Saluti Kwao: Masupastaa wa soka wanaomiliki klabu zao za soka

MADRID, HISPANIA: HABARI ndo hiyo. Kylian Mbappe amekuwa supastaa mwingine kwenye mchezo wa soka kuwekeza pesa zake kwenye kumiliki hisa katika klabu ya mchezo huo na kufanya kuwapo na uhakika wa mchezo wa mpira wa miguu kuwa na uhakika wa kudumu miaka na miaka.

Imekuwa kama kawaida kwa miaka ya hivi karibuni wanasoka kuamua kuwekeza pesa zao kwenye kununua hisa na kuwa wamiliki wa timu.

Katika kulithibitisha hilo, hii hapa orodha ya wanasoka wa nguvu kabisa wanaomiliki klabu zao za soka kwa maana ya kuwekeza na kununua hisa katika timu hiyo. Zitatoboa?

David Beckham – Inter Miami

Kabla ya David Beckham kutundika daruga zake katika nyakati zake za mwisho akiwa na kikosi cha PSG, kulikuwa na fununu juu ya mpango wa Mwingereza huyo kwenda kuwekeza kwenye klabu ya MLS ikiwa ni moja ya mambo yake ya ujasiriamali atafanya baada ya kuachana na soka kama mchezaji. Wengi kwa wakati huo walidhani, Beckham aliachana na soka la kuwa mchezaji basi moja kwa moja atakimbilia kwenye ukocha. Baada ya kuwa sehemu ya wamiliki wa klabu ya Salford City na wachezaji wenzake wa klabu ya Man United kwenye ile Class Of ’92, Beckham aliamua kwenda kuanzisha timu yake kwenye MLS. Na hapo ndipo ilipoibuka Inter Miami ambayo kwa sasa imesheheni majina ya mastaa wa maana kabisa, akiwamo supastaa wa Argentina, Lionel Messi, fowadi wa Uruguay, Luis Suarez na kiungo Mhispaniola, Sergio Busquets. Thamani ya Inter Miami kwa sasa inatajwa kuwa Dola 600 milioni.

Didier Drogba – Phoenix Rising

Pengine unaweza kukumbuka nyakati za kibabe kabisa za mshambuliaji Didier Drogba alipokuwa anawatesa mabeki wa timu pinzani uwanjani. Staa huyo alicheza Uturuki, China kabla ya kurudi Stamford Bridge kubeba tena taji la Ligi Kuu England, kisha akaenda Canada kukipiga kwenye kikosi cha Montreal Impact kilichokuwa kinashiriki ligi ya MLS. Na pengine utakuwa umesahau klabu zote alizochezea Muivory Coast huyo, hasa kwenye timu zake za mwisho mwisho, alipokipiga Phoenix Rising. Baada ya miezi kadhaa ya kuwa huru, staa huyo alikwenda kusajiliwa na klabu hiyo ya Arizona, ambako baadaye alinunua hisa chache za kuwa mmoja wa wamiliki wa klabu hiyo. Kwenye klabu hiyo, Drogba alikuwa mchezaji mmiliki, akifunga mabao 17 katika mechi 26 kabla ya kustaafu mwaka 2019.

N’Golo Kante – Royal Excelsior Virton

Baada ya kuachana na Chelsea kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, kiungo anayekaba kupita maelezo, N’Golo Kante aliwashangaza wengi baada ya kuamua kununua timu ya pili, alipokwenda kuwa mwenyekiti wa klabu ya Daraja la Tatu ya Ubelgiji, Royal Excelsior Virton. Kante anaamua kutumia mamilioni ya pesa anazovuna huko kwenye soka la Saudi Arabia kuwekeza kwenye klabu hiyo ya Ubelgiji. Msimu uliopita, Royal Excelsior Virton ilimaliza nafasi ya 10 kwenye ligi ya Belgian National Division 1. Kuna mambo mengi yanasubiriwa kwa hamu kuona kama klabu hiyo itapata mafanikio makubwa ndani ya uwanja kama ambavyo mmiliki wake amekuwa akipata kila anapoingia uwanjani.

Paolo Maldini – Miami FC

Beckham si mchezaji pekee wa kutoka kwenye soka la Ulaya aliyecheza kwa mafanikio makubwa ambaye amewekeza pesa zake kwenye klabu hiyo ya Florida. Kwa kifupi tu, Maldini alitangulia kuwekeza kwenye klabu hiyo kabla ya Beckham, alipofanya hivyo kwenye timu ya Miami FC mwaka 2015. Baada ya kuichukua timu hiyo ya Miami FC, Paolo alisaidia kumfanya Alessandro Nesta kuwa kocha wa kikosi hicho. Kwa miaka ya karibuni, beki huyo gwiji wa Italia amejiweka mbali kidogo na timu hiyo akielekeza nguvu zake kwenye kuwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu ya AC Milan. Hata hivyo, Maldini ameripotiwa kuachia ngazi kwenye wadhifa wake katika klabu hiyo ya Milan baada ya kutibuana na bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo.

