Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Septemba 19, 2024 kutoa hukumu ya kesi ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, inayomkabili Purity Njau.
Njau anadaiwa kutumia laini hiyo bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma ambaye ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Agosti 26, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Geofrey Mhini wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya hukumu.
Hatua hiyo inatokana na Mahakama kufunga ushahidi wa pande zote na upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne pamoja na vielelezo.
Awali, Wakili wa Serikali, Eva Kassa alisema kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya hukumu.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kati ya Juni hadi Agosti, 2023 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alibainika kutumia laini ya simu ya Amina Mohamed Juma.
Ilidaiwa mshtakiwa huyo alitumia laini hiyo bila kutoa taarifa TCRA wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.