KOCHA mkuu wa Simba, Fadlu Davids ameanza vyema Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kukiongoza kikosi chake kuibuka na ushindi katika mechi mbili kilizocheza, lakini wakati timu ikiongoza msimamo wa ligi ametoa maagizo mawili ambayo anataka yafanyiwe kazi kwa haraka.
Agizo la kwanza ni kupandishwa kwa wachezaji watano kutoka katika kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 kwenda katika kikosi cha wakubwa ambalo limeshaanza kufanyiwa kazi kwa wachezaji wawili, Daruwesh Ahmed na Okech Nyembe kutumika kwenye ligi.
Kocha huyo ameagiza kwamba wachezaji hao watano wawe wanashiriki kwa asilimia 100 katika pro-gramu za timu kwa maana ya kambi, mazoezi ya pamoja na kupata huduma zote ambazo wanapata wachezaji wa kikosi cha wakubwa.
“Mwalimu Fadlu na benchi lake la ufundi wameanza kufuatilia kwa ukaribu timu yetu ya vijana na kutakuwa na mechi ambazo itacheza wakati ligi itakaposimama, ambazo zitampa fursa kuwaona wachezaji na yeye mwenyewe atafanya uteuzi wa wachezaji wa kuwapandisha kwenye kikosi cha wakubwa,” chanzo ndani ya Simba kimeliambia gazeti hili.
Imeripotiwa pia kocha Fadlu ametaka awe anakutana mara kwa mara na makocha wa vikosi vyote vya vijana na kile cha wanawake cha Simba ili kubadilishana uzoefu wa utekelezaji majukumu.
“Miongoni mwa mambo ambayo kocha Fadlu amesisitiza kuwa anayahitaji ni timu zote za Simba kuwa na falsafa inayofanana kuanzia kikosi cha wakubwa na hivyo vingine. Anataka kuona siku za usoni ina-kuwa rahisi kwa mchezaji wa timu ya vijana kuingia katika kikosi cha wakubwa na kucheza kwa vile tayari anakuwa anafahamu falsafa ya timu kuanzia huko chini,” kilifichua chanzo hicho.
Meneja wa habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa Fadlu ametoa maagizo hayo ili kutekeleza kwa ufasaha kanuni mojawapo ya Ligi Kuu msimu huu ambayo inalazimisha kila timu kuwa na wachezaji wawili wa kikosi cha vijana kwenye mechi ya ligi.
“Kanuni zinasema kila mechi kuwa na wachezaji wawili kutoka kikosi cha vijana kwenye mchezo sasa mwalimu akasema kama ni hivyo, anahitaji kuwa na wachezaji watano kutoka timu ya vijana ambao ata-fanya nao program za mazoezi na atakaoridhika nao wawili atakuwa akiwatumia kwenye mechi ya ligi,” alisema Ahmed.
Katika hatua nyingine, Simba imepata habari njema kutokana na kupona majeraha kwa winga, Joshua Mutale ambaye ameshaanza mazoezi mepesi na wiki hii ataungana na wenzake kikosini.