SASA ENDELEA…
JINA langu naitwa Enjo. Ni mtoto wa tatu katika familia ya mzee Sebastian Chacha. Wa kwanza alikuwa mwanaume. Jina lake ni Raymond au Ray kama marafiki zake walivyozoea kumuita.
Yeye anafanya kazi Ujerumani. Ameshaoa na ana watoto wawili. Wa pili alikuwa mwanamke kama mimi, anaitwa Miriam. Anaishi Dar ninapoishi mimi, naye pia ameshaolewa na ana mtoto mmoja.
Wazazi wetu ni watu wa Kibaha. Baba yangu mzee Sebastian Chacha aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la kibaha kabla ya kufariki kwake.
Mzee Chacha alifariki dunia miaka michache iliyopita kwa ajali ya gari. Miaka miwili baadaye mama yetu naye alifariki.
Sasa nataka kuwapa kisa cha mimi kufahamiana na Eddie. Nilianza kufahamiana na Eddie kupitia mtandao wa Facebook. Eddie ndiye aliyetangulia kuona picha yangu na kuniomba urafiki. Kabla ya kumkubalia urafiki nilianza kupekua karasa zake.
Picha aliyokuwa ameiweka mbele ilimuonesha alikuwa kijana mtanashati aliyekuwa amevaa miwani ya bei ghali akiwa na pozi la Kizanzibari.
Picha mbali mbali alizokuwa ameweka zilimuonesha akiwa mrefu wa wastani na akiwa kwenye majengo ya kifahari. Alijitambulisha alikuwa mwanafunzi aliyekuwa anasoma huko Ujerumani lakini mzaliwa wa visiwa vya Zanzibar.
Nilipomkubalia urafiki mara moja nikaanza kuchati naye. Alinifahamisha kwamba alikuwa mzanzibar aliyekuwa anasoma huko Ujerumani na alipenda kuwa na mahusiano na mimi.
Alinitambulisha jina lake kamili alikuwa anaitwa Mohamed Salim El Shiraz. Wazazi wake walikuwa wanaishi Unguja.
Nilipomuuliza kwanini anaitwa Eddie wakati jina lake ni Mohamed. Akanijibu kuwa Eddie lilikuwa kifupi cha Mohamed.
Ingawa hatukuwahi kukutana lakini kusema kweli nilimpenda na aliponiambia atakaporudi Tanzania na kuanza kazi Mungu akipenda nitakuwa mchumba wake nilimkubalia.
Wakati huo nilikuwa nimemaliza masomo ya chuo kikuu. Wakati nahangaika kutafuta kazi nilikutana na bosi mmoja wa wizara ya Afya. Alikuwa anaitwa Frank Mchome. Nilijuana naye kwa sababu alikuwa rafiki wa baba yangu na alishawahi kuja nyumbani mara kadhaa ingawa baada ya baba kufariki dunia sikumuona tena.
Katika mazungumzo yetu aliniuliza kamanilishamaliza masomo. Nikamwambia nilimaliza tangu mwaka uliopita lakini sijabahatika kupata kazi.
“Usijali. Una sifa zote za kupata kazi, sifa ya muonekano wako na sifa ya elimu yako. Nitakufanyia mpango wa kazi.” Akaniambia. Nikafurahi sana.
“Kwa hiyo nikutegemee?” Nikamuuliza.
“Nitegemee kwa sababu nimekueleza kitu kilicho ndani ya uwezo wangu. Hebu nipe namba yako ya simu.”
Nikampa namba yangu nay eye akanipa namba yake.
“Nitakupigia kukufahamisha mipango yangu ikikamilika.”
Kwa vile suala la kazi nilikuwa na shauku nalo nikamuuliza.
“Inaweza kuchukua muda gani?”
“Nitakufanyia bidii. Haitachukua hata miezi miwili.”
“Nitakushukuru sana kaka. Nifanyie bidii. Hivi sasa nipo nipo tu, sina la kufanya.”
