REA yamtaka anayeendeleza mradi wa umeme Maguta kuongeza kasi

Na Mohamed Saif- Iringa

Serikali imemtaka anayeendelezamradi wa kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji wa Maguta uliopo Kijiji cha Masisiwe wilayani Kilolo, Iringa kuukamilisha kwa wakati.

Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage ametoa maelekezo hayo Agosti 26, 2024 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambao umefikia asilimia 95.

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi ZECO ambaye Makao Makuu yake yapo nchini Italia, ametakiwa kuhakikisha makubaliano ya utekelezaji wa mradiyanatekelezwa kwa wakati ili ukamilike Desemba 2024.

Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage (kushoto) akikagua miundombinu ya Bwawa la mradi wa kufua umeme wa Maguta.

“Hatua iliyofikiwa inaridhisha, hakuna kikwazo kinachosababisha mradi uchelewe, Mkandarasi anapaswa kuhakikisha ifikapo Desemba mwaka huu awe amekamilisha na umeme umeingia kwenye Gridi ya Taifa,” ameelekeza Mhandisi Advera.

Mhandisi huyo amefafanua kuwa mradi umesanifiwa kuzalisha Megawati 2.4 na kwamba unatekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza inayoendelea hivi sasa itazalisha megawati 1.2.

Amesema licha ya kuongeza umeme kwenye Gridi ya Taifa, mradi utazalisha ajira kwa wananchi wa eneo la mradi, utapunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa, ni rafiki kwa mazingira, utaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye maeneo mengi na hivyo kuleta chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Kilolo na maeneo mengine.

“Kukamilika kwa mradi huu kutakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa maeneo haya na maeneo mengine pia; umeme ni injini ya uchumi hivyo tunatarajia kuona maendeleo makubwa baada ya kuanza uzalishaji wa umeme,” amesema.

Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage akielekeza jambo alipotembelea Mradi wa kufua umeme wa Maguta kwa kutumia maporomoko ya maji.

Mhandisi Advera amebainisha kuwa mradi unatumia Nishati Safi na Salama kutokana na maporomoko ya maji hivyo ili uwe endelevu, hukun akitoa wito kwa kila mwananchi kulinda na kutunza mazingira ya maeneo ya vyanzo vya maji.

“Umeme unaokwenda kuzalishwa hapa ni wa maporomoko ya maji, sasa tusipolinda mazingira yanayozunguka hivi vyanzo vya maji yaani hii mito tutasababisha mradi ushindwe kutupa matokeo tunayoyatarajia,” amesisitiza Mhandisi Advera.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi kwa ujumla, msimamizi wa mradi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Lung’ali Natural Resources Co. Ltd inayosimamia mradi huo kwa niaba ya Kanisa Katoliki-Parokia ya Jimbo la Iringa, Padri Luciano Mpoma ameishukuru Serikali kwa mchango wake katika kuhakikisha mradi unakamilika.

Amesema mradi unatekelezwa kwa ufadhili wa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuendeleza Mitaji kwa ajili ya Maendeleo (UNCDF).

“REA imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mradi unafanikiwa na unaleta manufaa yanayokusudiwa. Mara zote wamefika hapa kukagua na kutushauri tunawashukuru sana,” amepongeza.

Miongoni mwa majukumu ya msingi ya REA ni pamoja na kuwezesha ujenzi wa miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati Jadidifu ambayo ni Nishati Safi na Salama.

Related Posts