Dodoma. Wabunge wa Tanzania wameibana Serikali bungeni kuhusu masuala ya ajira huku Serikali ikisema baadhi ya nafasi za ajira katika kada ya afya zimekosa waombaji hususan katika mikoa mitatu iliyoko pembezoni ya Mtwara, Lindi na Kigoma.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Agosti 27, 2024 na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka.
Akiuliza swali hilo, Kuchauka amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya waajiriwa wapya kuhama kwenye halmashauri za pembezoni.
Amehoji nini kauli ya Serikali kwa watumishi hao wanaoajiriwa lakini wanahama katika maeneo walioajiriwa baada ya miaka mitatu.
Akijibu swali hilo, Sangu amesema Serikali imeweka utaratibu mzuri wa mtu anapoajiriwa anapaswa kukaa katika kituo cha kazi kwa miaka isiyopungua mitatu.
“Tumeanzisha mfumo ambapo waajiri wanaomba uhamisho unaitwa E- Uhamisho. Hata hivyo ajira hizi tulizotangaza zimetangazwa kimkoa. Baadhi ya kada za afya hasa katika mikoa ya pembezoni zimekosa waombaji. Nafasi ni nyingi lakini wanaomba ni wachache,” amesema.
Ametaja mikoa hiyo ambayo imekosa waombaji ni Mtwara, Kigoma na Lindi.
Sangu ametoa rai kwa waombaji wa ajira wasikimbilie kuomba nafasi za mijini tu, bali waombe hata kwenye mikoa ya pembezoni kwa sababu Serikali imeweka vizuri miundombinu ya huduma za kijamii.
Naye, Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara amehoji kama Serikali iko tayari kutoa hadharani vigezo vya ajira ili kuondoa usumbufu wa vijana wanaoomba ajira kusumbua wabunge.
Amesema vijana hao wanadhani kuwa ukituma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwa wabunge watawasaidia kuwaombea ajira.
Waitara amesema hilo litawafanya vijana wajue ajira inatolewa kwa haki na atakayekuwa na sifa ndiye atakayepata.
Akijibu swali hilo, Sangu amesema kupitia Sektarieti ya Ajira, vigezo vyote viko wazi,namna ambavyo wanafanya usahili na matokeo yanatoka wazi, hata kwa wale wanaokosa hupewa sababu.
“Lakini tumetoa fursa yule ambaye anadhani hakutendewa haki kukata rufaa, kwa hiyo kila Mtanzania yuko wazi kuomba kazi,” amesema.
Mbunge wa Vunjo (CCM), Dk Charles Kimei amehoji Serikali inachukua hatua gani kuunda kanzidata ya vijana wanaojitolea katika maeneo mbalimbali.
Akijibu swali hilo, Sangu amesema wamechukua kanzidata ya vijana wanaojitolea na kuwa hawataingia katika ajira moja kwa moja bali nao watashindana kwenye nafasi za ajira.
“Lakini mwishoni yule aliyejitolea atakuwa na nyongeza ya faida. Serikali inaandaa mfumo mzuri ambao tutawabaini, namna ya kuwapata hawa wanaojitolea na namna ya kuwapatia stahiki ili waweze kuongeza molari ya kujitolea,” amesema.
Amesema Serikali imeshauandaa utaratibu mzuri na hivi karibuni watauwasilisha.
Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM) Ezra Chiwelesa amesema kumekuwa na utaratibu wa nafasi za majeshi ambapo watoto wanapatikana katika majimbo yao, lakini baada ya kufika mkoani wanawarudisha kwa madai kuwa wanakovu na mengine.
“Kumekuwa na vigezo vingi watu wa mkoa wanadhulumu watu wa wilayani. Tunaomba nafasi zipelekwe wilayani hasa zile zinazohitaji watu wa form four (kidato cha nne) wakitoka wilayani waende moja kwa moja kwa sababu watu wa mkoani wanakuwa na nafasi za kuchomeka watu wao, watu wanaotoka katika wilaya wanaachwa,” amesema.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Nachingwea (CCM), Anandus Chinguile amehoji iwapo Serikali haioni haja ya kuanzisha mfumo utakaowezesha kupata idadi sawa ya nafasi za ajira katika kila jimbo kuliko mfumo wa sasa.
Akijibu swali hilo, Sangu amesema kwa Mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2008, Toleo la 2 Aya ya 4.2, nafasi za Ajira hutolewa kwa ushindani na kwa kuzingatia sifa stahiki kwa mujibu wa miundo ya maendeleo ya utumishi ya kada husika.
Amesema pia nafasi wazi za ajira hutolewa kwa kuzingatia ikama ya watumishi katika taasisi husika ambayo inajumuisha mahitaji halisi yaliyopo katika taasisi husika.
“Kwa mujibu wa hati idhini inayoanzisha kila taasisi, mahitaji ya watumishi ya taasisi moja hutofautiana na ya taasisi nyingine kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukubwa wa taasisi na wingi wa majukumu,” amesema.
Aidha, amesema idadi ya taasisi za umma zinatofautiana kwa kila jimbo na kuwa idadi ya nafasi za ajira hutofautiana kati ya Jimbo moja na jingine.
Amesema kutokana na maelezo hayo, katika mwaka 2023/2024, Serikali imetoa kibali cha nafasi 47,404 za ajira mpya kwa waajiri wote ambapo kila mwajiri katika kila jimbo amepata nafasi kwa kuzingatia ikama ya watumishi katika maeneo hayo.
Aidha, amesema katika kutekeleza kibali hicho, Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi katika kada za elimu na afya, kimkoa na usaili utafanyika katika ngazi ya mkoa.