“Usijali. Mambo yatakuwa mazuri.”
“Sawa.”
Maneno ya Mchome yalinipa matumaini makubwa. Niliporudi nyumbani nikamueleza dada yangu Miriam.
“Nilikutana na Frank Mchome kama unamkumbuka.”
“Frank Mchome ni nani?”
“Yule kijana aliyekuwa rafiki yake baba. Alikuwa akija hapa nyumbani mara kwa mara.”
“Ohoo Frank Mchome, nimemkumbuka. Amekueleza nini?”
“Nilizungumza naye kuhusu mpango wa kazi.”
“Wapi?”
“Wizarani anakofanya yeye.”
“Kwani Yule yuko wizara gani?”
“Yuko wizara ya Afya.”
“Amekwambia atakufanyia mpango wa kazi.”
“Ameniambia atanifanyia mpango wa kazi.”
“Hapo hapo wizarani?”
“Hapo hapo ila ameniambia nimsubirie kidogo.”
“Akikupatia kazi litakuwa jambo la maana sana.”
“Amechukua namba yangu na yyeye amenipa namba yake.”
“Basi utakuwa unampigia mara kwa mara kumkumbusha.”
“Nitakuwa nampigia.”
Wiki mbili zikapita bila kupata mawasiliano yoyote kutoka kwa Frank. Ilipoingia wiki ya tatu Miriam alinuliza.
“Yule kaka hajakupigia simu?”
“Hajanipigia bado.”
“Na wewe hujampigia?”
“Sijampigia. Naona kama nitakuwa namghasi.”
“Unajua mdogo wangu mwenye shida ni wewe si yeye halafu alikuahidi yeye mwenyewe, ulitakiwa umuulize kumkumbusha.”
“Ngoja nimpigie sasa hivi.”
“Mpigie.”
Nikachukua simu yangu na kumpigia nikijifanya kama namsalimia.
“Enjo hujambo.” Akanisalimia mara tu alipopokea simu yangu.
“Sijambo. Habari za mawiki?”
“Nzuri Enjo. Nilikuwa bize, sikuwahi hata kukupigia.”
“Ndiyo nikasema leo nimsalimie kaka yangu. Tumekuwa kimya muda mrefu.”
“Nashukuru. Kuna kitu nilikuwa nataka kukufahamisha. Unajua wii ijayo naanza likizo. Ule mpango niliokuahidi nilishaanza kuushughulikia, sasa kwa vile nakwenda likizo itabidi nisimame kwanza mpaka nitakaporudi.”
“Unaanza likizo lini?”
“Wiki ijayo.”
“Hakuna tatizo, nitasubiri. Waswahili wanasema subira huvuta heri.”
“Ni kweli. Wewe endelea kusubiri na endelea kunitegemea. Mambo yatakuwa mazuri tu. Usijali.”
“Nashukuru kaka yangu. Mimi bado nakutegemea.”
“Sawa. Tutawasiliana.”
“Sawa kaka.”
Nikakata simu.
“Amekwambiaje?” Dada akaniuliza.
“Ameniambia anaanza likizo wiki ijayo. Kwa hiyo huo mpango utakuwa baada ya kurudi likizo.”
“Sasa kama usingempigia angekwambia lini?”
Hapo sikuwa na jibu la kumjibu dada.
“Angekwenda likizo na wewe ungeona kimya tu. Ndiyo maana nikakwambia wewe ndiye mwenye shida mpigie mara kwa mara kumuulizia.” Dada akaniambia.
“Sasa itabidi nisubiri mpaka atakaporudi likizo.”
Nikaendelea kusubiri kwa karibu wiki sita, yaani mwezi mmoja na nusu. Siku hiyo nilikuwa chumbani nikichati na Eddie majira ya saa nne asubuhi, Frank akanipigia simu. Nilipoona jina lake nikapokea simu haraka.
“Hello…”
“Hello Enjo. Habari yako?”
