Kapanga, kijiji cha mfano wa kutumia mapato kuendeleza wanakijiji

Dodoma. Kijiji cha Kapanga mkoani Katavi kilikuwa na matatizo kadhaa ikiwamo, wingi wa vifo vya mama na mtoto, upungufu wa walimu na wakazi wake kutokuwa na bima ya afya.

Ni kijiji chenye wakazi 7,875 lakini hakikuwa na zahanati na kilikabiliwa na upungufu wa vyumba madarasa, walimu na wauguzi. Michango kwa ajili ya huduma za jamii, iliwafanya wanaume kuyakimbia makazi yao kwa kukosa fedha na mitaji.

Kijiji hicho ni miongoni mwa vijiji vinane vinavyozalisha hewa ya kaboni vilivyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi.

Serikali ya Kijiji cha Kapanga imekuwa kilelezo kuhusu umuhimu wa viongozi wanaochaguliwa kutumia fedha za miradi kwa maendeleo ya wananchi.

Wakati wa tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa mkoani Dodoma, vijiji vya Kagunga na Kapanga kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, viliweka banda kuelezea mafanikio yao yaliyotokana na uongozi thabiti.

Fedha za miradi ya maendeleo ni rasilimali muhimu zinazopaswa kutumika kwa uangalifu na kwa malengo mahsusi ili kuboresha maisha ya wananchi.

Viongozi wa kisiasa wanaochaguliwa na watendaji wa Serikali wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya umma, ikiwemo kuimarisha miundombinu, kuboresha huduma za jamii na kukuza uchumi wa nchi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kapanga, Deus Ibrahim anasema kijiji chao ni miongoni mwa vijiji vinane katika halmashauri hiyo vyenye misitu inayozalisha hewa ukaa au kaboni.

Anasema biashara ya kaboni mwanzo iliwaingizia Sh1.3 bilioni ambazo walizutumia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wanakijiji.

Ibrahim anasema fedha hizo walizitumia kujenga zahanati, nyumba ya wauguzi, madarasa mawili kwa shule ya msingi na mengine mawili kwa shule shikizi, pamoja na vyoo.

“Pia, tumewalipia bima ya afya wanakijiji takriban 2,000 ambao walikuwa hawana, tumeanzisha mradi wa kukopesha vikundi vya ujasiriamali na tumeajiri vijana 14 kulinda msitu. Lakini, pia tumeajiri walimu wawili na wauguzi wawili,” anasema Ibrahim.

Anasema pia wametoa Sh100 milioni kwa ajili ya kununua vifaatiba kwenye zahanati waliyoijenga kutokana na mapato ya biashara ya kaboni.

“Mipango ya baadaye tunatarajia kupata Sh40 bilioni kutokana na biashara ya kaboni, tukizipata tutajenga madarasa mengine mawali, ofisi, matundu ya choo na daraja,” anasema Ibrahim.

Kwa upande wake Raheli Yoram ambaye ni mwenyekiti kamati ya mipango na fedha ya kijiji,  anasema mapato ya biashara ya kaboni yameokoa maisha ya wananchi, hasa vifo vya mama na mtoto.

“Zahanati tuliyoijenga imesaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuwa zahanati ilikuwa mbali na mjamzito alilazimka kupelekewa kwa baiskeli kama familia haina nauli ya basi.

“Nauli ya basi ni Sh2, 000 kwenda na kurudi ni Sh4, 000, hapo bado hela ya chakula, lakini zanahati imesaidia kupunguza shida hiyo,” anasema Joram ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa zahanati na madarasa.

Anasema mapato hayo ya biashara ya kaboni yameondoa michango ya wananchi kwa ajili ya maendeleo ya kijiji, ambao kila baada ya miezi sita walitakiwa kuchanga Sh15,000.

“Michango hii ilisababisha wanaume wakimbie miji, lakini sasa imeondolewa na miradi yote ya maendeleo inagharamiwa na mapato ya biashara ya kaboni,” anasema.

Anasema kutokana na usimamizi mzuri wameweza kutoa chakula cha mchana kwa watoto wanapokuwa shuleni na mikopo inayowezesha wananchi kiuchumi.

Umuhimu wa matumizi sahihi

Fedha za miradi ya maendeleo zinapopelekwa kwenye kuboresha miundombinu kama vile barabara, shule, hospitali na miundombinu ya maji na umeme, zinaboresha maisha ya wananchi.

Barabara nzuri, kwa mfano, zinasaidia kupunguza gharama za usafiri na muda wa kusafiri, hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kama vile matibabu na elimu.

