Simba, Fountain Gate na mwanzo mpya

Dar es Salaam. Historia ya nyuma itazikwa rasmi na leo Simba na Fountain Gate zitaanzisha rasmi ushindani mpya kwenye Ligi Kuu wakati zitakapokutana kwenye Uwanja wa KMC Complex,Mwenge, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.

Mabadiliko ya jina na uendeshaji ambayo Fountain Gate imeyafanya msimu huu yanaipa fursa ya kufuta unyonge wa nyuma ambao ilikuwa nao dhidi ya Simba wakati ilipokuwa ikiitwa kwa jina lingine ambalo sasa halipo tena hivyo ushindi wao ugenini leo utakuwa ni ishara tosha kuwa yaliyopita si ndwele na wameamua kuganga yajayo.

Simba imekuwa na historia nzuri mbele ya Fountain Gate ambapo haijawahi kupoteza mchezo wowote dhidi ya timu hiyo pindi zilipokutana katika Ligi Kuu apo nyuma wakati huo Fountain Gate ikiitwa Singida Big Stars.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba timu hizo zimekutana mara nne katika Ligi Kuu ambapo Simba imeibuka na ushindi mara tatu na mechi zilitoka sare na mabao yaliyofungwa katika mechi hizo ni 13, Simba ikifunga tisa na Fountain Gate yenyewe ikipata mabao manne tu.

Ushindi kwa Fountain Gate utawafanya kuwa na mwanzo mzuri katika Ligi lakini hapana shaka utawaondolea nuksi waliyomaliza nayo msimu uliopita ya kutofanya vizuri ambapo katika mechi tano za mwisho, walipata ushindi mara moja tu, sare moja na kupoteza tatu.

Simba yenyewe inaingia ikiwa na takwimu bora katika mechi zilizopita za Ligi Kuu ambapo haijapoteza mechi 10 mfululizo zilizopita za Ligi ikishinda nane na kutoka sare mbili.

Katika mchezo wa leo, Simba itamkosa winga wake Joshua Mutale ambaye anauguza majeraha ya nyama za paja aliyoyapata katika mchezo uliopita dhidi ya Tabora United na atakosekana kwa muda wa wiki mbili.

Wageni Fountain Gate ndio wanaanza kuonja ladha ya Ligi Kuu Bara msimu huu kwa vile walishindwa kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Namungo FC mwishoni mwa wiki iliyopita kwa vile wachezaji wake hawakuwa wamesajiliwa kutumika kwenye ligi.

Sababu ya wachezaji hao kutoingizwa kwenye mfumo wa usajili ni adhabu ya kufungiwa ambayo Fountain Gate ilikuwa ikiitumikia kutokana na kuchelewa kufanya malipo ya stahili ya mchezaji wake wa zamani, Rodrigo kutoka Brazil.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema kuwa anaamini mchezo utakuwa mgumu lakini watahakikisha wanapata ushindi.

“Fountain Gate ni timu nzuri sana ambayo imejitengeneza vizuri kwenye ulinzi. Tumejiandaa vizuri lakini tunawachukulia kwa uzito mkubwa na tunawaheshimu kama timu nzuri na tumejiandaa kama siku zote kwa ajili ya kuchukua pointi tatu,” alisema Davids.

Kocha wa Fountain Gate, Mohammed Muya alisema kwa upande wao wako tayari kuumana na Simba leo

“Wachezaji wetu wako na afya njema. Tumefanya vizuri mazoezi yetu yameziba sehemu zote ambazo tulikuwa tunahitaji kuzifanyia kazi kwa ajili ya kwenda kukutana nao Simba hapo kesho (leo). Tunahiheshima Simba ni timu kubwa, ina uwekezaji mkubwa lakini na sisi ni timu kubwa na tuna uwekezaji mzuri,” alisema Muya.

Baada ya mchezo huo wa Simba na Fountain Gate, kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi kuanzia saa 1:00 usiku kutakuwa na mchezo baina ya wenyeji Namungo FC na Tabora United.

Related Posts