Mashabiki Simba SC waitwa KMC Complex… “Njooni mhesabu”

MASHABIKI wa Simba mzuka umewapanda baada ya kupata uhakika kwamba straika mpya wa timu hiyo, Lionel Ateba leo ataliamsha kwa mara ya kwanza akiwa na uzi wa kikosi hicho kwenye Uwanja wa KMC katika pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate.

Mechi hiyo ya raundi ya pili kwa Simba na mchezo wa kwanza kwa Fountain Gate, utapigwa kuanzia saa 10:00 jioni, huku mashabiki wa Msimbazi bila ya shaka wakiwa na kiu ya kutaka kuhesabu zaidi mabao na pointi baada ya awali timu hiyo kuanza msimu kwa kishindo ilipoinyoa Tabora United kwa mabao 3-0.

Baada ya kukosa mchezo huo wa kwanza dhidi ya Tabora kwa sababu za kiutawala, Ateba ana nafasi kubwa ya kutumika leo katika mechi hiyo Fountain kwa vile ameshapata vibali vyote vinavyomhalalisha kutumika kwa mechi za ligi na michuano mingine, ikiwa ni wiki chache tangu asajiliwe kutoka USM Alger ya Algeria.

Straika huyo Mcameroon alisajiliwa na Simba katika siku za mwisho za dirisha la usajili baada ya mapendekezo ya haraka na ghafla ya kocha mkuu, Fadlu Davids ambaye alionyesha kutokuridhishwa na viwango vya washambuliaji wawili wa kati aliowakuta, Steven Mukwala na Freddy Koublan aliyeondoka.

Na hilo lilipelekea mabosi wa Simba kuingia msituni fasta na kumwaga zaidi ya Sh 500 milioni kwa USM Algera kwa ajili ya kuishawishi iwauzie Ateba jambo ambalo lilikubalika na sasa nyota huyo aliyekuwemo katika kikosi cha Cameroon kilichoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zilizofanyika Ivory Coast mwanzoni mwa mwaka huu.

Wageni Fountain Gate ndio wanaanza kuonja ladha ya Ligi Kuu Bara msimu huu kwa vile walishindwa kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Namungo FC mwishoni mwa wiki iliyopita kwa vile wachezaji wake hawakuwa wamesajiliwa kutumika kwenye ligi.

Sababu ya wachezaji hao kutoingizwa kwenye mfumo wa usajili ni adhabu ya kufungiwa ambayo Fountain Gate ilikuwa ikiitumikia kutokana na kuchelewa kufanya malipo ya stahili ya mchezaji wake wa zamani, Rodrigo kutoka Brazil.

Hata hivyo, juzi Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) liliiondolea Fountain adhabu hiyo jambo lililoihakikishia kukamilisha mchakato wa usajili wa wachezaji, hivyo kuwa na uhalali wa kikanuni kushiriki Ligi.

Simba imekuwa na historia nzuri mbele ya Fountain Gate ambapo haijawahi kupoteza mchezo wowote dhidi ya timu hiyo pindi zilipokutana katika Ligi Kuu apo nyuma wakati huo Fountain Gate ikiitwa Singida Big Stars kisha Singida Fountain Gate.

Kumbukumbu zinaonyesha timu hizo zimekutana mara nne katika Ligi Kuu ambapo Simba imeibuka na ushindi mara tatu na mechi zilitoka sare na mabao yaliyofungwa katika mechi hizo ni 13, Simba ikifunga tisa na Fountain yenyewe ikipata mabao manne tu.

Katika hali ya kushangaza wachezaji waliofunga mabao yote 13 katika mechi baina ya timu hizo mbili hawapo kwenye vikosi vyao msimu huu hivyo leo ni zamu kwa wengine wapya kuingia katika historia hiyo.

Mabao tisa ya Simba dhidi ya Fountain enzi za Singida hapo mwanzo, yalifungwa na Saido Ntibazonkiza ambaye ana manne huku mengine matano yakifungwa na Peter Banda, Jean Baleke, Freddy Koublan, Pape Sakho na Moses Phiri ambao wote kwa sasa hawapo ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi.

