Mashindano ya Kitesurfing kuvutia utalii wa michezo Zanzibar

Zanzibar. Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Dk Aboud Jumbe amesema mashindano ya Kitesurfing yanatarajia kuwa chachu ya kukuza utalii wa michezo visiwani humo.

Dk Jumbe ameyasema hayo Jumamosi Agosti 24, 2024 akihutubia katika mashindano ya ‘Zanzibar Cup Kusi 2024’ yaliyofanyika Kiwengwa visiwani humo huku yakihudhuriwa na washiriki kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Austria, Italia, Afrika Kusini, Uingereza, Poland, Czech Republic, Hispania na Tanzania.

“Mashindano haya (Zanzibar Cup Kusi 2024), yanatarajiwa kuvutia washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, huku yakiwa na lengo la kukuza utalii wa michezo na kuvutia watalii zaidi kwenye visiwa vyetu.

Kitesurfing ni mchezo ambao unalingana vyema na mandhari yetu ya fukwe na mazingira ya kuvutia ya pwani ya Zanzibar,” amesema Dk Jumbe.

Aidha, katika mashindano hayo mshindi wa kwanza alikuwa Jacopo Cantini kutoka Italia alipata Dola za Marekani 3,000 (Sh 8 milioni), mshindi wa pili alikuwa Suleiman Abdallah kutoka Paje visiwani Zanzibar alishinda Dola za Marekani 1,000 (Sh 2.7 milioni), mshindi wa tatu alikuwa Seif Shaaban kutoka Kiwengwa visiwani humo akishinda Dola za Marekani 500 (Sh1.3 milioni).

Nafasi ya nne ilikamatiwa na Khamis Suleiman Pandu naye kutokea Kiwengwa alishinda Dola za Marekani 300 (Sh806,548).

Pia, Dk Jumbe aliwashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha mashindano hayo ya kimataifa ambayo kwa Zanzibar yanafanyika mara ya pili.

“Tunamshukuru sana Stefano Conte kutoka Italia kwa kuratibu mashindano haya kwa mara nyingine tena, pamoja na wadhamini wetu wakuu Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Melia Zanzibar, RIU Hotel, Verde Hotel, na Rasello. Pia tunawashukuru Neptune Beach Resort and Spa, Kiwengwa Beach Resort, Tui Blue, Zanzibar Serena Hotel, Park Hyatt Zanzibar, na Bawe Island kwa kusaidia kuwezesha mashindano haya.

“Vile vile, tunashukuru ushirikiano kutoka kwa wadau kama Ofisi ya Rais PDB, ZATI, ZATO, HAZ, Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, Ubalozi wa Italia nchini Tanzania, na Chama cha Kite Surfing Zanzibar kwa ushirikiano wao mkubwa katika kufanikisha tukio hili,”amesema na kuongeza.

Related Posts