Sido yaja na mashine za kuchanganyia virutubisho lishe

Dar es Salaam. Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) limejipanga kutengeneza mashine ya kuchanganya virutubisho vya lishe shuleni ili kusaidia wanafunzi kupata chakula chenye mchanganyiko unaotakiwa kiafya.

Utengenezaji wa mashine hizo unakuja wakati kukiwa na kamapeni ya Serikali kuhimiza wanafunzi kupata lishe bora katika chakula wanachopata shuleni.

Akizungumza leo Jumatatu Agosti 26, 2024 wakati wa kuonyesha mashine hizo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Sido, Laurence Kayungi amesema licha ya wazazi kuwa na moyo wa kuchangia chakula kwa ajili ya watoto shuleni, bado chakula hicho hakina virutubisho.

“Ndipo Sido tumekuja na mbinu ya kutengeneza mashine kwa ajili ya kuchanganyia virutubisho kwenye vyakula, baada ya kuona wanafunzi wanakula vyakula ambavyo havina virutubisho, ambapo mchakato huo utawalenga wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari,” amesema Kayungi.

Amesema watatengeneza mashine 3,033 kwa ajili ya kuzalisha unga wenye virutubisho, ikiwa ni maelekezo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.

 “Mashine hizo ni mbili, moja ikiitwa Kinyunyuzio (dosing fire) kazi yake kubwa ni kuongeza virutubisho kwenye unga na mashine nyingine inaitwa Mixture Mashine, kazi yake ni kuchanganya unga na virutubisho kwa pamoja,” ameongeza.

Mratibu wa Lishe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Abigal Marwa, amesema hiyo ni ishara tosha kwa kusema kwamba sasa Tanzania imepiga hatua kwenye masuala ya sayansi na teknolojia.

Amezitaka taasisi za Serikali ambazo ni pamoja na Shirika la Viwango (TBS), taasisi za elimu na afya kuhakikisha mashine hizo zimaleta manufaa ya lishe kwa watoto.

Ofisa Uthibiti Ubora wa TBS, Rhoda Kidolezi amesema washachukua sampuli ya unga uliochangnywa na mashine hiyo, ili kuthibitisha ubora wake.

Kwa upande wake, Ofisa Lishe Wizara ya Afya, Peter Kaja amewataka wazazi kujenga utamaduni wa kuchangia chakula shuleni kwa ajili ya watoto wao, ili kurahisisha upatikanaji wa lishe.

“Wazazi ni wakati sasa wa kuchangia chakula shuleni kwa ajili ya watoto wao na mifumo maalumu imeshawekwa kwa ajili ya utekelezaji wa kutoa huduma hiyo,” amesema Kaja.

Related Posts