Bangi gramu 4,095 yamtupa maisha jela

Arusha. Siku ya kufa nyani miti yote huteleza, hii ndio kauli unayoweza kuitumia kuelezea safari ya miaka 11 ya Mtanzania Nusura Mtinge kujinasua na kifungo cha maisha jela baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kubariki kifungo hicho.

Licha ya kulikana jina lake, lakini mahakama hiyo iliyoketi Moshi imeona adhabu ya kifungo cha maisha alichohukumiwa kwa kosa la kusafirisha gramu 4,095.1 za bangi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ilikuwa sahihi.

Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji mkuu (CJ) wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na majaji Dk Mary Levira na Zephrine Galeba walitoa hukumu hiyo Agosti 21, 2024 baada ya kusikiliza rufaa iliyowasilishwa na Nusura na kuitupilia mbali.

Nusura alikamatwa Julai 23, 2013 akiwa katika hatua za mwisho za kusafiri kwa Shirika la Ndege la Turkish Airline, ndege namba TK 673 iliyokuwa imepangiwa kuondoka saa 10:20 alfajiri kwenda Istanbul Uturuki kwa safari ya kibiashara.

Rufaa hiyo ya jinai namba 61 ya mwaka 2021, ilikuwa inapinga hukumu iliyotolewa Desemba 23, 2020 na Jaji Mohamed Gwae wa Mahakama Kuu kanda ya Moshi iliyomhukumu kifungo cha maisha jela kwa kusafirisha gramu 4,095.1 za bangi.

Siku hiyo ya Julai 23, 2013, Nusura aliyekuwa anasafiri na Shirika la Ndege la Turkish kuelekra Istanbul nchini Uturuki, alikuwa KIA tayari kwa safari hiyo na safari yake hiyo ya siku 15 ilikuwa ni ya kibiashara na ndege ilikuwa iondoke saa 10:20 alfajiri.

Nusura alikuwa amepanga kurejea nchini Agosti 3, 2013 na akiwa KIA na kama ulivyo utaratibu, alipitia mchakato wa ukaguzi na mzigo wake ulioandikwa MEIQITUN ulipopitishwa kwenye mashine (HBS), ulionekana vitu visivyoeleweka.

Shahidi wa 8 wa Jamhuri, Ahmed Mwachalula aliyekuwa katika mashine hiyo ya HBS, aliamua kuufanyia ukaguzi mzigo huo kwa kutumia mashine ya X-ray lakini bado mashine hiyo nayo ilishindwa kubaini aina ya mzigo huo uliopo kwenye begi.

Mwachalula akamjulisha askari mwanamke WP namba 2102 Sajenti Ndeshi aliyekuwa shahidi wa 7 ambaye anafanya kazi kituo cha Polisi KIA lakini wakati huohuo akatangaza kwa kipaza sauti na kumtaka mwenye mzigo huo ajitokeze.

Baada ya kujitokeza, Nusura alipojitokeza na kujitambulisha kwa WP Ndeshi na kueleza kuwa ingawa jina lililopo kwenye hati yake ya kusafiria ni Nusura Sultani Mtinge lakini kwenye tiketi limekosewa na kuandikwa Nusura Sultani Mtinde.

Alilitambua begi kuwa ni mali yake na alitakiwa aondoe vitu vyote vilivyokuwemo ambavyo vilikuwa ni chupa za maji, mbegu za mbuyu, matunda, majani ya chai na nguo mbalimbali, na liliporudishwa kwenye mashine, bado kuna vitu vilionekana.

Hapo ndipo WP Ndeshi alipomuita mkuu wa kituo (OCS) wa kituo cha KIA, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) ambaye alimtaka WP Ndeshi kulichana begi hilo, kulikutwa sabuni saba zilizokuwa katika muundo wa vipande vya matofali.

Moja kati ya vipande hivyo vilichanwa mbele ya mrufani na kukutwa majani makavu na majani hayo katika vipande hivyo saba yalipopelekwa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kupimwa katika maabara, ilibainika ni dawa aina ya bangi.

Baada ya kufikishwa kortini, mrufani alisomewa kosa la kusafirisha dawa hizo za kulevya ambapo alikana mashitaka na kueleza kuwa safari yake kwenda Istanbul haikuwa kwa ajili ya biashara bali alikuwa anakwenda kwa ajili ya matibabu.

Aliwasilisha kortini kielelezo D2 kikionyesha kwamba alikuwa anaugua uchovu usioelezeka, kubanwa kifua, matatizo ya kupumua na matatizo yanayohusiana na matatizo ya moyo na alishatibiwa katika Hopitali ya Mwananyamala Dar es Salaam.

Kuhusiana na dawa hizo, Nusura alikana kuzifahamu wala kuwa na uhusiano nazo na alikanusha jina la Nusura Sultani Mtinde na kwamba jina lake halisi ni Nusura Sultani Mtinge na hahusiki na nyaraka zozote za kusafiria zenye ubini wa Mtinde.

Katika kujaribu kujinasua na kadhia hiyo, Nusura alimwita dada yake aitwaye Salma Sultani Mtinge ambaye ushahidi wake uliunga mkono ushahidi wa mrufani kuwa alikuwa ni mgonjwa kama ambavyo kielelezo D2 kinavyojieleza.

Ingawa wazee washauri wa mahakama walimuona Nusura hakuwa na hatia ya kosa la kusafirisha dawa hizo za kulevya, lakini Jaji Gwae alimtia hatiani kwa kosa hilo na kumhukumu kifungo cha maisha jela, na ndipo akakata rufaa kupinga.

Katika rufaa hiyo, Nusura aliegemea sababu 11 ikiwemo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu alikosea kisheria alipoacha wajibu wake wa kuchunguza ushahidi wote na hivyo kuamua kimakosa kuwa kielelezo cha sita ambacho kilikuwa na dawa za kulevya zinazodaiwa kuwa ni bangi ni mali yake aliyokuwa akisafirisha.

Nyingine ni Jaji kukosea kwa kushindwa kutambua kielelezo cha 23 ambacho kilipatikana kinyume cha sheria, kwa kushindwa kuzingatia Jamhuri haikutoa cheti kuthibitisha upekuzi hasa ikizingatiwa kuwa haukuwa upekuzi wa dharura.

Hoja nyingine ni Jaji kukosea kisheria kumtia hatiani bila kuzingatia kanuni zinazopaswa kuzingatiwa katika mlolongo wa uhifadhi wa vielelezo, ushahidi wa mashtaka kutofautiana na kesi ya mashtaka kutothibitishwa bila kuacha shaka.

Nusura aliwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Majura Magafu huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Rose Sulle ambapo wakili Sulle aliweka wazi msimamo wa kutounga mkono rufaa.

Wakili Magafu aliweka wazi suala moja kuu ambalo Nusura alitaka mahakama hiyo iamue ni kama dawa za kulevya anazodaiwa kukutwa nazo na kudai Jamhuri ilishindwa kuthibitisha kuwa Nusura alikutwa na dawa hizo kinyume cha sheria, na mnyororo wa utunzaji wa vielelezo ambavyo ni dawa ulikatika.

Kuhusu cheti cha kukamata, wakili Magafu alieleza hati hiyo ni batili na hakuna hukumu halali inayoweza kukiegemea na kuwa namba iliyokuwa kwenye tiketi ambayo ni kielelezo namba 23, ambayo ilikuwa tofauti ikilinganishwa na namba halisi ya kwenye tiketi halisi ya kielektroniki kwa namba moja kuzidi.

Wakili Magafu aliomba kielelezo hicho na tiketi ya kupandia ndege ‘boarding pass’ kufutwa kwenye kumbukumbu za mahakama na kudai mahakama haikuthamini ipasavyo ushahidi na ingefanya hivyo isingemtia hatiani mteja wake.

Kwa upande wake, Wakili Sulle alidai tofauti kati ya tarakimu kwenye kielelezo cha 23, ilikuwa ni hitilafu ya kuandika na hata kielelezo hicho na tiketi ya kupandia ndege vikiondolewa kwenye kumbukumbu hakutakuwa na athari yoyote kwa upande wa mashtaka, ushahidi utakaobaki utatosha kumtia hatiani.

Kuhusu mlolongo wa uhifadhi wa vielelezo ambazo ni dawa hizo, wakili Sulle alidai hilo lilizingatiwa ipasavyo na ushahidi wa mashahidi sita uliweka wazi mlolongo wa uhifadhi wa dawa hizo tangu zilipokamatwa KIA hadi zilipotolewa mahakamani kama kielelezo na kuomba rufaa itupiliwe mbali.

Baada ya kusoma misingi ya rufaa iliyowasilishwa na kuzingatia mawasilisho ya mawakili wa pande zote, jopo la majaji watatu lilieleza kuwa malalamiko makubwa ya mrufani ni uharamu wa cheti cha kukamata dawa hizo na kielelezo cha 19.

Kuhusu uhalali wa cheti cha kukamata,Jaji Galeba kwa niaba ya jopo hilo la majaji wenzake,  alisema utofauti wa namba za ‘serial’ kwenye tiketi ya kielektroniki na tiketi ya kupandia ndani ya ndege ‘boarding pass’ hazikubashiwa wakati wa usikilizwaji wa awali (PH), hivyo haikutarajiwa kuwasilishwa katika hatua ya rufaa.

“Wakati wa usikilizwaji wa awali (PH) mbele ya mahakama ya awali, kati ya mambo manne na nyaraka ambazo hazikubishaniwa, ni tiketi ya kielektroniki na tiketi ya kupandia ndani ya ndege,na nyaraka zote mbili zina jina la mrufani la ukoo Mtinde na siyo Mtinge,”walisema majaji hao.

“Tunapofikia uamuzi wa hoja iliyo hapo juu, ni muhimu tuseme mamlaka ya Mahakama hii ya kuondoa au kufuta ushahidi wowote wa maandishi kutoka kwa rekodi ya mahakama, sio uwezo ambao Mahakama hii inautumia kwa kawaida,” walieleza majaji hao hao katika hukumu yao hiyo.

“Hasa pale ambapo hati au sehemu ya hati haikupingwa hata kidogo wakati wa kuitoa au wakati wa kumhoji shahidi aliyeitoa,” walisema.

Wamesema katika kesi hiyo wametathmini upya ushahidi wa mashahidi hawa wawili (shahidi wa 4 na 7) na hawakubaliani kwamba hawakuwa mashahidi wa kuaminika kwa sababu hawakuwa wanamfahamu mrufani.

“Kwa hivyo, malalamiko hapo juu hayana msingi.Kwa kumalizia, kwa kuzingatia mjadala katika rufaa hii, isipokuwa kwa agizo tulilofanya la kufuta kielelezo cha 19 na rufaa hii haina uhalali tunaitupilia mbali,” walisema majaji hao.

Related Posts