Geita. Washtakiwa watatu kati ya wanne walioshtakiwa kwa kosa la mauaji ya Milembe Suleiman (43) wametiwa hatiani na kuhukumuiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Mahakama imetoa adhabu hiyo baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri, kuwa umethibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka.
Hukumu hiyo imetolewa leo Agosti 21, 2024 kuanzia saa 3.02 asubuhi hadi saa 5.12 asubuhi na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Kelvin Mhina.
Jaji Mhina aliyesikiliza kesi hiyo amesema kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri, Mahakama imewatia hatiani washtakiwa wa kwanza hadi wa tatu, na kumuachia huru wa nne, Musa Lubingo.
Waliotiwa hatiani katika kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023 ni mshtakiwa wa kwanza, Dayfath Maunga (30), wa pili Safari Lubingo (54) na wa tatu, Genja Pastory.
Jaji Mhina amesema mambo muhimu ya kuzingatia ni kama kweli Milembe, aliyekuwa mfanyakazi wa mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), alifariki dunia, kifo kilikuwa cha kawaida au la, kama walioshtakiwa ndio waliohusika, na kama mauji hayo yalikuwa ya kukusudia au la.
Amesema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani, hakuna ubishani kuwa Milembe alifariki dunia na mwili wake ukakutwa na majeraha kama ilivyothibitishwa na shahidi wa sita wa upande wa Jamhuri, daktari aliyeufanyia mwili huo uchunguzi.
Mbali ya daktari aliyethibitisha kwa kutoa hati ya uchunguzi wa mwili, amesema shahidi wa nne wa upande wa Jamhuri aliyekuwa mwenyekiti wa mtaa wa Mwatulole, alithibitisha kuukuta mwili kwenye nyumba zilizokuwa zinajengwa, hivyo hakuna shaka kuwa Milembe alifariki dunia.
Kuhusu kifo kisicho cha kawaida, Jaji Mhina amesema taarifa ya daktari inaeleza kuhusu majeraha yenye ukubwa wa sentimita 14, nane na sita aliyoyapata kichwani, shingoni na mkononi, hivyo inaonyesha alifikwa na mauti kwa njia ya kikatili.
Amesema kwa mujibu wa ushahidi, kifo cha Milembe hakikuwa cha kawaida.
Jaji Mhina amesema kuhusu nani alimuua, ushahidi upo kwenye vinasaba, ripoti ya uchunguzi, picha za CCTV na maelezo ya washtakiwa.
Amesema ushahidi wa DNA wa damu uliochukuliwa kwenye jambia lililotumika kumuua Milembe, matokeo yanaonyesha ni ya mwanamke, huku sampuli za mate na damu ziliyochukuliwa kwenye mpini wa jambia vilikuwa ya mtu mmoja mwanaume ambaye ni mshtakiwa watatu (Pastory).
Jaji Mhina amesema ushahidi wa shahidi wa 22 na wa 28 unaongeza uzito wa ushahidi wa DNA, pale mshtakiwa wa tatu alivyopelekwa Geita na kuonyesha jambia lililotumika kumuua na simu za marehemu.
Amesema ushahidi wa shahidi wa tano kuhusu alama za vidole zilizokutwa kwenye chupa zilibainika kuwa za mshtakiwa wa tatu, na kwa mujibu wa wataalamu hakuna alama za vidole zinazofanana na za mwingine.
Amesema katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu (Pastory) alikiri na kueleza namna alivyotupa silaha na simu za marehemu na kwambaMei 6, 2023 aliwaongoza askari kwenda kuwaonyesha maeneo alikotupa jambia na simu.
Jaji Mhina amesema kwa mujibu wa DNA ya alama za vidole na kitendo cha yeye kuwapeleka askari eneo alikotupa simu na jambia, vinaunga mkono maelezo ya onyo aliyoyatoa licha ya kuwa akiwa mahakamani aliyakataa maelezo hayo.
Amesema katika ushahidi uliotolewa kwenye maelezo ya onyo, mshtakiwa amekiri kuwa yeye ndiye alimkata Milembe kichwani na ushahidi wake unaunga mkono ushahidi uliotolewa.
Kuhusu mshtakiwa wa kwanza (Dayfath), shahidi wa 11 ambaye ndiye aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo, alikiri kupanga kutafuta wauaji na kuishi na Milembe kama mume na mke, pia alieleza alikuwa akinyanyaswa na alitaka kuondoka lakini ilishindikana.
Katika ushahidi huo, amesema unaeleza namna alimtafuta mshtakiwa wa pili (Lubingo) aliyewatafuta washtakiwa wengine, akiwemo Patory na kuwalipa Sh2.6 milioni.
Amesema pamoja na mshtakiwa kudai hakuandika maelezo, ushahidi huo unaangalia kama kuna mwingine wa kuunga mkono maelezo yaliyokataliwa na kuwa ushahidi wa mazingira unaongeza nguvu kwenye mwingine wa maelezo ya onyo.
“Mshtakiwa alikamatwa Mei mosi na yeye ndiye aliyemtaja mshtakiwa wa pili na kueleza anakoishi, na shahidi wa 24 ameeleza alivyomkamata shahidi wa pili, na bila mshtakiwa wa kwanza kutoa taarifa mshtakiwa wa pili, wa tatu na wa nne wasingekamatwa kwa mazingira hayo, ushahidi unaunga ushahidi wa mshtakiwa wa kwanza na wa pili,” amesema.
Jaji amesema licha ya kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha washtakiwa kutenda kosa hilo au kuwa eneo la tukio, lakini mshtakiwa wa kwanza na wa pili ndio walipanga mauaji, na mshtakiwa wa kwanza ndiye aliyelipa wauaji.
Amesema kwa mujibu wa sheria anayesaidia au kutafuta muuaji anakuwa na hatia ya kusababisha kifo.
Kuhusu mshtakiwa wa nne jaji amesema kwa mujibu wa shahidi wa nane wa upande wa Jamhuri, alijitoa kwenye hatua za awali na hakuhusika tena na mauji hayo.
Kutokana na ushahidi huo, Jaji Mhina amesema upande wa mashtaka umethibitisha kosa kwa mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu kuwa walitenda kosa kinyume cha vifungu vya 196 na 197 vya Sura ya 16 (Kanuni ya Adhabu) iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Awali kabla ya hukumu kutolewa, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Scolastica Teffe aliieleza Mahakama kuwa hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya washtakiwa hao.
Wakili wa utetezi, Laurent Bugoti ameiomba Mahakama kutoa hukumu kwa mujibu wa sheria kwa kuwa hakuna mbadala wa adhabu ya kesi ya mauaji.
Akitoa hukumu, Jaji Mhina amesema kwa mujibu wa sheria washtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu wanahukumiwa kunyongwa hadi kufa na kwamba, wana haki ya kukata rufaa endapo hawajaridhika na hukumu hiyo.