SIMBA jana ilikuwa uwanjani kucheza mechi ya pili ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate, huku mastaa wa timu hiyo wakifichua, kocha Fadlu David anayewanoa ni zaidi ya kocha kwa namna anavyoishi nao kambini, jambo linalowafanya waonekane wakali uwanjani kwa kila mechi wanayocheza.
Simba ilianza msimu mpya wa ligi hiyo kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Fadlu katika ligi hiyo, kwani ameajiriwa hivi karibuni kuchukua nafasi ya Abdelhak Benchikha wa Algeria aliyetimka Aprili mwaka huu saa chache baada ya Simba kulazwa 2-1 na Yanga.
Kocha huyo ameiongoza Simba kucheza jumla ya mechi saba, zikiwamo nne za kirafiki na tatu za mashindano, mbili za Ngao ya Jamii na moja ya Ligi Kuu, huku kikosi hicho kikipoteza mara moja tu kwa kuchapwa na Yanga bao 1-0, huku ikishinda michezo sita ikifunga jumla ya mabao 11 na yenyewe kufungwa mabao manne tu (hii ni kabla ya mechi ya jana jioni).
Lakini siri ya mafanikio ya timu hiyo iliyoundwa upya kwa sasa chini ya Fadlu baada ya kusajili wachezaji wapya 13 na kutema mastaa kadhaa waliokuwako msimu uliopita, imefichuliwa na wachezaji wa timu hiyo waliozungumza na Mwanaspoti na kusema kazi kubwa imefanywa na kocha huyo Msauzi.
Mastaa wa kikosi hicho, licha ya kutotaka kutajwa majina yao, walimuelezea Fadlu kutokuwa na upendeleo, haangalii ukubwa wa majina, isipokuwa mchezaji anayejituma mazoezini ndiye anayepewa nafasi, mkali na rafiki na amekuwa akifanya kazi zaidi ya kocha kwa namna anavyozungumza na wachezaji.
Walisema hali hiyo ni tofauti na ilivyokuwa enzi za Benchikha waliyedai alikuwa mkali na asiye na muda wa kuzungumza na mtu hasa anayemzingua mazoezini au katika mechi.
Kiungo mmoja ambaye ni mzawa, alisema Fadlu anapoona kuna kitu hakijaenda sawa kwa mchezaji anakikemea muda huo huo, ili mwingine ajifunze, bila kuangalia ukubwa wa jina lake.
“Anasimamia nidhamu, kuanzia muda ambao mchezaji anatakiwa apatikane wakati wa kunywa chai, mazoezi, chakula cha mchana na usiku, nje na hapo unaweza ukaona upande wake wa pili,” alisema, huku beki aliye mzawa akiweka wazi kwa muda waliokaa naye, walimshuhudia hana mambo ya konakona, muwazi na anataka kila mmoja ajisikie ana umuhimu katika timu.
“Kuna wakati akimwona mchezaji hayupo sawa ni mwepesi kumuita na kukaa naye chini, hata kama mambo ni nje ya kazi, basi anakujenga na maisha mengine yanaendelea, kifupi ni kocha ambaye yupo wazi sana ni kama baba ambaye ana muda wa kucheka na kumkanya mwanaye,” alisema beki huyo mzoefu.
Winga mwingine wa kigeni alisema; “Faida kubwa ya kocha tuliyenaye, ukikosea ni rahisi kukuweka katika mstari, hana upendeleo, katika mazoezi anapenda mchezaji anayejituma na anasema wazi ndiyo yanayompa taswira ya kipi kinakwenda kufanyika katika mechi.”
Katika hatua nyingine beki wa kati wa timu hiyo Mcameroon, Che Fondoh Malone amefichua matarajio makubwa aliyonayo kwa msimu wa pili mfululizo wa kuwatumikia Wekundu hao akisema amepata uzoefu jinsi ilivyo ngumu na ushindani, unaowafanya wajitume kwa bidii, kuhakikisha wanapigania mataji.
Simba kwa msimu mitatu mfululizo iliyopita haijatwaa taji la Ligi Kuu Bara wala Kombe la Shirikisho na sasa chini ya Fadlu mashabiki na wanachama wamekuwa na matumaini kutokana na aina ya wachezaji waliosajiliwa na soka inalocheza tangu iwe na kocha huyo Msauzi.
Malone aliyasema hayo wakati akizungumza na mashabiki mbalimbali kupitia mtandao wa TikTok, ambapo Mwanaspoti lilipata nafasi ya kumuuliza anapenda kitu gani Tanzania? Ndipo alipofunga haya.
“Ukiachana na ushindani wa ligi na sapoti ya mashabiki, Tanzania ni nchi ya amani, ndiyo maana tunafanya kazi kwa amani na utulivu mkubwa, kwa ufupi napenda kila kitu katika nchi hii,” alisema Che Malone aliyetwaa tuzo ya Nyota wa Mchezo kati ya Simba na Tabora United wiki iliyopita walipoifumua mabao 3-0.
Beki huyo aliyefunga bao la kwanza kwa timu hiyo katika mchezo huo, alisema ana matumaini makubwa ya Simba kufanya vizuri kwa jinsi timu inaundwa na wachezaji wenye vipaji, uwezo na umri mdogo, pia kwa jinsi wanavyojituma na kufuata maelekezo ya kocha, huku akiwaomba mashabiki kuiunga mkono timu hiyo.