Russia, Ukraine zabadilishana wafungwa wa vita 230

Russia. Russia na Ukraine zimefikia makubaliano ya kubadilishana wafungwa wa vita 115 kila upande, katika mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE iliyotolewa Jumamosi Agosti 24, 2024, UAE imesaidia kufanikisha mabadilishano haya, ambayo ni matokeo ya mikutano saba ya majadiliano kati ya pande hizo kwa mwaka huu.

Tovuti ya Al-Jazeera imeripoti kuwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy amethibitisha kuachiliwa kwa wapiganaji 115 wa Russia, huku Russia nayo ikitangaza kuwa wapiganaji wake 115 waliokuwa wametekwa katika ukanda wa Kursk wamerudishwa mikononi mwa vikosi vya Ukraine.

Tangu kuanza kwa vita hiyo miaka miwili iliyopita, pande zote zimekuwa zikifanya mabadilishano ya wafungwa wa vita, licha ya kutokuwepo kwa dalili za kurejesha amani kati yao.

Mabadilishano haya ni ya kwanza kufanyika tangu Ukraine ilipofanya shambulizi la ghafla katika eneo la Kursk mnamo Agosti 6, 2024.

Katika mabadilishano makubwa yaliyowahi kuripotiwa kati ya pande hizo mbili, mnamo Januari 3, 2024, mataifa haya mawili yalibadilishana wafungwa 478 kupitia mazungumzo yaliyosimamiwa na UAE.

Taarifa ya UAE imeeleza kwa jitihada zake, mataifa haya yameshabadilishana takriban wafungwa 1,788 tangu kuanza kwa vita hiyo.

Zelenskyy ameongeza kuwa miongoni mwa wafungwa waliorejeshwa na Russia ni askari wa taifa, askari wa mpakani, jeshi la ulinzi la taifa na wanamaji.

Ameongeza kuwa serikali inaendelea na juhudi za kuwarudisha nyumbani askari waliobaki.

Kamishna wa Haki za Binadamu wa Ukraine, Dymtro Lubinets, amesema askari 82 wa Ukraine waliorejeshwa ni wale waliokamatwa wakati wa uvamizi wa kwanza wa Russia katika eneo la Mariupol mwaka 2022.

Mabadilishano haya yalifanyika siku moja kabla ya Ukraine kusherehekea miaka 33 ya uhuru wake kutoka kwa utawala wa Russia, ingawa mvutano kati ya nchi hizo unaendelea.

Katika sherehe hizo, Zelenskyy amesema, “Russia ilijaribu kuidhoofisha Ukraine, lakini ushindi umerudi nyumbani.”

Shambulio la Ukraine katika eneo la Kursk linatajwa kuwa moja ya mashambulio makubwa dhidi ya Russia tangu kuanza kwa vita hiyo mwaka 2022.

Hata hivyo, Russia inaendelea na uvamizi wake katika maeneo ya mashariki mwa Ukraine.

Endelea kufuatilia Mwananchi Digital kwa habari zaidi.

Related Posts