Polisi yamdaka anayedaiwa kuiba mtoto wa miaka minne

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi linamshikilia Zakia Mohamed (26) mkazi wa Mikwambe wilaya ya Kigamboni jijini Dar es salaam kwa tuhuma za kumuiba mtoto Zulkalya Ndambwe (4) tangu Agosti 8, 2024.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi iliyotolewa leo Jumanne Agosti 27, 2024, na Msemaji wake, David Misime, Zakia amekiri kumuiba mtoto huyo na anaendelea kushikiliwa ili kukamilisha uchunguzi.

“Imebainika kilichomfanya kutenda tukio hilo ni baada ya kupata taarifa ya mtu aliyekuwa anatafuta mtoto asiye na wazazi na anaishi katika mazingira magumu ili aweze kufuata taratibu za kumuasili.

“Kutokana na tamaa zake yeye akaona ni dili amepata na akisukumwa na tamaa hizo akaenda kuiba mtoto huyo,”Jeshi la Polisi limedai katika taarifa hiyo.

Jeshi la Polisi limebainisha kwamba, Zakia alipotakiwa kuanza kutekeleza utaratibu hasa kuwapeleka ndugu wa mtoto, vyeti vyake pamoja na kiongozi wa Serikali ya mtaa kwa utambuzi alisita na kushindwa kutekeleza masharti hayo, ndipo alipotiliwa shaka.

 “Mashaka mengine yalijitokeza pale alipoanza kudai ajengewe nyumba ya vyumba vitatu au apewe Sh50 milioni,”imesema taarifa hiyo.

Kutokana na taarifa za kupotea kwa mtoto huyo tayari zilishasambaa maeneo mbalimbali, Agosti 23, 2024 Jeshi la Polisi lilipokea taarifa  kutoka kwa raia wema  mtoto huyo amepatikana Mikwambe jijini Dar es Salaam akiwa na mama mmoja.

 “Askari baada ya kupokea taarifa hiyo walifanikiwa kumkamata Zakia Mohamed,”imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, uchunguzi wa awali ulibaini mtoto huyo alichukuliwa na mwanamke mmoja mweupe alipokuwa anacheza na watoto wenzake.

Related Posts