Mikumi. Uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi umetakiwa kuzingatia utunzaji wa uoto wa asili kutokana na mabadiliko ya mazingira ukilinganisha na hali ya zamani.
Imeelezwa kuwa hatua hiyo itasaidia kulinda mazingira, kuendeleza uchumi na kuboresha maisha ya viumbe vilivyopo ndani na nje ya hifadhi hiyo.
Wito huo umetolewa leo Jumanne Agosti 27, 2024 na Baraza la Wazee wa Mtaa wa White House, Kata ya Mafisa, mkoani Morogoro, baada ya kutembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani, kujifunza na kujionea mabadiliko ya sasa.
Mwenyekiti wa Wazee wa Mtaa wa White House, Shomari Kalipeni amesisitiza umuhimu wa utunzaji wa uoto wa asili, akieleza kuwa ni njia muhimu ya kulinda mazingira, kuimarisha uchumi na kuhakikisha ustawi wa viumbe hai wote, ikiwa ni pamoja na binadamu wanaoishi karibu na hifadhi hiyo.
“Ukiangalia mazingira yaliyopo katika hifadhi hii sasa hayafanani na hali ilivyokuwa miaka ya 90. Niwaombe wahifadhi waendelee kutunza uoto wa asili uliopo kwa manufaa ya wanyama na vizazi vijavyo. Kutunza uoto wa asili ni muhimu kwa kudumisha mazingira yenye usawa, kusaidia kupambana na changamoto za kiikolojia na kiuchumi na kuhakikisha ustawi wa viumbe vyote, ikiwemo binadamu,” amesema Kalipeni.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mafisa White house, Said Yasin ameonya juu ya athari za ukataji miti kiholela akisema unaweza kusababisha ukame na kupoteza maisha ya wanyama.
Hivyo, amesisitiza kuwa uongozi wa hifadhi unapaswa kuwachukulia hatua za kisheria wale wanaobainika kuharibu mazingira ndani ya hifadhi.
Ofisa Mwandamizi wa Utalii wa Hifadhi ya Mikumi, Herman Mtei amewapongeza wazee hao kwa hatua yao ya kutembelea hifadhi hiyo, akisema imefungua njia kwa wazee wengine nchini kutembelea vivutio vya kitalii.
Mtei amesema uongozi wa hifadhi utaendelea kuhakikisha hifadhi hiyo inatunzwa vizuri kwa faida ya wanyamapori na Taifa kwa ujumla.