Mbunge aibua sakala la utekaji bungeni, Spika asema ni mazito

Dodoma. Malalamiko ya watu kuuawa, kutekwa na kupotea yametinga bungeni ambapo Mbunge wa Nkasi Kaskazini (Chadema), Aida Khanani ameomba mwongozo wa Spika ili chombo hicho kijadili na kutoa maelekezo kwa Serikali ili haki ya kuishi iendelee kupatikana.

Mbunge huyo ameomba mwongozo huo leo Jumanne Agosti 27, 2024 mara baada ya kupindi cha maswali na majibu bungeni.

Amesema kwa siku za karibuni kumekuwa na matukio ya utekaji, upoteaji na mauaji yanayoendelea kwa watoto, wanaharakati, viongozi wa vyama vya siasa na makundi mbalimbali nchini.

“Kwa kuwa jambo hili limeshazungumza na taasisi mbalimbali ambazo wameshafanya tathimini, Tume ya Haki za Binadamu, TLS (Chama cha Wanasheria wa Tanganyika), pamoja na vyama vya siasa ikiwemo Chadema,” amesema.

Amesema kwa kuwa jambo hilo lina maslahi na linaumiza Watanzania na Bunge liko kwa ajili ya Watanzania, ameomba atoe hoja na Bunge limuunge mkono.

“Bunge hili lijadili na kutoa maelekezo kwa Serikali ili angalau Watanzania waendelee kupata haki yao ya kuishi,” amesema.

Akijibu mwongozo huo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema mambo aliyozungumza mbunge huyo ya kuuawa, kupotea na kutekwa kwa watu ni mazito.

Amesema taasisi mbalimbali alizotaja mbunge huyo kuwa zimezungumzia suala hilo, yeye hajazisikia wala kupitia taarifa zao ili kuona wamelieleza kwa sura ipi.

“Kwa yale mambo ambayo yako nje ya utaratibu wa kawaida ama yale ambayo Bunge linaona Serikali haifanyi lolote basi Bunge inaweza kuchukua hatua hizo.

Pamoja na kwamba mheshimiwa Aida alitoa hoja kabla ya kanuni ya 54… lakini nilimwacha afanye hivyo kwa sababu niliona na wabunge wengine waliounga mkono,” amesema.

Amesema lakini kanuni ya 54 inamtaka mbunge kutoa maelezo ya mwongozo anaouomba na Spika akishajiridhisha ndio kwa kutumia kanuni ya 55 atoe maelezo kwa kina ili Bunge liweze kumuunga mkono kwa wabunge 10 kusimama ama la.

“Hata hivyo jambo aliloeleza la utekaji, mauaji ni mambo ambayo kama uchunguzi umefanyika ama unapaswa kuwa uchunguzi umefanywa. Sio mtu kama mimi nikasimama, nikasema kuna mtu sijamuona ama nikasema kuna mtu ameuawa.

Mimi simjui aliyeuawa sasa Bunge itakuwa inailekeza nini Serikali katika mazingira kama hayo,” amesema.

Dk Tulia amesema kwa sababu hizo alizozisema pamoja na uzito wa mambo hayo, Serikali ichukue hatua zile inazochukua na kama zile za kawaida zinashindikana basi iongeze nguvu kwenye kuhakikisha raia wanakuwa salama.

“Lakini kwa maana ya hoja ya dharura ambayo Bunge linaweza kujadili, hapana hajakidhi masharti ya kanuni ya 55,” amesema.

Related Posts