Janga la usomaji wa zimamoto vyuoni

Unaposikia ‘zimamoto’ tafsiri inayoweza kuja haraka kichwani mwako ni kitendo cha kutumia maji, mchanga au vifaa maalum kuzima moto.

Picha nyingine inayoweza kujengeka akilini ni lile gari maalum linalotumiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pale yanapotoa huduma ya kuzuia majanga ya moto katika maeneo mbalimbali.

Hata hivyo, neno hilo limepata umaarufu sana kwa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu hasa inapokaribia kipindi cha mitihani.

Kwao neno ‘zimamoto’ humaanisha aina ya usomaji ambao mwanafunzi anasoma kwa kukariri muda mfupi kabla ya kuingia kwenye mtihani. Neno lingine maarufu kwa aina hiyo ya usomaji ni ‘kutoboa’

Mariam Ahmed anayesoma mwaka wa pili katika chuo kikuu kimoja nchini, anasema wanafunzi wengi huamua ‘kutoboa’ kwa sababu muda mwingi wanautumia katika mambo yasiyohusiana na masomo.

‘’Hivyo kinapofika kipindi cha mtihani, wanajikuta wana mlundikano wa mada nyingi za kusoma. Sasa ili waweze kufanya mtihani inabidi wakariri wapate chochote cha kujaza,’’ anasema.

Mariam anaungwa mkono na Hyder Peter, mwanafunzi wa mwaka wa tatu anayesema: “Hii ndio sababu ukipita maeneo ya chuo kipindi cha karibu na mitihani hadi usiku wa manane, utakuta wanafunzi wapo darasani wanajisomea.’’

Ni mtindo mbovu wa usomaji

Mdau wa elimu na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Faraja Kristomus anasema aina hiyo ya usomaji, haina manufaa chanya kwa mwanafunzi kwani baada ya kujifunza kile anachofundishwa, huishia kukariri ili tu aweze kujibu mitihani.

Kristomus anasema mtu anaposoma kwa kukariri kile ambacho anakipata hukaa katika sehemu ya kumbukumbu ya muda mfupi na pale anapomaliza matumizi yake huweza kusahau, jambo ambalo halitakiwi kwa msomi.

Anasema aghalabu wanaotumia mtindo huo kujisomea hujikuta wakisahau maarifa mengi waliyosoma awali.

‘’Wengine mara tu baada ya kumaliza mitihani huwa wanasahau yote waliyojifunza. Hiyo ndiyo sababu baadhi ya watu hutafsiri kuwa na maarifa katika kujifunza, ni kile kinachobaki baada ya kusahau vingine ulivyojifunza, ”anasema.

Aina hiyo ya usomaji anasema inasababisha kuzalishwa kwa wataalamu waliokosa ubobevu kwenye taaluma zao.

‘’ Hii ni kwa kuwa mwanafunzi anakuwa amekariri baada ya kujifunza, hivyo maarifa yake katika fani husika huwa ya kiwango kidogo.Kujifunza ni mchakato wa muda mrefu ambao unahusisha kujua vitu kwa hatua, ”anasema na kuongeza kuwa mara nyingi wasomaji wa mtindo huo wanakosa kujiamini kwa kuwa na uelewa mdogo wa maarifa.

Kwa upande wake, Muhanyi Nkoronko ambaye ni mtafiti wa elimu anasema aina hiyo ya usomaji, inaweza kuchochea baadhi ya wanafunzi kufanya udanganyifu katika mitihani kutokana na kuwa hawajajiandaa vizuri.

Pia anasisitiza jambo hilo linasababisha kuzalishwa kwa wataalam ambao hata watakapoajiriwa, wakikabidhiwa majukumu hawatoyafanya kwa ufanisi.

‘’ Kuna athari kwa wataalamu waliosoma kwa mtindo huu kushindwa kutumia taaluma zao vizuri kutatua changamoto zinazoikabili jamii. Pia kunaweza kuwa na wahitimu ambao hawawezi kuhoji wala kujibu hoja jambo ambalo si jema kitaaluma,’’ anafafanua.

