Wanafunzi waliofariki dunia Wakiogelea, kuzikwa kesho

Rorya. Watoto wanne kati ya sita waliofariki dunia baada ya kuzama na kunasa kwenye tope katika bwawa la skimu ya kilimo cha umwagiliaji katika kijiji cha Ochuna, Wilaya ya Rorya mkoani Mara wanatarajiwa kuzikwa kesho Agosti 28, 2024 katika eneo la pamoja.

Watoto hao, wote wakiwa ni wa kike, wanafunzi wa Shule ya Msingi Ochuna, walifariki dunia Agosti 24, 2024 jioni baada ya kuzama na kunasa kwenye tope katika bwawa hilo walipokuwa wakiogelea.

Akizungumza na Mwananchi leo Agosti 27, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka amesema maandalizi ya mazishi yanaendelea ambapo pamoja na mambo mengine Mbunge wa Rorya, Jaffari Chege ametoa majeneza sita kwa ajili ya tukio hilo.

“Kama mnavyojua, watoto watatu ni wajukuu wa bibi mmoja kwa maana kwamba wawili ni wa binti yake na mmoja ni wa kijana wake, kwa hiyo hawa wawili wa binti, yaani wa mama mmoja, wao wanakwenda kuzikwa kwao katika kijiji cha Kamageta kwa sababu huku walikuwa wakiishi na kusoma kwa bibi yao na wanne wanaobakia watazikwa katika eneo la pamoja hapohapo kijijini Ochuna,” amefafanua Chikoka.

Amesema ofisi yake inaangalia namna ya kuwezesha shughuli hiyo ya maziko kufanyika huku akiongeza kuwa taarifa za awali zinaonyesha kuwa shughuli hiyo itahudhuriwa na watu zaidi ya 2,000.

Amesema hivi sasa wanajipanga kuangalia namna gani halmashauri ya wilaya ya Rorya itafanikisha shughuli hiyo bila kuathiri bajeti za familia husika.

“Awali, uongozi wa kijiji ulipendekeza watoto wazikwe katika eneo la shule na baada ya majadiliano, tumewaagiza watafute eneo lingine na nimeambiwa tayari limepatikana hapohapo kijijini.

“Pia, muda si mrefu naingia kwenye kikao na watu wangu tuone tunalifanikishaje hili jambo kwani tusingependa kuingilia familia kwenye matumizi yao hasa kwenye zile fedha za rambirambi alizotoa Rais,” ameongeza Chikoka.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ochuna, Erick Nyagandi amesema tayari eneo la pamoja litakalotumika kwa ajili ya maziko limepatikana baada ya mkazi mmoja wa kijiji hicho kujitolea.

“Kuna mzazi mmoja wapo ambaye mwanaye ni miongoni mwa waliofariki ametoa eneo kwa ajili ya maziko na tunatarajia kuwapumzisha watoto wetu kesho,” amesema.

Nyagandi amesema uongozi wa kijiji ulitoa pendekezo la watoto hao kuzikwa katika eneo moja ili iwe rahisi kwa wanakijiji wote kupata fursa ya kushiriki tofauti na ambavyo kila familia ingefanya shughuli hiyo kivyake, jambo ambalo lingewapa wakati mgumu wanakijiji kushiriki hasa ikizingatiwa familia zilizopata msiba zinaishi jirani.

“Tunaushukuru uongozi wa wilaya kupokea wazo letu na kuamua kusimamia jambo hili, pia, tunazishukuru familia kukubaliana na wazo hili, kwa sasa tunaandaa ratiba ya shughuli nzima kisha itatolewa kwa wananchi ili washiriki,” ameongeza.

Watoto hao waliofariki ni pamoja na Suzana Mwita na Unice Okumbe, wanafunzi wa darasa la tatu, Elizabeth Okumbe na Pendo Nyasanda (darasa la nne), Anjelina Suke wa darasa la tano na  Evaline Sylvanus aliyekuwa darasa la sita.

Kufuatia tukio hilo, Rais Samia Suluhu Hassan alituma salamu za rambirambi na kutoa mkono wa pole wa Sh30 milioni kwa familia zilizopata msiba huo.

Related Posts