Dar es Salaam. Wakati vilio na simanzi vikitawala kwenye mazishi ya Ezenia Kamana (36), mkazi wa Tandika Maghorofani, familia yake imesema imemuachia Mungu na imetangaza kutoweka matanga, lakini imewakaribisha watu wanaotaka kuifariji.
Ezenia amezikwa katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiacha watoto watatu, mmoja wa kiume na wawili wa kike.
Kabla ya kifo chake, Ezenia alitoweka nyumbani kwake Tandika Maghorofani Agosti 19, 2024, na uchunguzi wa polisi ukaanza mara baada ya tukio hilo kuripotiwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, uchunguzi ulionyesha kuwa Ezenia alikuwa na rafiki wa kiume aitwaye Abdallah Miraji (Mussa), mkazi wa Sinza kwa Remmy na walikuwa na mgogoro. Abdallah alikamatwa na alipoulizwa, alikana kumfahamu alipo Ezenia.
Mnamo Agosti 22, 2024, polisi walipokea taarifa za viungo vya binadamu vilivyokutwa kwenye mifuko eneo la Silversand, barabara ya Mtaa wa Freedom, Kunduchi. Polisi walikuta mifuko minne ya plastiki iliyojaa viungo vya binadamu ikiwa ni pamoja na paja, vipande vya mikono miwili, eneo la kifua, tako, matumbo, na nguo.
Polisi walisema mtuhumiwa baadaye alikiri kumuua mpenzi wake na kuutenganisha mwili wake kabla ya kuutupa maeneo tofauti.
Walisema baadaye, mnamo Agosti 23, 2024, mtuhumiwa aliwaongoza polisi hadi eneo la Tegeta Block D, ambapo alionyesha sehemu alipotupa miguu na kichwa cha marehemu.
Kwa niaba ya familia, Jaji Stanley Kamana alilishukuru Jeshi la Polisi na wote waliowasaidia wakati wa kipindi kigumu walichopitia.
Alivishukuru pia vyombo vya habari kwa kuripoti tukio hilo, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia maumivu ya familia wakati wa kutoa taarifa.
Amesema familia haitakuwa na matanga, lakini inakaribisha watu kuwafariji.
Ezenia alikuwa mtoto wa nne kati ya sita na hadi umauti unamfika alikuwa Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), tawi la Maguruwe, Wilaya ya Temeke.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Temeke, Hamis Slim Hamis, alisema Ezenia alikuwa kiongozi mwenye uwezo na aliyeuwanganisha wale wenye mamlaka na wanaowaongoza.
Amesema tangu mwaka 2022, Ezenia alikuwa mstari wa mbele kutekeleza majukumu aliyopangiwa.