Yanga kumuuza Mzize, yataja thamani yake hadharani

KAMA kuna klabu inampigia hesabu straika chipukizi wa Yanga, Clement Mzize, basi inapaswa kukaa chini na kujipanga kwelikweli, baada ya mabosi wa klabu hiyo kutangaza rasmi bei ya mchezaji huyo.

Yaani kama klabu ina fedha za mawazo, isifikirie kabisa kumng’oa mchezaji huyo klabuni hapo kwa sasa.

Mabosi wa Yanga wamesema klabu inayotaka Mzize kwa sasa italazimika kwenda mezani ikiwa na Dola 1 milioni (zaidi ya Sh 2 bilioni) na hakutakuwa na longolongo zozote za kuachiwa.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba klabu za Wydad Casablanca ya Morocco na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inampigia hesabu mshambuliaji huyo aliyepandishwa misimu mitatu iliyopita akitokea timu ya Vijana ya Yanga U20.

Mabosi wa Yanga wajanja sana, baada ya kusikia klabu hizo barani Afrika na hata za ndani zikimmezea mate straika chipukizi huyo, fasta wakaamua kumuongezea mkataba mpya, kisha kuweka dau jipya la kumuuza. Awali Azam FC ilidaiwa kumpigia hesabu, lakini ikatangaziwa dau ya Sh 400 milioni ili kumng’oa Jangwani, lakini kwa sasa dau hilo limepanda hadi Sh 2 bilioni.

Tuanzie hapa kwanza. Yanga ina bilionea Gharib Said Mohammed ‘GSM’, halafu ina Rais mwenye hesabu kubwa, Injinia Hersi Said ambaye fasta tu wamezima vuguvugu la kumchomoa Mzize klabuni wakimpa mkataba wa maana kisha wakawatajia Waarabu bei wanayotaka kumuuza chipukizi huyo.

Yanga imemsainisha Mzize mkataba mpya kimyakimya unaomfanya aendelea kusalia ndani ya klabu hiyo kwa miaka miwili zaidi hadi mwaka 2027.

Mkataba wa sasa wa Yanga na Mzize ulikuwa unafikia tamati mwisho wa msimu huu, ambapo nafasi hiyo ukaziibua klabu nyingi ndani na nje ya nchi zikianza kuonyesha nia ya kutaka kumsajili.

Ingawa Yanga haijatangaza maamuzi hayo rasmi, lakini Mwanaspoti limejiridhisha kuwa, mshambuliaji huyo bado yupo mitaa ya Twiga na Jangwani baada ya mabosi wake kumalizana naye.

Dili hilo jipya Mzize anaweza kuwa kijana mdogo anayelipwa fedha nzuri kutokana na kupandishiwa vizuri mshahara wake lakini pia akipewa dau zuri la usajili ambalo halijawekwa wazi.

“Ameshasaini mkataba mpya utakaomfanya awepo klabu hadi mwaka 2027,” alisema mmoja wa vigogo wa klabu hiyo.

Kusaini kwa Mzize kunaifanya Yanga kuwa na jeuri juu ya ofa zote zinazoendelea kumiminika kumhitaji mshambuliaji huyo ambaye kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi amewaambia mabosi wake kwamba wala wasiwe na haraka watakuja kuvuna pesa nzuri huko mbele, akiendelea kuimarishwa taratibu.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini iliiomba Yanga kuridhia kwa kumnunua kwa Dola 200000  ( 542.3 milioni) ofa ambayo mabosi wa klabu hiyo bingwa Tanzania waliigomea kwa jeuri.

Mbali na Kaizer inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga Nasreddine Nabi, aliyempandisha timu kubwa wakati akiwa Jangwani pia Wydad ya Morocco inayofundishwa na Rhulani Mokwena wa Afrika Kusini nayo inatajwa kuwa na nia ya kutaka kumsajili ikiweka mezani dola 100,000 (Sh 271.1 milioni).

Kigogo huyo wa Yanga, ameliambia Mwanaspoti kwamba, kama kuna timu inataka kweli huduma ya mshambuliaji huyo basi haraka waje na kiasi cha Dola 1 milioni (zaidi ya Sh 2 bilioni) ambapo wao ndio watampeleka haraka uwanja wa ndege au kokote timu hiyo ilipo ili akaitumikie.

“Hatuna shida ya kuuza wachezaji, hakuna aliyetarajia kama tungemuuza Fiston Mayele, lakini tulifanya biashara, hivyo hata Mzize anaweza kuuzwa kama tukiona kuna timu imefikia bei tunayotaka,” alisema bosi huyo wa juu kabisa katika uongozi huyo wa Yanga na kuongeza;

“Kusema tutamuuza Mzize kwa dola 100,000 huo ni kama utani, hata wanachama na mashabiki wetu watatufukuza. Lakini kama kuna timu itaweka dola milioni moja, watutumie hata ujumbe wa Whatsapp tu, sisi tutampeleka haraka kwa hiyo klabu ilipo.”

Msimu uliopita Mzize alihusika katika mabao zaidi ya 10 ya mashindano akifunga mabao sita na kutoa asisti nne katika Ligi Kuu, pia akifunga matano ya Kombe la Shirikisho akiwa Mfungaji Bora, mbali na matatu ya mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika yaliyosaidia kuiingiza Yanga makundi baada ya miaka 25.

Related Posts