Afande atia neno michezo | Mwanaspoti

“MICHEZO ni fursa ya ajira na burudani na kama unataka kuwa na afya bora ya akili na mwili, huwezi kukwepa mazoezi.”

Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Malipo Yona ameyasema hayo leo wakati wa tamasha la michezo lililokwenda sambamba na mdahalo wa utoaji elimu juu ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi kutoka Kata ya Kibamba.

Yona ambaye ni Polisi Kata wa Kibamba, alisema michezo ni zaidi ya afya na burudani, pia ni fursa ya ajira kwa vijana na kizuri zaidi mtu anapofanya mizoezi anaepukana magonjwa kwa sababu mwili unakuwa na kinga.

“Kama kuna mtu anasema amechelewa, mimi nasema bado hujachelewa, unachotakiwa kufanya ni kufanya mazoezi, jijengee tabia ya kufanya mazoezi kila siku kwa ajili ya kutunza afya yako, lakini kama unakipaji cha michezo basi kitumie vizuri ili kikupatie ajira,” alisema Yona.

Mdahalao huo ulishirikisha wanafunzi wa kike 80 ambao ni mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia kutoka klabu tatu za Sekondari, ambazo ni Mbezi Inn, Kibwegere na Kibweheri, zote kutoka kata ya Kibamba, wilaya ya Ubungo.

“Mazoezi ni moja ya tiba mzuri ambayo imeweza kusaidia vijana kupata ajira, imeweza kusaidia watu kuwa na afya nzuri, hivyo ufanyaji wa mazoezi mara kwa mara unasaidi kujenga afya ya akili na mwili.”

Alibainisha kuwa ukosefu wa mazoezi kwa watoto huathiri afya zao, hivyo ni vizuri wazazi na walezi kuwahamasisha watoto wao kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zao ili kuepuka magonjwa ili taifa liwe na vijana wenye afya njema.

Eliwampuka Kintungi, katibu mtendaji wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Voice of Encouragement Tanzania (VET), linalojihusiaha na uwezeshaji watoto wa kike katika masuala ya elimu, afya na ukatili wa kijinsia, ambalo ndio liliandaa tamasha hilo, alisema ni vizuri kila mmoja akatenga muda wa kufanya mazoezi ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto wilaya ya kipolisi Kimara, Joyce Mapunda alisema kazi yao kubwa ni kutoa elimu ya ukatili na kuzuia pamoja na kuhamasisha michezo kwani afya bora inatokana na mazoezi.

Aprotuna Mapunda, mwalimu wa Sekondari ya Kibweheri, alisema wataendelea kuhamasisha michezo kwa wanafunzi kwa sababu tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa mtu anapojihisha na mazoezi ya kuushughulisha mwili ni kitu kizuri kwa ukuaji wa afya ya ubongo.

“Kama mnavyofahamu, michezo ni zaidi ya afya na burudani lakini baada ya tamasha hili, sote tumefurahi na miili yetu imeimarika,† alisema Mapunda.

Katika tamasha hilo la michezo, wanafunzi hao walichuana katika mchezo wa kuvuta kamba, kukimbiza kuku na kukimbia na gunia.

Kwa upande wake mshindi wa mbio za kukimbiza kuku, Glory Gervas, ambaye ni mwanafuzi wa kidato cha pili Sekondari ya Mbezi Inn alisema ushindi wake unatokana na mazoezi anayofanya na kwamba kuku huyo wataenda kunywa supu na wanafunzi wenzake shule kwao.

“Unapofanya mazoezi yanasaidia sana, yanatupa afya njema, uwezo wa kutambua, kujifunza kwa urahisi, na tabia nzuri ya kujichanganya na wengi kutokana na kufanya mazoezi,” alisema Gervas.

Hata hivyo, mshindi wa shindano la kula alikuwa ni Angela Isaya, mwanafunzi wa kidato cha kwanza sekondari ya Kibwegere, akifuatiwa na Shakila Hamis mwanafunzi wa kidato cha nne kutoka sekondari ya Kibwegrere, huku mshindi wa tatu akiwa ni Gloria Gervas kutoka sekondari ya Mbezi Inn.

Washindi hao walipewa zawadi ya vifaa vya shule ikiwemo madaftari, kalamu na sodo.

Related Posts