Na Said Mwishehe,Michuzi TV
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) CPA Amoss Makala amewataka wanachama wa hicho pamoja na wananchi kuwachagua wagombea watakaotokana na Chama hicho katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
CPA Makala ambaye pia ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam amesema zipo sababu za msingi za CCM kushinda ushindi wa heshima katika uchaguzi huo wa Serikali Mitaa mwaka huu kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana yakiwemo ya utekelezaji wa Ilani katika kuleta maendeleo ya wananchi.
Akizungumza wilayani Kigamboni alipokuwa akizungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara CPA Makala amesema kwamba mwaka huu kutakuwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambako ndiko ndio maamuzi ya wananchi wanafanya katika kuchagua viongozi wao ,hivyo ni uchaguzi muhimu.
“Lengo la Chama cha siasa ambacho kimesajiliwa ni kushika dola, Chama cha siasa ambacho kimesajiliwa hakifanyi kazi ya kuhubiri kuhusu kufika mbinguni maana hiyo ni kazi ya viongozi wa dini huko misikitini na kanisani lakini kazi ya Chama cha siasa ni kukamata dola.Ili ushike dola unatakiwa kushinda chaguzi mbili chaguzi ya Serikali ya Mtaa na uchaguzi Mkuu.
“Mafanikio ambayo yamepatikana yametokana na ushindi wa kishindo ambao CCM tuliupata mwaka 2019.Novemba 27 mwaka huu itafanyika uchaguzi wa Serikali za mitaa na kama CCM lengo lake ni kushika dola Wana CCM hakikisheni wagombea wa CCM wanashinda uchaguzi huo.
“Mwenyekiti wa Mtaa ndio anajua zahanati ijengwe wapi,ndio anajua maegesho ya magari yajengwe wapi,sasa ikitokea Mwenyekiti wa Mtaa ni wa upinzani halafu Diwani, Mbunge na Rais ni WA CCM mnawezaje kufanya maendeleo?
“Hivyo ili kwenda na kasi ya maendeleo ya Rais Dk.Samia ni lazima tuhakikishe wagombea wanaotokana na CCM wanashinda, ni kama vile uwe na tochi halafu katikati unabadilisha betri katikati taa haitawaka,”amesema Makala.
Akifafanua zaidi amesema amani na utulivu unatokana na muunganiko huo wa viongozi wa vitongoji na mitaa wanaotokana na CCM huku akieleza yeye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na alisumbuliwa na panya road lakini siri kubwa ilikuwa ni wenyeviti wa Serikali za Mitaa ambao wanajua mitaa yao.
“Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27 mwaka huu tunazima zote na tunawasha kijani.Mimi ndio Msemaji wa CCM ,ndio nakisemea Chama Cha Mapinduzi nataka niwahakikishie tutawaletea wagombea safi ambao hawana makando kando.
“Hatutaleta mgombea ambaye kesi zote za viwanja anahusika yeye, hatutaleta wagombea wa kusafisha na dodoki, tutaleta wagombea walio safi.Tunataka kushinda kwa ushindi wa heshima wa asilimia 99.9.
“Lakini ili kushinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa lazima wana CCM wajiandikishe katika daftari la Wakazi.Oktoba 1 daftari la wakazi litaanza, hivyo wananchi wakajiandilishe ili wajiandae na uchaguzi utakapofika basi waende kupiga kura. Tuandae watu wetu na wafuasi wetu ili wakajiandikishe,tunazo sabababu za kushinda na mojawapo ni utekelezaji wa Ilani ambao unatosha CCM kuomba imani ya wananchi.”
Aidha amesema sababu nyingine ya CCM kushinda uchaguzi wa Serikali za mitaa unatokana na vyama vya upinzan kupoteza muelekeo na sera pamoja na migogoro imekuwa mikubwa akitolea mfano CHADEMA ambako kuna mpasuko mkubwa, Tundu Lissu gari yake iliharibika na wana CCM wakachanga fedha Sh.milioni 5.3 kutengeneza gari yake.
“CCM tuko tayari kumnunulia gari jipya Tundu Lissu kama gari yake itaendelea kumsumbua.Wapo waliokuwa wanasema Lissu hatapokea fedha lakini alipokea na ameishukuru kwasababu CCM tulimchangia Lissu na sio CHADEMA.Kugombana kwao kwetu ni fursa hivyo tutaitumia kushinda.”
Wakati sababu ya tatu itakayowezesha CCM kushinda uchaguzi wa Serikali za mitaa,CPA Makala amesema Chama hicho kimeongeza idadi ya wanachama wanaojiunga kwa kasi imekuwa kubwa.
Hivyo ameendelea kuwakumbusha huu ni mwaka wa uchaguzi anaomba wananchi kuipa iamani CCM na kuhusu changamoto ambazo zipo Serikali itaendelea kutafuta ufumbuzi wake.