MIAKA inaenda kwa kasi sana. Na asikuambie mtu, kuna wakati mtu unaweza kukufuru kwa jinsi maisha ya hapa duniani yanavyotatiza. Maisha yanakatisha tamaa mno. Yaani kama sio kuumbwa kwa sahau, walahi hakuna ambaye angeweza kufanya jambo lolote la maana.
We fikiria tu, mtu unasoma au kujilimbikizia mali kwa kujenga majumba, kununua magari ama kuzaa watoto na kugombea madaraka na vyeo. Tena ukiwa amejaa kiburi cha fedha na umaarufu kwa ajili ya nini, kama hatma ya maisha na mbwembwe zote hizo ni kifo?
Maisha ya dunia ni mafupi na yanayodanganya sana, ila ndivyo hivyo tena hatuna ujanja maadamu tumezaliwa na kujikuta tunaishi. Fikiria tu katika umri ulionao umewasindikiza wangapi makaburini, jenga picha wameondoka na umri gani na nafasi gani walizokuwa nazo katika jamii? Wapo wenye umri mdogo hata maisha yenyewe hawajayafaidi wameondoka ghafla tu. Kuna matajiri na waliokuwa wakitetemesha kwa fujo zao, wapo wapi? Kadhalika kuna watu waliotegemewa na familia, koo, jamii na taifa kwa ujumla, nao wapo wapi?
Wameondoka wangali michango yao ikihitajika katika sehemu husika, kama ambavyo mashabiki wa soka wanavyomisi maujuzi ya kina Hamis Thobias Gaga ‘Gagarino’, Said Mwamba ‘Kizota’, Method Mogella ‘Fundi’, Ramadhani Lenny na mafundi wengine waliotamba eneo la kiungo.
Juzi kati nikiwa napiga stori mbili tatu na mshkaji wangu mmoja mitaa ya Magomeni alimzungumzia Pacome Zouzoua wa Yanga, akidai amerudi upya kikosini tangu alipokuwa majeruhi na kukosa mechi kadhaa za katikati ya msimu uliopita akiwa na kikosi hicho cha Jangwani. Alisema Pacome wa sasa ndiye yule aliyewafanya Yanga wakavunja benki na kumng’oa ASEC Mimosas ya Ivory Coast. Pacome aliyemaliza msimu wa 2022-2023 kama MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast.
Nilimbishia na kudai Pacome wa Asec alikuwa habari nyingine. Mjadala ulikuwa mrefu sana, lakini mwishowe tukakubaliana kwamba, kinachofanya tumjadili Pacome na nyota wengine wa kigeni wanaocheza eneo la kiungo ni kutokana na kuwakosa mafundi wazawa wa eneo hilo kwa sasa.
Tulikubaliana tunawa-misi watu kama kina George Lucas ‘Gazza’, Hussein Marsha, Mao Mkami ‘Ball Dancer’, Athuman Abdallah ‘China’, Dadi Athuman na wengine. Ndipo wote tukajikuta tukiwakumbuka kina Gagarino na wenzake waliotangulia mbele ya haki. Udongo umefukia mafundi wa mpira buana! Zile burudani ambazo zinawafanya wadau wamjadili Pacome, James Akaminko, Marouf Tchakei, Duke Abuya, Augustine Okejepha kama sio Debora Mavambo na wakati mwingine tukipagawa na kazi tamu za Clatous Chama ama Feisal Salum ‘Fei Toto’ zinatokana na kuwakosa watu waliojua kuuchezea mpira kama kina Gaga.
Kwa wale waliomuona Gaga na hata Kizota enzi za ubora wao watakubali kwamba, kwa aina ya viungo waliopo sasa hakuna anayefikia angalau nusu ya uwezo waliokuwa nao mafundi hao. Walikuwa wanajua kuurahisisha mpira. Waliburudisha na pia kuzipa timu matokeo uwanjani.
Hata hivi majuzi tu, kiungo wa zamani wa Simba, Nico Njohole amekiri kwa sasa hakunja viungo watoa burudani na wanaosisimua kama ilivyokuwa zamani. Yusuf Macho ‘Musso’ mmoja ya wakali wa eneo hilo naye aliwahi kunukuliwa akisema kama hivyo, huku huku akiwataja Haruna Niyonzima na Salum Abubakar kwamba angalau kidogo waliokuwa wakionekana bora kuliko wengine. Niyonzima aliwahi kucheza Simba na Yanga kabla ya kurudi kwao Rwanda, huku Sure Boy wakati akipewa ujiko huo alikuwa Azam FC kabla ya sasa kuhamia Yanga kwa msimu wa tatu sasa.
