Rorya. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa jumla ya Sh30 milioni kama rambirambi kwa familia zilizopoteza watoto sita kwenye bwawa la skimu ya umwagiliaji katika kijiji cha Ochuna wilayani Rorya, huku mashuhuda wakisimulia kilichotokea.
Watoto hao wa kike walifariki dunia jana Agosti 24, 2024 jioni baada ya kuzama na kunasa kwenye tope katika bwawa hilo wakati wakiogelea.
Akitoa salamu za Rais Samia na kukabidhi fedha hizo kwa familia, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amesema Rais amesikitishwa na tukio hilo na yupo pamoja nao katika wakati mgumu wa maombolezo.
“Yeye kama Rais, mzazi na mlezi amesikitishwa sana na tukio hili ambalo limehusisha watoto wenye umri kati ya miaka 12 hadi 9 wakiwa ni wanafunzi, ambao kwa vyovyote walikuwa na ndoto zao zikiwamo za kulitumikia Taifa,” amesema Chikoka.
Amesema kutokana na msiba huo Serikali ya wilaya itaratibu mazishi ya watoto hao yanayotarajiwa kufanyika kati ya Jumanne au Jumatano wiki hii, ambapo hivi sasa miili imehifadhiwa katika Hospitali ya Utegi wilayani humo.
“Tumewaambia wana familia wajadiliane lakini sisi tunataka ikiwezekana tufanye shughuli ya kuwaaga kwa pamoja siku ya Jumanne au Jumatano,” amesema.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ochuna, Erick Nyagandi amesema chanzo cha tukio hilo ni mtoto mmoja aliyekuwa akiogelea kuanza kumkimbiza bata majini.
Amesema wakati mtoto huyo akiogelea bata maji alitua bwawani humo na kisha mtoto huyo kuanza kuogelea akimfuata na akajikuta amefika kwenye kina kirefu chenye matope.
“Akaanza kuzama ndipo alipoanza kupiga kelele na watoto wenziye ambao waliingia majini na kuanza kumfuata alipokuwa na wao bila kujua hatari iliyokuwepo wakajikuta wanazama mmojammoja hadi wakafika sita,” amesema.
Amesema awali kabla ya tukio kutokea eneo hilo lilikuwa na watoto 13 waliokuwa wakiogelea na wengine wakifua, ambapo baada ya muda sita walimaliza kufua na kuondoka eneo hilo, huku wakiwaacha wenzao saba katika eneo hilo.
“Walibakia saba na waliozama ni sita huyu wa saba yeye aliogopa kuingia majini na ndio chanzo cha watu kujua nini kimetokea, wanakijiji walifika eneo la tukio kwa haraka, lakini bahati mbaya watoto wote hatukufanikiwa kuwakuta hai,” amesema.
Amesema tukio kama hilo liliwahi kutokea mwaka 2004 ambapo watoto wawili walizama na kufariki dunia kwenye bwawa hilo, ambalo mbali na kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji pia ni chanzo cha maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
“Hapa kijijini tuna mabwawa mawili ambayo yote yanatumika kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na umbali wa kutoka hapa kwenye miji ilipotokea misiba hadi bwawani ni kama kilomita mbili,” amesema.
Nyagandi amesema kufuatia tukio hilo uongozi wa kijiji hicho umependekeza maziko ya watoto hao yafanyike kwa wakati mmoja, ili kutoa nafasi kwa wanakijiji kushiriki kikamilifu kwenye tukio hilo.
“Lakini tumeomba kama inawezekana kwa sababu wote ni wanafunzi wa hapa shule itenge eneo dogo kwa ajili ya kuwazika watoto ili iwe kumbukumbu kwa kijiji chetu,” amesema.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ochuna, Richard Gasper amesema wanafunzi waliohusika katika tukio hilo ni wa kuanzia darasa la tatu hadi la sita huku wengi wao wakiwa ni miongoni mwa waliokuwa wanafanya vizuri kitaaluma.
“Darasa la sita amefariki mmoja, la tano mmoja la nne wawili na la tatu wawili, kwa kweli hili ni pigo kubwa sana kwa jumuiya ya Ochuna Shule ya Msingi lakini pia nitoe shukrani na pongezi kwa mkuu wetu wa wilaya kwa namna alivyoshirikiana na sisi tangu jana hadi sasa.”
