Dk Ndugulile kusuka, kunyoa uchaguzi WHO leo

Dar es Salaam. Mkutano wa Afya wa 74 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoendelea Brazzaville, Congo leo Jumanne, Agosti 27, 2024 unatarajiwa kumpitisha Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika ambapo miongoni mwa wagombea watano Tanzania inawakilishwa na Dk Faustine Ndugulile.

Wagombea wengine ni pamoja na Dk Boureima Hama Sambo (Niger) Dk N’da Konan Michel Yao (Cote d’Ivoire),  Dk Ibrahima Soc’e Fall (Senegal) na Dk Richard Mihigo (Rwanda).

Dk Ndugulile ambaye ni mwanateknolojia, mtunga sera, mwanasiasa na mwakilishi wa wananchi kutoka Jimbo la Kigamboni, Dar es Salaam kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) anawakilisha nchi baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwania kinyang’anyiro hicho.

Mawaziri wa Afya kutoka Kanda ya Afrika walianza mkutano huo jana Jumatatu baada ya kufunguliwa na Rais wa Congo, Denis Sassou Ng’uesso.

Iwapo azma ya Tanzania ya kuwania nafasi hiyo itakamilika, Dk Ndugulile atachukua nafasi ya Dk Matshidiso Moeti kutoka Botswana, ambaye muda wake unamalizika Agosti 2024 baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo tangu mwaka 2015.

Katika mkutano huo muhimu, ujumbe wa Tanzania unajumuisha wataalamu na viongozi kutoka Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wabunge wa Bunge la Tanzania.

Wajumbe hawa wanatarajia kushiriki mikutano ya pembezoni ili kujadili masuala muhimu na kuhakikisha upatikanaji wa kura kutoka kwa nchi wanachama wapatao 47 wa WHO.

Dk Ndugulile ni daktari mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 kwenye afya ya jamii ndani na nje ya nchi. Amewahi kuwa mwakilishi wa Bara la Afrika katika Taasisi ya kimataifa ya Ukimwi na mwanzilishi wa mtandao wa dunia kuhusu ugonjwa wa TB.

Pia amewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hapa nchini.

Machi 11, 2023, Dk Faustine Ndugulile aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya ushauri masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge duniani (IPU). Kwa uteuzi huo unaofanywa na Rais wa umoja huo wa mabunge duniani, ulimfanya Dk Ndugulile kuwa sehemu ya wabunge 12 duniani wanaoishauri IPU kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu afya.

Uteuzi huo ulianza Februari 2023 ambao utadumu miaka minne.

October 24, 2023 Dk Ndugulile achaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika Jijini Luanda nchini Angola.

Kamati ya ushauri ya masuala ya afya, ina majukumu ya kushauri mabunge ya nchi na umoja wa mabunge duniani kuhusu masuala mbali mbali yanayohusu afya.

Pia, katika uchaguzi huo, Seneta Lorraine Clifford-Lee wa Ireland alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, huku wajumbe wengine wa kamati hiyo wakitokea nchi za Mexico, Croatia, Cuba, Pakistani, Urusi, Saudi Arabia na Uzbekistan.

Katika mkutano huu, Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson alichaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani IPU Oktoba 27, 2023.

Related Posts