“Nzuri kaka. Upo mzima.”
“Nashukuru Mungu, sijui wewe.”
“Mimi ni mzima tu, naendelea vizuri. Bado uko likizo au umesharudi?”
“Nilisharudi tangu wiki iliyopita. Hapa niko ofisini kwangu.”
“Hawajambo uliokwenda kuwasalimia?”
“Nilipoondoka hawajambo. Sijui nilipowaacha.”
“Mungu ni mwema watakuwa hawajambo tu.
“Tunaweza kukutana leo?”
“Muda gani?”
“Majira ya saa saba hivi.”
“Tunaweza. Nikufuate wapi?”
“Unapafahamu pale Shash Mahal?”
“Sipafahamu. Hebu nitambulishe ni wapi?”
Frank akanielekeza hadi nikapafahamu. Ulikuwa ni mgahawa uliokuwa jirani na posta kuu.
“Nimeshapafahamu.” Nikamwambia.
“Sasa tukutane hapo saa saba mchana.”
“Nitakukuta hapo au utanikuta hapo?”
“Vyovyote itakavyokuwa lakini natumaini utanikuta hapo.”
“Sawa. Nitafika.”
“Sawa.”
Frank akakata simu.
Alitaka tukutane Shash Mahal kwa niaba gani? Nikajiuliza. Nikafikiria kwamba mwenye shida ni mimi, sikupaswa kuuliza maswali mengi. Ilikuwa saa nne na nilihitajika nikutane naye saa saba. Nilikuwa nina masaa matatu ya kujiandaa.
Nilitoka chumbani nikaenda sebuleni ambako dada yangu alikuwa amekaa akitazama televisheni.
“Frank amenipigia sasa hivi.” Nikamwambia kwa kumshitua.
“Amekwambia nini?”
“Nikutane naye Shash Mahal saa saba mchana.”
“Kwa ajili ya huo mpango?”
“Nafikirini kwa ajili hiyo.”
“Alisharudi likizo?”
“Alisharudi.”
“Haya nenda kamsikilize. Ulimpigia wewe au amekupigiayeye?”
2
“Amenipigia yeye mwenyewe.”
“Nenda kamsikilize. Labda amefanikisha.”
Saa saba kasoro dakika tano pikipiki ya bodaboda ikanishusha mbele ya mkahawa wa Shash Mahal. Nikamlipa mwenye bodaboda kisha nikayatupa macho yangu mbele ya mlango wa mkahawa huo.
Wakati nainua hatua kuelekea kwenye mkahawa huo nikasikia sauti ya kume ikiita jina langu kutoka upande uliokuwa umeegeshwa magari mbele ya mkahawa huo.
Nikageuza kichwa change kutazama nyuma. Nikaona gari moja limefunguliwa mlango na mtu akishuka. Nilipomtazama vizuri mara moja nikagundua alikuwa Frank.
Kumbe alipofika na gari lake hakushuka kwenye gari. Alisubiri garini ili nitakapofika aweze kuniona.
“Enjo niko hapa. Nilikuwa nakusubiri wewe. Kama ningetangulia kuingia ningekusumbua.” Akaniambia huku akinifuata.
“Na nilikuwa nataka kuingia.’
“Sasa tuingie pamoja.”
Tukaingia pamoja na kwenda kukaa kwenye meza iliyokuwa tupu. Tulipokaa tu mhudumu akatuletea menyu.
“Acha tule huku tukizungumza.”
Frank akaagiza ugali kwa kuku. Menyu ilipofika kwangu nikachagua pilau ya kuku na bilauli ya juisi.
“Natoka kazini.” Frank akaniambia mara tu mhudumu alipoondoka. Akaongeza.
“Nimeona muda huu wa kuja kula ndio niutumie kwa mazungumzo na wewe. Nimerudi likizo nimekuta kazi nyingi zilikuwa zinanisubiri. Hapa nikitoka kazini ni jioni kabisa.”