Dar es Salaam. Imeelezwa asilimia 69.4 ya wafanyakazi nchini hawana mikataba ya ajira, hali inayoonekana kukiuka haki zao.
Hayo yamebainishwa katika ripoti ya Biashara na Haki za Binadamu iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2023/24 iliyozinduliwa leo Agosti 27, 2024 jijini Dar es Salaam.
Ripoti hiyo inaonyesha changamoto hiyo imeongezeka kwa asilimia 4.8 kutoka asilimia 64.6 mwaka 2021/2022.
“Wafanyakazi waliodai kuwa na mikataba walikuwa wengi katika mikoa ya Arusha (asilimia 94), Dar es Salaam (asilimia 87), Dodoma (asilimia 85), Geita (asilimia 85), Mbeya (asilimia 85) na mikoa ya chini ilikuwa ni Mara (asilimia 15), Pwani (asilimia 49), Mwanza (asilimia 55), Morogoro (asilimia 55), na Mtwara Mtwara (asilimia 59),” amesema Wazambi Fundikira aliyewasilisha ripoti hiyo.
Wakati wafanyakazi wengi wakikosa mikataba ya kazi, ripoti imeeleza ni asilimia 37 pekee wanatambua uwepo wa vyama vya wafanyakazi nchini.
“Changamoto hii inaendana na nyingine kama vile kufukuzwa kazi kinyume cha taratibu na sheria za nchi, kutonufaika na mifuko ya hifadhi ya jamii na kiwango cha mshahara kisichoendana na gharama za sasa za maisha,” inaeleza ripoti hiyo.
Kuhusu haki za makundi maalumu, amesema wanawake na watu wenye ulemavu wameendelea kuwa waathirika katika upatikanaji wa ajira, huduma, na mazingira muhimu.
Akizungumzia mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wa ndani, Wazambi amesema wamebaini changamoto kadhaa zikiwamo za mazingira magumu ya miundombinu, kutokuwepo kwa miundombinu ya kutupa taka na tatizo la Wamachinga.
“Wafanyabiashara wengi waliohojiwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga na Iringa walitaja wafanyabiashara wajulikanao Wamachinga kama kikwazo kikubwa. Walisema kuachiwa kwa machinga ambao hawalipi kodi wanaathiri biashara zao, hasa kutokana na tabia zao za kuuza bidhaa nje ya masoko na kuwazuia wafanyabiashara wanaolipa kodi,” amesema.
Akizungumzia haki ya kumiliki ardhi, Wazambi amesema changamoto zilizoelezewa katika eneo hilo ni ucheleweshwaji wa malipo ya fidia, tathmini ya ardhi isiyoendana na hali ya maisha, na ushirikishwaji mdogo wa wananchi katika utwaaji wa ardhi kwa ajili ya shughuli za uwekezaji, hususani katika maeneo yenye shughuli za uziduaji.
“Asilimia 16 pekee walikiri kuhusu ushirikishwaji wa kutosha kwa wananchi katika eneo hili,” amesema.
Kwa upande wa haki za mazingira amesema kumekuwa na changamoto za hasa kwenye uchafuzi wa hewa na ardhi.
“Kampuni nyingi hazina sera za mazingira zenye ufanisi wa kutunza na kurudisha hali ya mazingira baada ya shughuli za uwekezaji. Ni takribani asilimia nne pekee ya kampuni zimeonekana kuwa na sera za utunzaji mazingira,” amesema.
Akizungumzia uwajibikaji wa kampuni (CSR), amesema ni asilimia 56 ya wanajamii waliokubali kunufaika na kampuni zinazorudisha kwa jamii.
“Hata hivyo, kampuni hizi zimeonekana kukiuka zaidi haki za kazi, ajira na haki za mazingira katika utendaji wa shughuli za biashara,” amesema.
Akizungumza baada ya kuzindua ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji mstaafu Mathew Mwaimu amesema katika tathmini waliyofanya kati ya mwaka 2013 hadi 2017 ilionekana shughuli za biashara zina faida kubwa katika kuimarisha maendeleo ya uchumi, kijamii na kisiasa na kiutamaduni.
“Kwa upande mwingine shughuli za biashara na uwekezaji zina manufaa makubwa kwa uchumi wa nchi kwa ujumla, husababisha uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa msingi ya utawala bora, hususani katika utwaaji wa ardhi kwa ajili ya shughuli za uwekezaji usiozingatia misingi ya sheria,” amesema.
Amesema kwa sasa THBUB imepewa jukumu la kuratibu uandaaji wa mpangokazi wa haki za binadamu na biashara unaotakiwa kukamilika mwaka huu.
Akizungumza baada ya ripoti kuwasilishwa, Katusume Kafanabo kutoka Chama cha Wafanyakazi na Kilimo (TPAWU), amesema kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo wafanyakazi, wengine hutumia njia ya majadiliano, wengine kisheria, wengine migomo baridi ili kupata suluhisho.
“Kwa mfano kwa miaka minne mfululizo wafanyakazi wa mashamba ya chai, waliamua kugoma baada ya kuona majadiliano na sheria yameshidikana,” amesema.
Amesema kuna changamoto ya waajiri kukataa vyama vya wafanyakazi katika maeneo ya kazi.
“Baadhi ya waajiri wanawafukuza wafanyakazi wanaoonekana kuwa na uelewa wa sheria za kazi,” amesema.
Akizungumzia masilahi, amesema japo sheria za kazi zinasema kila baada ya miaka mitatu Serikali inatakiwa ifanye mapitio ya nyongeza za mishahara, lakini mapitio hayakufanyika tangu mwaka 2013 hadi 2022.
Kuhusu changamoto za ardhi, Joyce Komanya wa kitengo cha biashara na haki za binadamu cha LHRC, amesema katika utafiti walibaini wananchi wengi hawashirikishwi katika utwaaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
“Changamoto nyingine ni ubadilishwaji wa ardhi kutoka ya kijiji na kuwa ardhi ya jumla. Wengi wanalalamika kutopewa taarifa wakati wa ubadilishwaji wa ardhi, wakati taarifa hizo zipo halmashauri na Kituo cha Uwekezaji Tanzania –TIC,” amesema.
Hata hivyo, mwanasheria kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Method Msokele amesema utwaaji wa ardhi hufuata utaratibu ikiwa pampoja na kutoa taarifa kwa umma.
“Hivyo hakuna mtu ambaye ardhi yake imechukuliwa bila taarifa. Kwanza Waziri wa Ardhi hutoa taarifa kupitia gazeti la Serikali na kisha hatua nyingine hufuata,” amesema.