Dar es Salaam. Raia wa Burundi, Kabura Kossan (65) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kughushi kitambulisho cha Taifa (Nida) na cha Mpiga kura.
Vilevile anadaiwa kutakatisha Sh8 milioni zilizotokana na kununua eneo lenye ukubwa wa heka 100 lililopo Kijiji cha Kibesa, Wilaya ya Mkuranga, huku akijua anaishi nchini Tanzania kinyume cha sheria.
Mshtakiwa huyo amesomewa mashtaka yake leo Jumanne, Agosti 27, 2024 na wakili wa Serikali, Aaron Titus, Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.
Hata hivyo, kabla ya kusomewa shtaka hilo Hakimu Swallo amesema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.
Hakimu Swallo amesema mshtakiwa hatakiwi kujibu chochote kutokana shtaka la kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana.
Akimsomea mashtaka hayo, wakili Titus amedai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 24289/ 2024.
Amedai katika shtaka la kwanza, Kossan anakabiliwa na shtaka la kuwepo nchini bila kuwa na kibali.
Anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 17, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inadaiwa siku hiyo mshtakiwa akiwa raia wa Burundi, alikutwa akiishi nchini bila kibali.
Shtaka la pili, katika tarehe isiyofahamika ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mshtakiwa alighushi Kitambulisho cha Mpiga Kura chenye jina la Charles Ng’andu kwa lengo la kuonyesha kuwa kimetolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Wakili Titus amedai shtaka la tatu ni kuwasilisha kitambulisho hicho cha kughushi cha Mpiga kura kwa maofisa wa Polisi.
Shtaka la nne, mshtakiwa huyo anadaiwa katika tarehe isiyofahamika, alighushu kitambulisho cha Taifa chenye jina la Charles Ng’andu akionyesha kuwa kimetolewa na Mamlala ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Iliendelea kudaiwa kuwa mshtakiwa huyo baada ya kughushi Kitambulisho cha Nida, alikiwasilisha kwa maofisa wa Polisi, wakati akijuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Shtaka la sita ni kutakatisha fedha, tukio analodaiwa kulitenda kosa hilo Septemba 15, 2010 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa akiwa raia wa Burundi aliweza kujipatia eneo lenye ukubwa wa heka 100 lililopo kijiji cha Kibesa, Wilaya ya Mkuranga kwa gharama ya Sh8 milioni, huku akitambua kuwa fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la kuishi nchini bila kuwa na kibali.
Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Swallo alisema shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili mshtakiwa huyo, halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo ataendelea kukaa rumande hadi kesi yake itakapoisha.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Swalloa aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 9, 2024 kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande.