Abiria wa Qatar wanaotumia CRDB kupata punguzo

Dar es Salaam. Benki ya CRDB kwa kushirikiana na  kampuni ya malipo ya Visa International imetangaza kutoa nafuu ya nauli ya asilimia 22 kwa abiria wa Shirika la Ndege la Qatar watakaolipia tiketi zao kwa kutumia kadi za Tembocard Visa.

Nafuu hiyo inajumuisha punguzo la asilimia 12 litakalotolewa na kampuni ya Visa International pamoja na asilimia 10 ya fedha taslimu itakayorudishwa kwenye akaunti ya mteja wa CRDB baada ya kulipia tiketi yake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Agosti 26, 2024 jijini hapa wakati wa kuzindua kampeni hiyo itakayodumu kwa miezi sita, Mkurugenzi wa Wateja wa Awali na Kati wa Benki ya CRDB, Buberwa Paul amesema ushirikiano huu unalenga kujenga utamaduni wa wateja kutumia kadi kufanya malipo na kuachana na matumizi ya fedha taslimu.

“Punguzo hili la asilimia 22 ni sehemu ya motisha kwa wateja kujenga utamaduni wa kutumia kadi kufanya malipo. Nitumie nafasi hii kuwakaribisha wateja wetu wanaotaka kusafiri kutumia ndege za Shirika la Ndege la Qatar ili kunufaika na punguzo hili ili,” amesema Paul.

Mkurugenzi huyo amesema ushirikiano wa CRDB, Visa International na Shirika la Ndege la Qatar unazijumuisha taasisi mbili kubwa zenye ubora unaotambulika ndani na kimataifa uliozifanya zitunukiwe tuzo za aina tofauti.

Tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, Paul amesema Benki ya CRDB imetunukiwa takriban tuzo 200 ndani na kimataifa, ikiwamo tuzo za utoaji wa huduma bora za Visa, wakati Shirika la Ndege la Qatar likishinda tuzo ya shirika bora la ndege zinatolewa na kampuni ya Skytrax mara nane kati ya mwaka 2011 mpaka mwaka 2024.

Shirika hilo pia limeshinda tuzo ya shirika lenye daraja bora la biashara duniani (world’s best bisness class), ukumbi bora wa daraja la biashara duniani (world’s best business class lounge) na shirika bora la ndege ukanda wa Mashariki ya Kati.

“Benki ya CRDB na Shirika la Ndege la Qatar pia tunafanana kwenye ubunifu. Benki yetu ndio kiongozi katika ubunifu wa huduma na bidhaa zinazokidhi mahitaji na matarajio ya wateja wetu vivyo hivyo kwa Shirika la Ndege la Qatar ambalo limeshinda tuzo za kimataifa kutokana na ubunifu wake.  Sisi sote wawili tunajali na kuyatunza mazingira,” ameeleza Paul.

Meneja Mkazi Shirika la Ndege la Qatar, Isaack Wambua amesema ndege zao zenye makao makuu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamad uliopo jijini Doha ambao ulishinda tuzo ya uwanja bora wa ndege duniani mara tatu kuanzia mwaka 2021, zinatua katika viwanja vingine 170 duniani kote, hivyo k­­uwapa abiria wao uhakika wa kufika popote wapatakapo huku Benki ya CRDB ikiwahakikishia  kukamilisha safari zao kwa gharama nafuu.

“Punguzo hili la Benki ya CRDB litakalodumu mpaka Desemba mwaka huu, linawahusu wateja wetu wote wanaotumia kadi za Tembocard Visa ambao ni zaidi ya milioni nne.

“ Kwa kuwa tunatambua kwamba wanazo biashara nje ya nchi na huwa wanasafiri kwa malengo tofauti, tunaamini wataitumia fursa hii kusafiri na ndege za Shirika la Qatar kwenda wanapopataka,” amesema Wambua.

Related Posts