Dar es Salaam. Umajumui wa Afrika, uzalendo na uzoefu ndizo sababu zilizotajwa na baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki kama turufu kwa Raila Odinga katika nafasi ya Uenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).
Viongozi hao katika hotuba zao, wamemwelezea Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya, ndiye anayestahili kuwa kiongozi wa jumuiya hiyo inayobeba sauti ya pamoja ya Afrika.
Odinga anagombea nafasi hiyo, kumrithi Moussa Faki Mohamed, Waziri Mkuu wa zamani wa Chad anayetarajia kumaliza muhula wake wa pili wa uenyekiti wa AU mapema mwakani.
Hii ni mara ya pili Kenya inatupa karata yake katika kuwania nafasi hiyo, ilifanya hivyo mwaka 2017 alipogombea Amina Mohammed lakini hakufanikiwa.
Katika uchaguzi wa nafasi hiyo, wakuu wa nchi za Afrika, hupiga kura kwa siri na inahitaji kupata angalau theluthi mbili ya 36 ili utangazwe kuwa mshindi.
Marais waliomwaga sifa hizo kwa Odinga ni Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Yoweri Museveni wa Uganda, Salva Kiir wa Sudani Kusini na William Ruto wa Kenya.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni za nafasi hiyo ya Odinga leo Jumanne, Agosti 27, 2024 Ikulu ya Nairobi Kenya, Rais Museven amesema jumuiya ya AU ndilo jukwaa linaloiwezesha Afrika kuwa na sauti ya pamoja katika majadiliano na ulimwengu.
Kwa sababu hiyo, amesema Odinga ni mgombea sahihi kwa nafasi hiyo kwa kuwa mara nyingi amekuwa akisisitiza umajumui wa Afrika.
“Kwa sasa tunataka mtu atakayetuongoza kutupeleka kwenye ustawi na siyo yule ambaye anatafuta kazi tu. Kwa hiyo Odinga ni mgombea sahihi kwenye nafasi hii,” amesema.
Ameijenga hoja yake hiyo kwa kurejea uhalisia wa hali ya nchi za Afrika, akisema ugonjwa mkubwa unaozikabili ni umasikini na kukosa ustawi.
Lakini ustawi wa mataifa hayo, amesema utafikiwa iwapo nchi hizo zitakoma kutegemea misaada na badala yake kila raia, wakiwamo wazee wajishughulishe na shughuli za uzalishaji.
“Kama utazalisha bidhaa na huduma na ukawa na hesabu nzuri utapata fedha na kuuepuka umasikini. Kwa hiyo hiki ndicho kipimo chetu,” amesema.
Museveni amesema kitakachozalishwa kitauzwa katika mataifa ya ndani ya Afrika aliyodai yanaendekeza ukabila na udini, bila kuzalisha.
“Kuna ambaye hana kile unachozalisha na huyo ndiye utakayemuuzia ndani ya Afrika, kwa hiyo sisi wenyewe tunaweza kuzalisha na kuuza ndani,” ameeleza.
Kwa mujibu wa Museveni, siri nyingine ya mafanikio ya mataifa ya Afrika ipo katika uzalendo, akifafanua kwa namna yoyote nchi zinahitajiana.
“Unaponunua bidhaa zetu unatupa nafasi ya kwenda juu, lakini ukitufungia, najua kuna watu wamefungia kununua sukari tafadhali fungua sukari hiyo,” ameeleza huku akiangua kicheko.
Amesema inapotokea mataifa ya Afrika yanafungiana kuuziana bidhaa, yanaukaribisha umasikini.
Amesisitiza namna pekee ya kuuondoa umasikini kwa nchi za bara hilo ni kudumisha uzalendo ndani ya nchi, kadhalika umajumui wa Afrika kwa ujumla.
“Kwa hiyo uongozi unapaswa uwe moja ya jawabu la uchumi katika jamii zetu. Uongozi uchambue jamii zinakosa nini na uhakikishe unazipatia,” ameeleza.
Katika mazingira hayo, amesema Odinga ndiye mtu sahihi katika nafasi ya uenyekiti wa kamisheni ya AU, kwa kuwa historia yake inaashiria uwezo wa utendaji wenye manufaa kwa waafrika.
Katika hotuba yake, Rais Samia amesema licha ya hatua zilizopigwa ni muhimu kwa nchi za Afrika kuhakikisha AU inaendelea kuwa imara ili kukabili changamoto za ulimwengu.
Katika kulitekeleza hilo, amesema kunahitajika mambo mengi ikiwamo mageuzi ya kitaasisi ili kuimarisha uwajibikaji na kudumisha amani ili kukomesha vita katika mataifa ya bara hilo.
Sambamba na hayo, ameeleza ili AU ifikie ajenda ya maendeleo inahitaji kuangalia mipango ya miundombinu yake na kuhakikisha sauti ya Afrika inasikika katika mijadala ya kidunia.
Katika kuzingatia umuhimu wa yote hayo, amesema Tanzania imeamua kumuunga mkono Raila Odinga katika nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).
“Tanzania inamjua Odinga kama mwanamajumui wa Afrika. Amelinda uhusiano wa viongozi wengi wa Afrika na hata wadau wengine nje ya bara hili,” ameeleza.
Amesema ni vyema kwa uzoefu wake kutumikia nafasi hiyo itakayowezesha kuleta maendeleo ya miundombinu na kutatua changamoto nyingine.
Amesema ni imani yake kuwa, Ondinga ndiye msingi wa mageuzi ya Afrika na watu wake.
Kwa upande wa Rais wa Sudan Kusini na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Mashariki (EAU), Salva Kiir amesema ushiriki wake katika uzinduzi wa kampeni hizo unatoa ishara ya taifa lake kumuunga mkono Odinga.
Rais Ruto wa Kenya, amesema hatua yake ya kumuunga mkono Odinga katika nafasi mbalimbali haikuanza sasa, amekuwa akifanya hivyo tangu zamani na imempitisha katika madhira mbalimbali.
“Nimewahi kushitakiwa katika mahakama mbalimbali za kimataifa kwa sababu ya kumshabikia Odinga kwa hiyo nimekuwa shabiki wake wa muda mrefu,” amesema.
Amesema Odinga ni mtu sahihi katika kuiongoza AU, ni mwana demokrasia na Kenya imenufaika na mchango wake kwenye mabadiliko ya Taifa hilo na ana uzoefu wa kutosha kutumikia nafasi hiyo.