“Hawa wanafunzi wawili wa darasa la tatu tangu wameanza shule hapa walikuwa wanashindania namba moja na mbili, mmoja wa la nne tangu ameanza shule yeye ni namba moja, huyu wa la tano pia ni namba moja hadi anafikia hapo,” amesema.
Amewataja wanafunzi waliofariki kuwa ni Suzana Mwita na Unice Okumbe wote wa darasa la tatu, Elizabeth Okumbe na Pendo Nyasanda wote wa darasa la nne.
Wengine ni Anjelina Suke wa darasa la tano na Evaline Sylvanus wa darasa la sita.
Wakielezea namna tukio lilivyotokea baadhi ya wazazi wa watoto hao wamesema walifika eneo la tukio baada ya kusikia yowe bila kujua tukio lilihusu nini.
“Mimi nilisikia kelele nikamuuliza jirani yangu kuna nini akasema kuna watoto wamezama ila sijui ni watoto wa nani, tukaondoka kuelekea bwawani ile nafika nakuta mwili wa mwanangu ndio unaopolewa,” amesema Anna Joseph mzazi wa Anjelina.
Amesema siku ya tukio mtoto wake akiwa na mtoto wa jirani yao walikuwa wanatoka kanisani, walipofika kwenye bwawa hilo wakakuta wenzao wanaogelea nao wakaamua kwenda kuwashuhudia wenzao.
Amesema binti yake huyo ambaye alikuwa anashika namba moja shuleni hakuwa na tabia ya kuogelea, siku zote alikuwa akifuata maji bwawani na kuja kuogea nyumbani.
“Siku zote mwanangu Anjelina alikuwa akienda bwawani anachota maji na kuja kuoga nyumbani na hata jana yeye hakuwa ameingia kuogelea ila aliingia kumuokoa rafiki yake Pendo ndipo wakazama wote na miili yao ilikutwa sehemu moja,” ameeleza.
Christina Mangaranya amesema mwanaye Pendo Nyasanda alifariki baada ya kuzama na kuibuka mara mbili akiwa kwenye harakati za kujiokoa.
“Alipoona anazidiwa akapiga kelele ndipo rafiki yake Anjelina akajitosa majini kwenda kumuokoa, bahati mbaya wakazama na kufariki pamoja. Wote walikuwa wanatoka kanisani wakaenda hapo kuwaona wenzao ambao wengine walikuwa wanafua na wengine wakiogelea,” amesema.
Sheba Emmanuel amesema familia yao imepoteza watoto watatu ambao ni wajukuu waliokuwa wakiishi kwa bibi yao, huku miongoni mwa waliofariki ni mtoto wake.
“Hapa jumla wako watatu ambapo wawili ni watoto wa binti wa hapa na mmoja ni mtoto wa kijana wa hapa, wote walikuwa wanaishi na bibi yao,” amesema.
Amesema siku ya tukio watoto hao watatu waliondoka kwenda kufua nguo zao bwawani na kama ilivyo kawaida yao, lakini bahati mbaya hawakuweza kurudi tena nyumbani.
Shuhuda wa tukio hilo, Asteria Fataki amesema akiwa nyumbani kwake alisikia kelele za kuomba msaada kakini baadaye kelele hizo zikapotea.
Amesema baadaye tena akasikia kelele ndipo akaamua kuchukua fimbo kuelekea eneo ambapo kulikuwa na kelele akidhani watu wanapigana na alipofika bwawani akamkuta mama mmoja akiwa anapiga yowe, huku kukiwa na watoto wengine tisa wakitaka kuingia bwawani kuwatafuta wenzao ambao tayari walikuwa wamezama.
“Mimi ni mwalimu na watoto na wote tisa waliokuwa wanataka kuingia majini ni wa shule yetu, hivyo nikatumia fimbo kuwazuia wasiingie na wakanielewa nikaanza kupiga kelele kwa kushirikiana na huyo mama niliyemkuta bwawani.”
“Baada ya kuona hakuna watu wanakuja ikabidi tugawane maeneo, mimi nilikimbia kueleka upande wa chini mwenzangu akakimbilia upande wa juu tukawa tunapiga kelele bahati nzuri nikafika eneo watu walikuwa wanacheza mpira nilipowapa taarifa wote tukaelekea bwawani na kuanza kuwatafuta watoto,” amesimulia.