Mwanza. Mkazi wa Kitongoji cha Nyakasenge wilayani Magu mkoani Mwanza, Warioba Lucas, maarufu ‘Wevi’ (41) amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu mkoani humo akiuguza majeraha ya moto aliyoyapata baada ya kujimwagia Petroli kisha kujichoma moto.
Warioba anadaiwa kujitendea unyama huo jana Jumatatu Agosti 26, 2024, saa 5 asubuhi siku moja baada ya mume wake kudaiwa kuchukua fedha zake Sh40,000 na kunywea pombe, jambo linalotajwa kumkera.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Agosti 27, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema uchunguzi wa awali unaonesha mwanamke huyo alifikia uamuzi huo baada ya kuchoshwa na tabia za mume wake, Jumanne Ngika (45) kuchukua fedha za familia kwenda kuzitumia kwa ulevi na starehe nyingine.
Kamanda Mutafungwa amesema baada ya kujichoma moto, wananchi walibaini tukio hilo na kuvunja mlango wa chumba alimokuwemo na kukuta umeshasambaa kwenye nguo zake, kisha kuanza kuuzima kwa kutumia maji na mchanga na kufanikiwa. Hata hivyo, alikuwa ameshaungua sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Kitendo hicho kilimkasirisha sana yule mama majeruhi naye akaanza kunywa pombe hadi tarehe 26, 2024, akajifungia chumbani mwao akavaa nguo nyingi na kuamua kujichoma moto, katika tukio hilo mali kadhaa ziliungua japokuwa nyumba haikuteketea.”
“Majirani walijitokeza na kubomoa mlango huku wakimwaga maji na mchanga ili waweze kuzima moto na kumuokoa lakini wakati wanafanya hivyo tayari mama huyo alikuwa ameshapata majeraha makubwa sana mwilini,” amesema Mutafungwa.
Kamanda huyo amesema, “taarifa zilifika kituo cha Polisi, askari wetu walifika eneo la tukio kwa ajili ya kumuokoa lakini pia kufanya uchunguzi wa suala hilo. Alikuwa katika hali mbaya mwili wote ngozi ilikuwa imechubuka na alikuwa hawezi kuongea, alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Magu kwa ajili ya matibabu.”
Kamanda Mutafungwa amesema tayari jeshi hilo linamshikilia mume wake anayeitwa, Jumanne Ngika (45) kwa usalama wake na mahojiano kuhusiana na tukio hilo.
“Wanandoa hao wamekuwa katika migogoro ya mara kwa mara, mwanamume amekuwa akituhumiwa na mke wake ambaye ni majeruhi, kwa kufuja pesa za familia kwa matumizi ya kunywa pombe na starehe nyingine,” amesema kamanda huyo.
Askofu wa Kanisa la International Evengelical Assemblies of God Tanzania (IEAGT) mkoani Shinyanga, David Mabushi ameeleza kitendo cha kilichofanywa na majeruhi huyo cha kujimwagia mafuta kisha kujichoma moto kuwa, kimesababishwa na jamii kujitenga na Mungu.
Askofu Mabushi ameitaka jamii hususan wanandoa kujiweka karibu na Mungu na kuzingatia mafundisho ya vitabu vitakatifu.
Amesema wanaopitia changamoto katika mahusiano yao wawe wanawashirikisha wataalamu wa uhusiano ili wapate mwarobaini wake na kuepuka athari ikiwemo kuchukua hatua za kujiondoa uhai.
“Mtu asiye na hofu ya Mungu ndiyo anaweza kufanya hivyo akihisi analipa kisasi, tatizo la watu kujichukulia sheria mkononi limekuwa kubwa nchini cha kufanya watu wamrudie Mungu,” amesema askofu Mabushi.
Mwanasaikolojia wa kujitegemea na daktari wa magonjwa ya binadamu mkoani Mwanza, Jacinta Mutakyawa akizungumzia vitendo vya mauaji, amesema vinachangiwa na ongezeko la tatizo la afya ya akili, malezi mabovu, ubinafsi na wanandoa kukosa maarifa ya kukabiliana na changamoto.
Jacinta ameitaka jamii hususan wanandoa kupima afya ya akili na kutafuta suluhu ya matatizo yao kwa watalaamu, kuliko kuchukua uamuzi unaoweza kuleta madhara kwao na familia zao.