Siri ya uwezo wa Chama, Pacome mtaalamu wao afunguka

SIRI ya viungo wawili Yanga ambao ni Pacome Zouzoua na Clatous Chama imefichuka, baada ya kuonekana kuwa na viwango bora hasa katika michuano ya kimataifa iliyochezwa wikiendi iliyopita dhidi ya Vital’o ya Burundi. 

Huu ni msimu wa pili kwa Muivory Coast Pacome aliyetokea Asec Mimosas na wa kwanza kwa Chama ambaye alikuwa akiichezea Simba.

Viungo hao wamekuwa na balaa hasa katika mechi ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital’o, huku wakikisaidia kikosi chao kufuzu na wao kuweka rekodi kibabe.

Chama ambaye alianza kikosi cha kwanza katika mechi hizo alitoka na rekodi ya kufunga mabao mawili na kutoa asisti nne katika mabao 10 iliyofunga Yanga, hivyo ameshiriki kwenye mabao sita.

Kwa upande wa Pacome licha ya kuathiriwa na majeraha yaliyomfanya kushindwa kucheza robo fainali ya michuano hiyo msimu uliopita, lakini sasa anaonekana kuwa imara katika mechi mbili na amefunga bao moja.

Unaambiwa viungo hao kipindi cha hivi karibuni wamekuwa na mazoezi binafsi ambayo huyafanya nje ya yale ya kikosini pamoja na wachezaji wenzao, ndiyo maana moto wao umekuwa mkali zaidi.

Awali, Chama hakuwa na kasi jambo ambalo limeanza kuwa historia kwani sasa ana mbio za kutosha uwanjani, jambo linalomfanya kuwa katika nafasi ya kupata mpira kwa haraka na hata kufunga.

Kwa upande wa Pacome ameonekana kuwa imara hasa katika mechi za hivi karibuni, kwani hata mpinzani amkabe na kumsukuma kiasi gani lakini mpira hauchomoki miguuni.

Mwanaspoti lilipofuatilia siri nyuma ya viungo hao limegundua mambo kadhaa na hasa lilipotia timu kwa mkufunzi wao mpya anayejulikana kwa jina la Denzel Trainer, aliyefunguka maujuzi aliyowaongezea mastaa hao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Godfrey Mkinga ‘Denzel Trainer’ alisema Chama alianza kumuongezea ufiti tangu alipokuwa Simba kabla hajahamia Yanga na wapo mastaa wengine anaowapa maujuzi nje ya wawili hao.

Denzel alisema kabla hajaanza mazoezi na mchezaji hujipa muda wa kukaa na kuangalia mechi alizocheza ili aweze kufahamu changamoto ya ufiti aliyonayo.

“Nilipoanza na Pacome niligundua kuwa ana changamoto kidogo kwenye utimamu wa mwili (fitness) jambo ambalo linaweza kumfanya mchezaji kuanguka kwa haraka, ingawa ni mchezaji mwenye mbio, nguvu na akili ya kufunga.

“Lakini kwa Chama niliona changamoto ya mikimbio (speed) haikuwa vizuri licha ya kuwa ana akili kubwa ya kufunga na nguvu. Hapo ndipo nilipoanza kuwafundisha kwani nilijua changamoto zao,” alisema.

Aliongeza kuwa, “huwa naongea nao kabla ya mechi na kuwaambia kuwa nataka mabao au asisti, kwani naamini ni wachezaji bora na wana uwezo huo na ndio maana wanafunga kama mnavyoona.”

Yanga haijacheza mchezo hata mmoja wa ligi, huku rekodi zikionyesha kuwa msimu uliopita Chama alimaliza akiwa na mabao saba (Simba) na Pacome 11.

Huenda nyota hao wakawa viungo hatari ndani ya klabu hiyo kama wataendeleza rekodi ya kufunga mara kwa mara kama walivyofanya katika mechi zilizopita.

USIKOSE MAKALA MAALUMU YA MASTAA HAO MIKONONI MWA DENZEL TRAINER.

Related Posts