Polisi yawashikilia watatu akiwemo mtoto anayedaiwa kuiba watoto sita

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi linawashikilia watu wawili waliosikika wakimhoji mtoto aliyejitambulisha kwa jina la Evaristo katika moja ya picha jongefu zilizosambaa katika mitandao ya kijamii.

Pia, jeshi hilo limesema linamshikilia mtoto huyo na kuendelea na uchunguzi wa maelezo yaliyozungumzwa naye katika kipande hicho cha video akijinasibu kwa wizi wa watoto.

Katika kipande hicho cha video, mtoto huyo alisikika akijinasibu kwa wizi wa watoto akishirikiana na wenzake watatu kwa kuwarubuni kwa pipi.

“Nimeshateka watoto sita hadi sasa, wameshakufa,” alisikika mtoto huyo akihojiwa na watu wawili ambao zilisikika sauti zao kwenye video hiyo.

Taarifa ya kushikiliwa kwa watu hao imetolewa leo Jumatatu Agosti 26, 2024 na msemaji wa jeshi hilo, David Misime.

Kwa mujibu wa Misime, katika taarifa hiyo aliyetajwa kuwa mshirika wa mtoto huyo kwenye wizi huo wa watoto naye amekamatwa.

“Aliyemtaja kwamba akishaiba watoto wadogo akishirikiana na wenzake humkabidhi na yeye huwaua, kisha kuwafunga kwenye maboksi na kuwasafirisha hadi Dar es Salaam, askari wamefanikiwa kumpata,” ameeleza Misime.

Misime amesema pia jeshi hilo lilifika Kitongoji cha Nero wilayani Chalinze ambako mtoto huyo anadai kuiba watoto sita na baada ya mahojiano na viongozi mbalimbali, haijathibitika kupotea kwa mtoto yeyote.

“Viongozi hao wamethibitisha hakuna matukio kama hayo yaliyotokea kwenye maeneo yao,” amesema.

Kutokana na uhalisia huo, amesema uchunguzi unaendelea kwa kuwa kinachojionyesha katika video hiyo ni kwamba mtoto huyo alitoa baadhi ya maelezo, ili kujinasua katika mazingira magumu aliyokuwepo.

Katika taarifa hiyo, Misime amewaondoa hofu wananchi kuhusu picha hiyo mjongeo, akisisitiza haijathibitika hadi sasa kwamba kilichozungumzwa ni uhalisia.

“Kama kungekuwa na tukio au matukio ya wizi wa watoto sita, lazima taarifa zingekuwepo na zingekuwa zimesambaa maeneo mbalimbali,” amesema.

Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha mtoto huyo pamoja na wenzake wanatuhumiwa kujihusisha na wizi wa nguo na vitu vingine katika maeneo mbalimbali.

Related Posts