Kwa Fountain Gate, mabao yake manne yalifungwa na Deus Kaseke ambaye ana mawili na Bruno Baroso na Thomas Ulimwengu kila mmoja amefunga bao moja.

Ushindi kwa Fountain utawafanya kuwa na mwanzo mzuri katika Ligi lakini hapana shaka utawaondolea nuksi waliyomaliza nayo msimu uliopita ya kutofanya vizuri ambapo katika mechi tano za mwisho, walipata ushindi mara moja tu, sare moja na kupoteza tatu.

Simba yenyewe inaingia ikiwa na takwimu bora katika mechi zilizopita za Ligi Kuu ambapo haijapoteza mechi 10 mfululizo zilizopita za Ligi ikishinda nane na kutoka sare mbili.

Katika mchezo wa leo, Simba itamkosa winga, Joshua Mutale anayeuguza majeraha ya nyama za paja aliyoyapata katika mchezo uliopita dhidi ya Tabora Utd na atakosekana kwa muda wa wiki mbili.

Hata hivyo, uwepo wa Kibu Denis ambaye aliongeza chachu kwa Simba katika mechi iliyopita baada ya kuingia akitokea benchi hapana shaka kunamuondolea wasiwasi kocha Fadlu Davids kwenye uteuzi wa mchezaji atakayeziba nafasi yake.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema kuwa anaamini mchezo utakuwa mgumu lakini watahakikisha wanapata ushindi.

“Fountain Gate ni timu nzuri sana ambayo imejitengeneza vizuri kwenye ulinzi. Tumejiandaa vizuri lakini tunawachukulia kwa uzito mkubwa na tunawaheshimu kama timu nzuri na tumejiandaa kama siku zote kwa ajili ya kuchukua pointi tatu.

“Nafurahishwa na njia zetu za kutengeneza nafasi na kufungua wapinzani. Tunataka kuwa na aina ya uchezaji wa haraka. Nina uhakika Fountain Gate watakuja kucheza nyuma lakini sio kwa ilivyokuwa kama mechi iliyopita,” alisema Davids.

Kwa upande wa kocha wa Fountain Gate, Mohammed Muya alisema wako tayari kuumana na Simba leo

“Wachezaji wetu wako na afya njema. Tumefanya vizuri mazoezi yetu yameziba sehemu zote ambazo tulikuwa tunahitaji kuzifanyia kazi kwa ajili ya kwenda kukutana nao Simba hapo kesho (leo). Tunahiheshima Simba ni timu kubwa, ina uwekezaji mkubwa lakini na sisi ni timu kubwa na tuna uwekezaji mzuri.

“Kwa maandalizi tuliyopewa na uongozi wetu na morali waliyokuwa nayo wachezaji wetu umoja wao, usikivu wao na ushirikiano wanaotupa sisi benchi la ufundi tuna imani tunaenda kupata mchezo mzuri sana, Watanzania wote watapata burudani wanayoitarajia,” alisema Muya.

Baada ya mchezo huo wa Simba na Fountain Gate, kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi kuanzia saa 1:00 usiku kutakuwa na mchezo baina ya wenyeji Namungo FC na Tabora United.

Huo ni mchezo wa kwanza kwa wenyeji Namungo baada ya kushindwa kucheza dhidi ya Fountain Gatewiki iliyopita kwa sababu zilizoelezewa hapo juu.

Tabora United itakuwa ikisaka ushindi wa kwanza baada ya kuanza vibaya kwa kichapo cha mabao 3-0 walichokipata kutoka kwa Simba kwenye mechi ya kwanza.

Hapana shaka mashabiki wa soka wataanza kuziona sura nyingi mpya ambazo zimesajiliwa na timu hizo kwenye dirisha kubwa la usajili.

Kwa upande wa Namungo FC, wachezaji wapya amabo wanaweza kuonekana leo ni Beno Kakolanya, Djuma Shaban, Erick Kapaito, Amade Momade, Geofrey Julius, Moubarack Hamza na  Rafael Lothi.

Tabora United leo inaweza ikawatumia Heritier Makambo na Yacouba Songne ambao walikosa mechi ya kwanza dhidi ya Simba.

Related Posts