Mjadala wanawake, wanaume, watoto kulazwa wodi moja Mwanza

Dodoma. Mbunge wa Ilemela (CCM), Angelina Mabula amesema katika Kituo cha Afya cha Sangabuye wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza kilipandishwa hadhi 1999 kutoka zahanati lakini kituo hicho hadi leo kina wodi moja tu ambayo hulazwa wanawake, wanaume na watoto.

“Je ni lini Serikali itakamilisha miundombinu pale ikiwa ni pamoja na kujenga uzio,” amehoji Dk Mabula.

Baada ya swali hilo Spika Dk Tulia Ackson akahoji wanawezaje kulaza wodi moja wanaume, wanawake na watoto.

“Napata wasiwasi wanalazaje wanawake, wanaume na watoto katika wodi moja, wameweka mapazia ama ni nini,” amehoji Dk Tulia.

Akijibu swali hilo, Dk Mabula amesema “Unaweza kukuta kitanda hiki amelala mwanaume, kingine kina mwanaume ana mtoto ndani ya wodi moja na tangu mwaka 1999 miundombinu hiyo haijakamilika na nilishauliza swali hilo.”

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange amesema kwa mujibu wa sera ya Wizara ya Afya, hairuhusiwi kuwalaza wanawake na wanaume katika sehemu moja.

“Kwa taarifa hii tunaipokea kuna tatizo katika uongozi wa hospitali na manispaa yenyewe .Kwa hiyo naomba nichukue hoja hii nimwelekeze mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela kwa niaba ya Waziri wa Nchi leo afike pale mara moja na atupe taarifa rasmi ofisi ya Tamisemi,” amesema.

Amesema taarifa hiyo itawawezesha kuona jinsi nzuri ya kutoa huduma kwa wagonjwa kwa kuwa haikubaliki kulaza wanawake na wanaume kwenye wodi moja.

“Manispaa ya Ilemela ina uwezo wa kuanza ujenzi wa wodi nimuagize mkurugenzi kupitia mapato ya ndani kwa dharura wafanye reallocation (ibadilishe matumizi ya fedha) wakati ofisi ya Rais Tamisemi ikitafuta fedha kwa ajili ya wodi hiyo muhimu,” amesema.

Baada ya majibu hayo, Dk Tulia alimuagiza Dk Dugange aende kutafuta taarifa kwa mkurugenzi, halafu baadaye atampa nafasi ili aeleze wanaume na wanawake wanalalaje wodi moja.

Amesema lengo ni kuweka vizuri kumbukumbu rasmi za Bunge kuhusiana na changamoto iliyoelezwa na mbunge huyo.

Related Posts