kati ya Septemba 13 hadi 15, kisha kumalizia nyumbani jijini Dar es Salaam kati ya Septemba 20 hadi 22.

VIKOSI
Kikosi cha Yanga kilichoanza ni, Djigui Diarra, Aziz Andambwile/ Stephane Aziz KI, Nickson Kibabage, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Clatous Chama, Jonas Mkude, Clement Mzize/ Prince Dube, Kennedy Musonda/ Mudathir Yahya, Pacome Zouzoua/ Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ na Duke Abuya/ Maxi Mpia Nzengeli.

Kikosi cha Vital’O kilichoanza ni Hussein Ndayishimiye, Amedee Ndavyutse, Abdoul Karim Barandondera, Claude Masiri Luendo, Hussein Ibrahim, Kessy Jordan Nimbona, Yakubu Uwimana, Amissi Leon Irakoze, Autriche Nsanzamateka, Hamissi Harerimana na Prince Michael Musore.

Related Posts