Maagizo ya Dk Mwinyi kwa Takukuru, Zaeca

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amezitaka Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi (Takukuru na Zaeca) kuongeza ushirikiano ili kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Agosti 27, 2024 Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila aliyefika kujitambulisha.

Chalamila aliteuliwa Agosti 14, 2024 na kuapishwa Agosti 15 na Rais Samia Suluhu Hassan, akichukua nafasi ya Salum Hamduni aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga.

Rais Mwinyi amezitaka taasisi hizo mbili kuzidisha ushirikiano hasa kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo kwa masilahi ya Taifa.

“Ipo haja ya kuongeza ushirikiano, hususani katika miradi ya kimkakati ya maendeleo kuwe na tija na ilete matokeo chanya,” amesema Dk Mwinyi.

Amempongeza Chalamila kwa uteuzi alioupata na kumtakia heri kwenye majukumu yake mapya.

Rais Mwinyi amesifu jitihada za Zaeca za kuendeleza ufanisi wa majukumu hasa kwenye miradi ya Serikali kwani wanawajibika ipasavyo.

Chalamila amemuahidi Rais Mwinyi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Zaeca na Takukuru katika kufanikisha majukumu yao.

Amesema Takukuru na Zaeca wanashirikiana kwenye mambo mengi tangu waliposaini mkataba wa ushirikiano mwaka 2012, ikiwemo kujengeana uwezo, kushirikiana kwenye masuala ya uchunguzi wa kazi zao, kushiriki mikutano ya pamoja ya kikanda na kitaifa.

Chalamila amesifu na kupongeza juhudi za maendeleo makubwa zilizofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya uongozi wa Rais Mwinyi.

Amesema mbali na majukumu mengine waliyonayo Takukuru na Zaeca, imekuwa rahisi kwao kushirikiana hasa kuwadhibiti wahalifu wa pande mbili za Muungano wanaojaribu kukimbilia kwenye mipaka ya sehemu hizo Tanzania Bara na Zanzibar.

“Tunaahidi kuendeleza maono yenu viongozi wetu, na ushauri wenu katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi kwa kushirikiana na Zaeca,” amesema.

Amesema wataendelea kufanya uchunguzi katika miradi ya maendeleo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati kwa thamani ya fedha zinazokuwa zimetengwa bila kupotea hata shilingi.

Related Posts