Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema changamoto ya ucheleweshaji wa mafao kwa wastaafu haipo tena baada ya utekelezaji wa sheria inayotaka malipo kufanyika ndani ya siku 60 tangu kustaafu kwa mtumishi.
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Agosti 27, 2024 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya.
Katika swali hilo, Bulaya amesema Serikali imekuwa ikichukua fedha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na kwenda kuwekeza katika miradi ambayo urejeshaji wake unachelewa au miradi isiyokuwa na tija kabisa kama Dege Beach, hivyo kuleta usumbufu kwa wastaafu wanapotaka kuchukua mafao yao.
“Ni lini Serikali mtafanya tathimini katika miradi yote na kugundua hasara iliyojitokeza kutokana na kuwekeza katika miradi isiyo na tija,” amehoji Bulaya.
Akijibu swali Katambi amesema wameshaandaa mwongozo maalumu wa namna ya kuelekeza mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi nyingine za Serikali juu ya namna ya kuwekeza kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Mwongozo huo ndio unaotoa kanuni hiyo na kabla ya uwekezaji, hufanyika tathmini ya miradi na maandiko ya mradi na baadaye kwenda katika hatua za kupitishwa. Kupitisha miradi hii inahitaji pia idhini ya BoT,” amesema.
Kuhusu suala la marejesho ya uwekezaji, Katambi amesema kuna maeneo yanayolenga kutoa huduma na kuleta nafuu kwa wananchi.
Ametoa mfano Daraja la Kigamboni la jijini Dar es Salaam ambalo kama wangekuwa wamelenga katika kupata faida wananchi wangepata changamoto na adha kuliko lengo la Serikali kuhakikisha kuna huduma za kijamii.
Amesema pia sheria inawaelekeza kufanya tathmini kila baada ya miaka mitatu ambayo inawawezesha kujua mwongozo au changamoto zinazoweza kujitokeza katika miradi.
Katambi amesema Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) inasema malipo kwa wastaafu yatalipwa ndani ya siku 60 na kwamba wameshaanza kulipa chini ya siku 10 kupitia mifumo ya Tehama.
Kwa upande wa ucheleweshaji wa mafao, Katambi amesema changamoto za ucheleweshaji wa malipo ya wastaafu hazipo tena na kuwa fedha zinazotumika kuwekeza kwenye miradi sio sehemu ya fedha zinaenda kuwalipa wastaafu.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile amehoji ni lini NSSF itakamilisha makusanyo ya deni la ujenzi wa Daraja la Nyerere Kigamboni na kulikabidhi Serikalini.
Akijibu swali hilo, Katambi amesema NSSF ulianza rasmi uendeshaji wa Daraja la Nyerere Kigamboni Mei 2016 ambapo hadi kufikia Julai 2024 sawa na miaka tisa ya uendeshaji, jumla ya Sh102.18 bilioni zimekusanywa kutokana na tozo mbalimbali.
Amesema kwa mujibu wa taarifa ya upembuzi yakinifu wa mradi wakati wa kuanzishwa kwake, mradi utarejesha fedha za mfuko kiasi cha Sh344 bilioni hadi kukamilika kwake kwa kipindi cha miaka 30.
Katambi amesema fedha hizi ni gharama za uwekezaji pamoja na ulinzi na thamani ya fedha iliyowekezwa.
Amesema hivyo baada ya fedha hizo kurejeshwa mradi utakabidhiwa Serikalini.