Macho kitaaluma ni kocha mbali na uzoefu wake. Na hakuna asiyejua uwezo aliokuwa nao nyota hiyo wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars. Hivyo kauli yake inatoa picha kwamba Tanzania baada ya kuwa kwenye uhaba mkubwa wa kuwa na washambuliaji halisi, sasa tunaelekea kwenye viungo fundi.
Sio kama viungo wazuri hawapo la, wapo kweli na wanafanya kazi kubwa uwanjani, lakini hakuna warembaji ambao wanaweza kuwafanya mashabiki watoke majumbani kwao wakiwa na hamu ya kwenda kulipa kiingilio ili washuhudie mambo mawili kwa wakati mmoja. Yaani kuona soka la nguvu na pili kupata burudani kama waliokuwa wakiitoa kina Kizota, Gagarino, Lenny, China, Chambua, Dadi na wenzao kadhaa baadhi wakiwa hai na wengine wakiwa wametangulia mbele ya haki.
Leo Chama aliyekuja nchini akiwa umri umeshamtupa na hata Pacome, Stephane Aziz KI wamekuwa wakitukuzwa. Wamekuwa wakiimbwa na mashabiki, wakati vijana wazawa wenye vipaji na uwezo mkubwa wa kumiliki eneo la kati wakizidi kutoweka. Yu wapi Mohamed Ibrahim yule wa Mtibwa Sugar ambaye amepotelea kwenye benchi la Msimbazi?
Ebu niache kuzungumza viungo wachezeshaji, hata wale wakabaji nao wamekuwa na homa ya vipindi. Jonas Mkude, alitarajiwa kuja kuwa Lenny Ramadhani wa zama hizi, hasomeki. Mudathir Yahya, Mzamiru Yasin, Yusuf Kagoma, Aziz Andambwile na wengine bado hawasomeki.
Kwanini kina Pacome asijadiliwe mitaani? Kwa nini Chama asipewe ufalme? Sure Boy wa Azam alikuwa akitamanisha, lakini ghafla tumeanza kumsahau, kwa vile ndani ya Yanga kuna mafundi zaidi wa nafasi anayoicheza. Ni kama ilivyo kwa Mudathir Yahya, anakufurahisha mechi moja anakuudhi mechi inayofuata. Kulikuwa na mtu kama Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Athuman Idd ‘Chuji’ kama wangeamua kujikita kwenye soka badala ya mambo mengine, wangekuwa mbali sana. Walikuwa wakipita njia zilezile walizopita kina Gaga na Lenny kabla ya kuchepuka na wamestaafu bila kujadiliwa kama wanavyojadiliwa kina Pacome, Aziz KI na Debora kama si Tchakei, Akaminko James na wegineo wa kigeni.
Imefika wakati nyota wazawa wa Kitanzania kujitathmini juu ya vipaji walivyonavyo, umri na kazi wanazozifanya uwanjani kama zinalingana! Kwani ni jambo la aibu kina Chama walioanza kuchoka wanaendelea kutamba na wao wanapotea. Leo Chama aliyepunguza makali, eti anaimbwa midomoni, ilihali kuna mayanki kibao wenye uwezo mkubwa wa kusukuma ndinga pale kati wakiwa wameridhika!
Wengi tulitamani na kuwatabiria kina Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Hassan Dilunga, Mkude na wengine wangekuwa moto kwa vipaji walivyokuwa navyo. Lakini mambo yamebadilika.
Inashangaza tu kama inavyoshangaza katika eneo la ushambuliaji kwa nyota wa kigeni kuendelea kutamba kuliko wazawa. Miaka michache kina Meddie Kagere, Amissi Tambwe, Emmanuel Okwi ambao umri ulikuwa umesonga mbele waliwakimbiza kina Atupele Green, Habib Kyombo, Reliants Lusajo, Jeremia Juma na wengine kwa ufungaji mabao. Wazawa wenye damu changa walikubali unyonge na hata sasa kuendelea kuwa wanyonge mbele ya wageni ambao umri umewatupa mkono.
Inawezekana kuna mahali kama nchi tunakosea. Lakini kwa teknolojia iliyopo, vijana wanaweza kujifunza na wakitia juhudi wanaweza kutoboa.