BAADA ya kutupwa nje ya michuano ya kimataifa mbele ya APR ya Rwanda, matajiri wa Chamazi, Azam FC watakuwa na kibarua kizito kesho Jumatano dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni katika mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Msimu uliopita Azam ilivuna pointi sita dhidi ya JKT Tanzania ilikuwa ni baada ya mchezo wa kwanza Desemba 11, 2023 kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wao wa nyumbani (Azam Complex), waliporudiana Mei 21 mwaka huu wakashinda kwa mabao 2-0, mabao yao yalifungwa na Feisal Salum na Abdul Suleiman ‘Sopu’ ambaye kwa sasa anauguza majeraha.
Tofauti na mazingira yalivyokuwa msimu uliopita, utamu wa mchezo wa safari hii utachochewa na namna ambavyo vikosi vya timu zote mbili vimetoka kujiimarisha katika dirisha kubwa la usajili hivyo kila upande utatumia silaha zake kwa mara ya kwanza katika ligi hiyo.
Katika mchezo huo, Azam ambao msimu uliopita walishika nafasi ya pili nyuma ya Yanga, itakabiliana na nyota wao wa zamani, John Bocco ambaye anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya maafande hao wa Jeshi la Kujenga Taifa ambao wamesalia katika ligi kupitia mlango wa mchujo ‘play off’.
Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Azam, Youssouph Dabo anaamini vijana wake wataanzia pale ambapo waliishia msimu uliopita kutokana na malengo waliyojiwekea licha ya kuondolewa mapema katika Ligi ya Mabingwa.
“Fokasi yetu kwa sasa ni ligi na mashindano mengine ya ndani, sisi ni kama askari tunatakiwa kunyenyua vichwa na kuendelea na mapambano uzuri ni kwamba msimu ndio kwanza umeanza kila kitu kinawezekana,” alisema.
Kwa upande wake, kocha wa JKT Tanzania, Hamady Ally anatambua ukubwa na ubora wa Azam FC hivyo wamejiandaa vizuri kukabiliana nao na kuhakikisha wanakuwa na mwanzo mzuri wa ligi.
“Kila kitu kuhusu maandalizi kimekamilika, sote tunajua kuwa Azam wanatimu nzuri pamoja na kwamba wameondolewa katika michuano ya kimataifa, sisi tumejiandaa vizuri ili kukabiliana na kuhakikisha tunakuwa na mwanzo mzuri wa msimu,” alisema kocha huyo.
Rekodi zinaonyesha ndani ya msimu minne ambayo timu hizo zimekutana katika ligi, Azam haijawahi kupoteza dhidi ya maafande hao tangu 2018, wameshinda mechi sita ikiwemo moja ya Machi 8, 2019 waliyotoa dozi ya mabao 6-1, wametoka sare mara mbili.
Licha ya mabosi wa Azam kuonyesha kuwa na imani na kocha wao,Youssouph Dabo pamoja na kuondolewa kwao katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR ya Rwanda, Msenegal huyo anaweza kuwa kikaaongoni kama atashindwa kupata matokeo katika mchezo wa leo wa ligi dhidi ya JKT Tanzania.
Taarifa za ndani zinaelezwa kuwa mabosi hao wanaweza kubadili maamuzi ya uvumilivu wao kwa kocha huyo na kuamua kumfuta kazi mara moja ikiwa mwenendo wa timu hiyo utakuwa wa kusuasua kulingana na uwekezaji mkubwa uliofanywa.