Vivyo hivyo, kuboresha huduma za afya na elimu kunachangia kuongeza ustawi wa jamii kwa kupunguza magonjwa na kuongeza kiwango cha elimu miongoni mwa wananchi.

Pia, miradi ya maendeleo inayolenga kuongeza ajira na kujenga uwezo wa kiuchumi kwa wananchi, ina mchango mkubwa katika kupunguza umaskini.

Viongozi wanapowekeza kwenye miradi inayolenga kukuza sekta kama kilimo, biashara ndogondogo, na viwanda, wanatoa fursa za ajira na hivyo kuongeza kipato cha wananchi.

Hii inasaidia kupunguza utegemezi na kuongeza uwezo wa watu kujitegemea kiuchumi. Kwa mfano, miradi ya kilimo inayofadhiliwa na Serikali inaweza kuwasaidia wakulima kupata pembejeo bora, mafunzo na masoko na hivyo kuongeza uzalishaji na kipato chao.

Viongozi wanapojitahidi kutumia fedha za miradi kwa maendeleo ya wananchi, wanajenga utamaduni wa uwajibikaji na uadilifu ndani ya taasisi za Serikali.

Uwajibikaji huu unahakikisha kwamba rasilimali za umma zinatumika ipasavyo na kwa malengo yaliyokusudiwa, na hivyo kuzuia matumizi mabaya ya fedha.

Pia, uwajibikaji na uadilifu huongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao, kwani wanajua kwamba viongozi wao wanazingatia masilahi ya umma na si masilahi yao binafsi.

Kutumia fedha za miradi kwa maendeleo ya wananchi pia ni sehemu ya kuimarisha demokrasia na utawala bora.

Wananchi wanapoona miradi ya maendeleo ikitekelezwa vizuri na kwa uwazi, wanapata motisha ya kushiriki katika shughuli za maendeleo na hata katika michakato ya kisiasa kama vile uchaguzi na kuhakikisha wanapata viongozi bora watakaosimamia vizuri fedha zao.

Utawala bora unahitaji wananchi kushiriki kikamilifu na kutoa maoni yao juu ya jinsi wanavyotaka kuona maendeleo katika maeneo yao.

Kwa kutumia fedha za miradi kwa njia sahihi, viongozi wanachochea ushiriki wa wananchi na hivyo kuimarisha demokrasia ya nchi na ustawi wa wananchi.

Kwa mfano, miradi ya maji safi na salama inaweza kupunguza vifo vya watoto na magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji machafu.

Vivyo hivyo, miradi ya afya inayolenga kujenga na kuboresha hospitali na vituo vya afya inaweza kuongeza upatikanaji wa huduma za afya, hasa kwa watu wanaoishi vijijini na maeneo ya mbali.

Miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha miundombinu na mazingira ya kibiashara inaweza kuchochea uwekezaji wa ndani na nje.

Miundombinu bora kama barabara, umeme, na maji ni kichocheo kikubwa cha uwekezaji, kwani wawekezaji wanahitaji uhakika wa upatikanaji wa huduma hizi ili kuendesha biashara zao kwa ufanisi.

Wananchi wanapopata maendeleo kupitia miradi inayofadhiliwa na fedha za umma, nchi inakuwa na nafasi nzuri zaidi ya kushirikiana na jamii ya kimataifa.

Ushirikiano huu unaweza kuleta manufaa kama vile misaada ya kifedha na kiufundi, mikopo nafuu, na fursa za masoko kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.

Viongozi wanapojitahidi kutumia fedha za miradi kwa maendeleo ya wananchi, wanajenga taswira nzuri ya nchi yao na hivyo kuvutia misaada na ushirikiano kutoka kwa nchi rafiki na mashirika ya kimataifa na pia wanazuia mianya ya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma.

Kwa kuweka mifumo mizuri ya udhibiti na usimamizi wa fedha, pamoja na kuwa na uwazi na uwajibikaji, viongozi wanaweza kuhakikisha kwamba fedha za miradi zinatumika ipasavyo na zinanufaisha wananchi.

Maendeleo ya kiuchumi, kijamii yanayopatikana kutokana na matumizi sahihi ya fedha za miradi yanaweza kusaidia kukuza amani na utulivu wa kijamii.

Wananchi wanapopata huduma bora, ajira na fursa za kiuchumi, wanakuwa na sababu ndogo ya kushiriki katika machafuko au migogoro ya kijamii.

Vivyo hivyo, matumizi sahihi ya fedha za miradi yanaweza kusaidia kupunguza tofauti za kijamii na kiuchumi miongoni mwa wananchi, na hivyo kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kudumisha amani.

Related Posts