Safari ya Msechu kutoka kuwekewa puto hadi kukatwa utumbo

Dar es Salaam. Miongoni mwa mambo yanayoulizwa sana na Watanzania inapochapishwa picha ya msanii Peter Msechu katika mtandao wowote wa kijamii ni maendeleo ya puto alilowekewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.

Hiyo ni kutokana na wengi kuhisi kuwa puto hilo halikufanyi kazi kutokana na kutoonekana kumpunguza unene alionao na hatimaye Msechu ameiambia Mwananchi kuwa sasa amekatwa utumbo.

Hiyo ni baada ya kushindwa kupunguza ulaji kama alivyokuwa akila wakati amewekewa puto.

Msechu amesema hayo leo Jumatatu Agosti 26, 2024 wakati akichangia mada kwenye mjadala wa Mwananchi X Space, unaoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) Tanzania pamoja na Taasisi ya Lishe na Chakula Tanzania (TFNC), wenye mada inayohoji: Je, kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi ni kuimarisha afya au kujinyima uhondo?

Msechu amesema amelazimika kukatwa utumbo ili apungue uzito, suala ambalo amekuwa akipambana nalo kwa miaka mingi.

Akiwa miongoni mwa watu wa awali walionufaika na huduma ya kuwekewa puto Januari 2023 ili wapungue uzito katika hospitali ya Mloganzila, baadhi ya watu walikuwa wakisubiri kuona matokeo ya kupungua kwake.

Akitoa ushuhuda, Msechu amesema kabla ya kuweka puto alikuwa na uwezo wa kula chipsi sahani mbili mchana na nyingine jioni, huku matumizi ya vyakula vyenye mafuta kwake yakiwa kwa kiwango kikubwa.

 “Hali hii ilifanya nikawa naongezeka uzito kwa kiwango kikubwa. Nilianza kupitia changamoto ya uzito kuwa mkubwa hadi nilifikia kilo 150, huku afya ikianza kuwa ya kusuasua jambo lilinifanya niende kuweka puto,” amesema Msechu.

Amesema hadi anafikia uamuzi huo tayari alikuwa amejaribu njia mbalimbali za kupunguza uzito, ikiwemo kufanya mazoezi na dawa za mitishamba.

“Kuna mti mmoja ambao mke wangu aliambiwa uko nchi fulani nikila naenda kuharisha na uzito unapungua, akautafuta akauleta, kweli ukisikia tu ile harufu unaharisha. Nilipoutumia niliharisha karibu wiki nne, nilipungua kidogo lakini nilikuwa nikikutana na chakula narudi nilipokuwa,” amesema Msechu.

Amesema alipoweka puto ili apunguze kula ndani ya mwaka mzima kilo 30 zilipungua na walipomtoa Desemba 25, 2023 wataalamu waliamini ameiga mfumo bora wa ulaji kidogo na wenye afya.

“Kwangu ilikuwa tofauti, nimetolewa tu puto nikapiga simu nyunbani nikute wali maharage wenye nazi na wote walishangaa. Nilirudi kutamani kula vitu vya hovyo, sikufuata masharti ya kula au naweza kusema njaa ilirudi,” amesema Msechu.

Amesema alianza kula kwa kiwango kikubwa na wakati mwingine njaa ilipomzidia usiku alijifanya anaenda studio iliyopo nyumbani kumbe anakwenda jikoni.

 “Ndani ya miezi minne nilijikuta nimerudi kilo144, kwani kiwango changu cha ulaji kiliongezeka na hasa kwa vitu vya kukaangwa,” amesema Msechu.

Amesema baada ya kukaa na wataalamu waliomfanyia vipimo ndipo wakamshauri apunguze sehemu ya kupokea chakula, ili awe anakula kidogo hivyo akakatwa utumbo miezi minne iliyopita.

“Kwa sasa baada ya kukatwa utumbo nakula kidogo sana, nimeanza kuwa vizuri huku nikishauriwa kula vizuri mbogamboga ili nipunguze mafuta na imenisaidia kupunguza kilo 27 hadi sasa,” amesema.

Akishauri wengine, Msechu amesema lazima watoto wafundishwe shuleni namna ya kula ili kuwaepusha na madhara ya kutokuzingatia lishe.

Katika hili, Msimamizi Mkuu Miradi ya Lishe Helen Keller International, Dk Theresia Jumbe amesema hata vyakula vina mafuta yake, ila changamoto inakuja pale watu wanapoongeza mafuta katika upishi wa vyakula hivyo.

Amesema lazima watu wahakikishe kiasi cha mafuta wanachokitumia kisizidi kiwango kinachohitajika, kwani changamoto yake kiafya ni kubwa, ikiwemo kusababisha maradhi.

Akifafanua zaidi amesema mahitaji kwa watoto wadogo ni makubwa kwa kuwa bado wanakua kimwili, lakini katika umri wa kati wanahitaji kupunguza kiasi cha mafuta hadi kuekelea utu uzima.

“Kwa sisi watu wazima lazima tuanze kupunguza matumizi ya mafuta” ameshauri Dk Jumbe.

Kuhusu mafuta, Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Dk Germana Leyna amesema uongezaji wa mafuta  una madhara makubwa mwilini.

“Chakula kilivyo kabla ya kuongezwa chochote kina virutubisho vinavyotosheleza uhitaji wa mwili. Pale tunapoongezea mafuta kwa ajili ya ladha au muonekano lazima tujue tunaongeza baadhi ya madhara yanayopatikana kutokana na mafuta hayo.

“Mungu ametengeneza miili yetu inajiratibu yenyewe mfano unapokunywa maji mengi unayapunguza. Basi hata kwenye vyakula mwili upo hivyo pia ndio maana tunahisi njaa. Kutumia mafuta kwenye vyakula kunaongeza kiasi kikubwa cha nishati kwenye mwili,” amesema.

Akitolea mfano vyakula vyenye mafuta ya asili, amesema miongoni mwake ni karanga na baadhi ya samaki wenye mafuta yanajitoshekeza hivyo hakuna haja ya kuongeza.

Amesema vipo vyakula vyenye mafuta yake ya asili, hivyo hakuna haja ya kutumia mafuta mengine mwilini ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza, ikiwemo magonjwa.

“Tujaribu kutumia mafuta yanayopatikana kiuhalisia kuliko kutumia mafuta ya nyongeza,” amesema.

Kutokana na uhali holela wa mafuta, Mhariri wa jarida la Afya Gazeti la Mwananchi, Herieth Makwetta amesema kwa sasa hali inazidi kuwa mbaya, huku takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha magonjwa yasiyoambukiza yamesababisha asilimia 33 ya vifo vyote nchini kwa mwaka 2017, ambapo jumla ya vifo 134,600 viliripotiwa na kuhusishwa na magonjwa yasiyoambukiza.

Vifo hivi vilitokana zaidi na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu kwa asilimia 13, Saratani asilimia 7 na ajali kwa asilimia 11.

“Hata hivyo ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi umeelezwa kuwa chanzo cha magonjwa mengi yasiyoambukiza, ikiwamo shinikizo la damu ‘presha’, saratani huku ikichangia kwa kiasi kikubwa kuharibu ogani ya moyo,” amesema Makwetta

Amesema kupunguza kula mafuta kunakuepusha magonjwa yasioambukiza na kuwa na mwili mzuri, kutokuwa wanene kupindukia cha msingi ni kufuata maelekezo ya wataalamu.

Related Posts