Dar es Salaam. Kutokana na ufinyu wa eneo katika Kituo cha Afya cha Tandale ambao unasababisha changamoto katika utoaji wa huduma za afya kwa wananchi, kituo hicho kiko mbioni kuongezwa ukubwa. Kwa sasa, kituo hicho kinakadiriwa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 1,000 kwa siku, sawa na watu 30,000 kwa mwezi, kama alivyoeleza Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Wilfred Barinzigo.
“Wagonjwa wengi hapa ni wale wanaotibiwa na kuondoka pamoja na wale wanaolazwa. Ufinyu uliopo, kama vile katika jengo la wazazi, unasababisha usumbufu katika utoaji huduma,” amesema.
Ameongeza kuwa changamoto za huduma zinatokana na ufinyu wa eneo, ambapo kituo hicho kinatakiwa kiwe na uwezo wa kufanya upasuaji mkubwa na mdogo.
“Vilevile, tunahitaji kuwa na wodi za aina tatu; wodi ya kina mama, ya watoto, na ya kina baba kwa ajili ya mapumziko ya siku tatu.”
Dk Barinzigo amesema kuwa hayo yote hayatekelezeki kutokana na ufinyu wa nafasi, hivyo kupelekea wagonjwa wengi kupewa rufaa kwenda Mwananyamala, jambo ambalo wengi huliona kama usumbufu.
Amebainisha kuwa hata miundombinu ya barabara inachelewesha kufika haraka kituoni.
“Mpangilio wa jengo haujakaa kirafiki kutoa huduma kwa sababu ni muundo wa kizamani, ukizingatia Dar ni jiji,” amesema.
Dk Barinzigo amesisitiza kuwa wanapenda kupunguza msongamano Mwananyamala kwa kuwahudumia wagonjwa wao, hivyo upanuzi ni muhimu.
“Wagonjwa wanafuata huduma nzuri, mimi na wafanyakazi wenzangu tumejipanga kutoa huduma bora kuanzia lugha kwa wagonjwa, vipimo, matibabu. Tukisimamia hilo, wagonjwa wataongezeka zaidi ya hapa,” amebainisha.
Hayo yote yalibainishwa katika ziara ya Naibu Meya wa Kinondoni, Michael Urio, aliyoifanya hii leo, Agosti 26, 2024, kujionea hali halisi ya utoaji huduma sambamba na changamoto zinazokikabili kituo hicho.
Katika kutatua hilo, Urio amesema mchakato uliopo ni kufufua mazungumzo ya kumhamisha mmoja wa wakazi wa jirani ya eneo hilo ili kuanza upanuzi wa kituo hicho.
“Nitazungumza na Mstahiki Meya na Mkurugenzi kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa kituo kwa lengo la kuendelea kutoa huduma bora kwa wakazi wa Tandale na wale wanaotoka maeneo mengine,” amesema.
Ameongeza kuwa mazungumzo na mmiliki wa eneo yalishafanyika, ila kwa sasa kinachoendelea ni kukaa na familia yake kwa ajili ya kuwahamisha ili ujenzi uanze.
“Mchakato huu upo karibu kukamilika na watalipwa fedha. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,” amesema Urio.
Ameongeza kuwa kitendo cha kuchoma taka zinazozalishwa kituoni hapo hakifai kwani sehemu ya kuchomea ipo karibu na makazi ya watu wa karibu, hivyo suala hilo litafutiwe njia mbadala.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Tandale, Abdallah Chief, amesema idadi ya wagonjwa ni kubwa na eneo ni dogo kiasi cha kuwafanya watoa huduma kushindwa kutumia utaalamu walionao katika kutoa huduma.
“Serikali iharakishe mchakato huu kwani Tandale inapokea wagonjwa wengi, wengine kutoka Manzese, Kijitonyama, na Mburahati wote wanakuja,” amesema Chief.