Mwanasaikolojia Modesta Kimonga anasema aina hiyo ya usomaji, ina athari katika upande wa saikolojia na akili ya mwanafunzi.

Anasema kwa kuwa mwanafunzi husika huwa hajajiandaa vizuri, husababisha kuwa na hofu na hata msongo wa mawazo.

“Anapokuwa na hofu, inaweza ikamfanya kutofanya vizuri katika mitihani yake kutokana na kukosa utulivu,”anasema.

Aina hii ya usomaji inatajwa kama moja ya sababu zinazochangia wanafunzi kujihusisha na vitendo vya udanganyifu.

Mhitimu wa elimu ya juu, Abby Kwesa, anasema ikiwa mwanafunzi anasubiri kusoma hadi mitihani, huyu ni rahisi kwake kufanya udanganyifu.

“Kozi zinafundishwa kwa mihula au simesta, hiyo ni miezi nadhani sio chini ya mitatu. Mtu anawezaje kwa siku moja kuelewa alichofundishwa kwa miezi hiyo? Mtu wa aina hii atatafuta namna ya kurahisisha mambo na hapo ndipo vitendo vya udanganyufu wa mitihani huibuka, ” anasema.

Anavitaja vitendo hivyo kuwa ni pamoja na kuingia na majibu katika vyumba vya mitihani, kuibia kwa watahiniwa wengine, utoaji wa rushwa kwa wahadhiri na mbinu nyinginezo za udanganyifu wa kimitihani.

Hata hivyo, kwa baadhi ya watu akiwamo mwalimu mstaafu, Bakari Kheri, usomaji wa zimamoto ndio mtindo wao wa ujifunzaji na pengine tabia hiyo wametoka nayo kutoka madaraja ya chini ya elimu.

Kheri aliyemaliza masomo ya ualimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya mwanzoni mwa 2000, anaeleza:

‘‘Kimsingi, sio usomaji wa kuunga mkono kwa kuwa hapa kunakuwa ni kukariri zaidi kuliko kuelewa unachosoma, lakini niseme kuwa kwa baadhi yetu huo ndio mtindo wa kujifunza, tumeutumia miaka yote na tukafaulu tena kwa madaraja mazuri tu.

Mimi binafsi kwa mfano, hata kama naingia darasani kumsikiliza mhadhiri, kile kinachofundishwa hukiacha palepale.Sikuwa na utaratibu wa kujisomea kwa maana ya ratiba maalumu kila siku. Muda mwingi nilifanya mambo nje ya taaluma. Lakini kwa kuwa nilikuwa bado masomoni, staili yangu ilikuwa ndio hiyo, nacheza na ratiba ya mitihani na kusoma kujiwinda na huo mtihani.”

Mwalimu Kheri hata hivyo ana ushauri kwa wanafunzi wanaotumia mtindo huo wa usomaji, anasema:

‘’Ni mtindo unaoumiza, mimi kuna nyakati nililazimika kukesha kama nina mtihani siku inayofuata. Huku ni kujiumiza, lakini vipi kama mtihani au jaribio litatolewa kwa kustukiza? Ni dhahiri mwanafunzi huyu atafeli. Najua mtindo huo unatumiwa na baadhi ya watu, lakini sishauri wadumu nao. Wajitahidi kusoma kwa ratiba iwe kuna mitihani au la. Kwanza kazi inayokupeleka chuo ni kusoma na si vinginevyo. Sio mtindo mzuri wa usomaji.”

Wataalamu hao wanashauri wanafunzi wanaosoma kwa kuzima moto kuacha tabia hiyo kwani haina ustawi mzuri wa taaluma na afya zao kwa ujumla. Wanasisitiza kuwa ni vyema mwanafunzi kujiwekea utaratibu wa kuwa anajisomea mara kwa mara kile anachojifunza ili aweze kuelewa vizuri.

Related Posts