Ronaldo – Real Valladolid

El Fenomeno anamiliki hisa nyingi zaidi, asilimia 82 kwenye klabu ya Real Valladolid, ambayo imekuwa ikipanda na kushuka daraja kwa miaka ya hivi karibuni, ikitamba kwenye La Liga na Segunda Division. Mshindi huyo mara mbili wa Kombe la Dunia akiwa na Brazil, anamiliki pia hisa kwenye klabu vigogo ya huko kwao Brazil, Cruzeiro, ambapo baadaye aliamua kuuza hisa zake baada ya timu hiyo kuwa na matatizo mengi ya nje ya uwanja. Baada ya kuuza hisa za Cruzeiro, Ronaldo alisema kinachofuata ni kuipiga bei pia Valladolid, kabla ya kubadili mawazo na kuendelea kuwa mmiliki wa timu hiyo, alipogomea ofa ya Euro 28 milioni kutoka kwa kampuni ya ujenzi ya Inexo iliyotaka kuinunua klabu hiyo.

Gerard Pique – FC Andorra

Wakati beki Gerard Pique akiwa bado mchezaji wa kulipwa kwenye kikosi cha Barcelona, tayari alikuwa kwenye ndoto za kuwa rais wa klabu kwa maana ya kumiliki timu yake mwenyewe ya soka. Staa huyo amekuwa akivutiwa sana na mambo ya ujasiriamali. Kuna nyakati aliingia kwenye sakata la kuchunguzwa baada ya kufanya malipo ya ujanja ujanja ili kufanya mechi ya Spain Super Cup kuchezwa Saudi Arabia. Amekuwa akihusisha pia kwenye matukio ya mechi za michezo mingine ikiwamo tenisi kabla ya shirikisho la kimataifa la mchezo wa tenisi kusitisha mkataba naye wa kuandaa Davis Cup. Staa huyo anaripotiwa kumiliki hisa kwenye klabu ya soka ya FC Andorra, inayocheza ligi ya chini na amekuwa mmiliki wa timu hiyo tangu mwaka 2018.

Supastaa wa Ufaransa, Thierry Henry aliweka wazi dhamira yake ya kununua hisa kwenye klabu ya Como ya huko Italia, wakati alipozungumza na waandishi wa habari, Agosti 2022. Fowadi huyo wa zamani wa Arsenal na Barcelona alibainisha kuvutiwa na historia ya klabu ya Como na ndio maana alikuwa na mpango wa kuwekeza hapo. Miaka miwili baadaye, Como kwa sasa ipo kwenye Serie A, huku mchezaji mwenzake wa zamani Henry, kiungo Cesc Fabregas waliyecheza pamoja huko Arsenal ndiye kocha wa timu hiyo, huku mkali huyo wa Ufaransa akitimiza ndoto zake za kumiliki hisa kwenye klabu hiyo. Kwenye kikosi cha Como kwa sasa kuna mastaa wa maana kabisa, wakiwamo Raphael Varane, Pepe Reina, Alberto Moreno, Andrea Belotti na Patrick Cutrone watakaopambana kuhakikisha timu hiyo haishuki na kubaki kwenye Serie A.

Zlatan Ibrahimovic – Hammarby IF

Kuna gazeti moja liliripoti kwamba Ibrahimovich alikuwa anarudi kwao Sweden kumalizia maisha yake ya soka baada ya kuwa mmiliki mwenza wa klabu ya Hammarby IF mwaka 2019. Kipindi hicho, mchezaji huyo alikuwa huru wakati alipoachana na klabu ya LA Galaxy. Alirudi Ulaya, lakini hakwenda Sweden, badala yake alikwenda kujiunga na AC Milan huko San Siro, ambako alifunga mabao 37 na kushinda taji la Scudetto. Kitendo cha kuripotiwa kuwa mmoja wa wamiliki wa klabu ya Hammarby kuliwakera mashabiki wa timu yake ya zamani ya Malmo na kufanya jaribio la kuchoma moto sanamu ya mchezaji huyo lililokuwa nje ya uwanja wao kutokana na upinzani wa jadi kati ya timu hizo.

Yamekuwa majira ya kiangazi mazuri kabisa kwa Kylian Mbappe baada ya kukamilisha uhamisho wa ndoto zake kwa kutua kwenye kikosi cha Real Madrid bure kabisa akitokea Paris Saint-Germain. Staa wa kimataifa wa Ufaransa, Mbappe alilipa chini ya Euro 20 milioni kununua hisa asilimia 80 za klabu ya Caen. Timu hiyo ya Ligue 2 inatajwa kuwa kwenye hali mbaya ya kiuchumi. Caen ni timu maarufu sana kwenye soka la Ufaransa, ikiwatoa mastaa wa maana kabisa akiwamo N’Golo Kante, Thomas Lemar na Raphael Guerrero. Mbappe ameamua kuwekeza kwenye klabu hiyo.

Kwenye orodha ya wanasoka wanaoripotiwa kumiliki timu za soka yupo pia Wilfried Zaha anayedaiwa kumiliki klabu ya AFC Croydon Athletic, huku Cesar Azpilicueta akiripotiwa kumiliki timu ya Hashtag United, wakati wakali wa zamani wa Man United, Ryan Giggs, Paul Scholes, Gary Neville, Phil Neville na Nicky Butt wakimiliki kwa pamoja timu ya Salford City na nyota wengine, Eden Hazard, Demba Ba, Yohan Cabaye na Moussa Sow wakimiliki klabu ya San Diego 1904.

Related Posts