MKOA wa Arusha umeibuka kinara mpya wa riadha taifa baada ya kutwaa medali 21, dhahabu zikiwa 10, fedha tano na shaba sita.
Mshindi wa pili kwenye mashindano hayo yaliyofungwa juzi usiku ni mkoa wa Mjini Magharibi wa Zanzibar uliotwaa medali 13, dhahabu zikiwa saba, fedha na shaba tatu tatu.
Mkoa wa Pwani umehitimisha tatu bora kwenye matokeo ya jumla baada ya kutwaa medali nane, dhahabu tatu, fedha mbili na shaba tatu.
Mikoa mingine iliyoingia 10 bora na idadi ya medali ilizovuna kwenye mabano ni Kilimanjaro (dhahabu 2, fedha nne na shaba nne) na Tabora (dhahabu 1, fedha tatu na shaba mbili.
Dar es Salaam imemaliza ya sita ikiwa na dhahabu moja na shaba moja, Dodoma na wenyeji Mwanza kila moja imevuna shaba mbili na fedha mbili na kumaliza kwenye nafasi ya saba na nane.
Mbeya ambayo iliwakilishwa na mwanariadha mmoja aliyedhaminiwa na mdau wa michezo mkoani huo, Dk Tulia Ackson ilipata fedha mbili na kumaliza ya tisa huku Tanga iliyovuna fedha moja ikihitimisha 10 bora.
Mkoa mwingine uliopata medali ni Mara iliyotwaa shaba moja na kumaliza kwenye nafasi ya 11.
Mkurugenzi wa mashindano hayo, Mhidini Masunzu ameitaja mikoa ya Kagera, Manyara, Morogoro, Shiyanga, Simiyu na Geita kuwa imetoka kapa kwenye mashindano hayo msimu huu.
Akifunga mashindano hayo, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Isangi alisema hamasa ya mwaka huu inakwenda kuleta tija msimu ujao, akisisitiza viongozi wa mikoa kupeleka wachezaji kulingana na kota walizopewa.
“Kuna mikoa imepewa idadi ya wanariadha 10, yenyewe unaleta pungufu hii si sawa, msimu ujao kila mkoa ulete timu kulingana na kota walizopewa na ile ambayo itashindwa kuleta timu kama nilivyosema awali, viongozi wake hawatufai,” alisema.
Katika mashindano hayo Arusha iling’ara kwenye mbio ya mita 10,000 na 5000 kwa wanawake na wanaume, mita 800, relay ya 400 huku Mjini Magharibi ikitamba kwenye mitupo na Pwani iking’ara kwenye mbio fupi na relay ya mita 100.