Bunge labaini udhalilishaji na mateso shamba la Ephata, Serikali yapewa rungu

Dodoma. Kamati Maalumu ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mgogoro wa ardhi katika shamba la Malonje, linalomilikiwa na mwekezaji Kanisa la Efatha, imebaini vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa taratibu za mauzo ya shamba hilo.

Kamati hiyo imebaini kuwa kwa nyakati tofauti kumekuwepo vurugu kati ya walinzi wa mwekezaji na wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba la Malonje, lililopo Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa.

Kutokana na hilo, Bunge limeielekeza Serikali ibatilishe umiliki wa shamba la Malonje na vitalu 51 kwa kuzingatia sheria na masilahi ya umma.

Vurugu hizo zimekuwa zikihusisha matumizi ya nguvu kupita kiasi, ikiwemo silaha za moto kwa upande wa walinzi wa mwekezaji na silaha za jadi kwa upande wa wananchi.

Kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe 11 iliundwa na Spika Dk Tulia Ackson kuchunguza mgogoro wa ardhi katika shamba hilo uliodumu kwa takriban miaka 10 baina ya mwekezaji na vijiji tisa. Kamati iliongozwa na mwenyekiti wake, Profesa Shukrani Manya.

Spika aliunda kamati hiyo kutokana na hoja ya dharura iliyowasilishwa bungeni Novemba 7, 2023 na mbunge wa Kwela, Deus Sangu, akitaka Bunge lijadili mgogoro huo kutokana na athari zilizowapata wananchi wa vijiji vinavyolizunguka shamba la Malonje.

Leo Jumanne, Agosti 27, 2024, Profesa Manya amewasilisha bungeni ripoti ya kamati hiyo ya kile walichobaini na mapendekezo. Wabunge wameichangia taarifa hiyo na kuishauri Serikali kuchukua hatua kwa watumishi wote waliohusika.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Profesa Manya amesema: “Kwa mujibu wa ripoti ya kamati, vurugu hizi zilisababisha mlinzi mmoja wa mwekezaji kuuawa na wananchi kujeruhiwa. Kamati ilishuhudia alama za majeraha kwa wananchi, na ushahidi huo ulithibitishwa kwa nyaraka za hospitali.”

Profesa Manya amewataja baadhi ya wananchi waliotoa ushahidi mbele ya kamati ambao ni Festo Kamwanga (aliyepigwa risasi kifuani, shavuni na mguuni), Eliud Kauzeni (aliyepigwa risasi kichwani na begani, na anaendelea kuishi na risasi kichwani hadi sasa).

Wengine ni Dickson Simkonde (aliyepigwa risasi tumboni), Nuru Togwa (aliyekatwa masikio yote mawili) na Martin Kazikupenda Mpisi (aliyevunjwa miguu na sasa amekuwa na ulemavu wa kudumu).

“Vurugu hizi zinaashiria uvunjifu wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi na kumiliki mali,” amesema Profesa Manya.

Amesema kamati imebaini vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake katika vijiji vya Sikaungu, Msandamuungano, Mawenzusi, Isesa, na Ulinji.

“Wanawake saba walieleza walifanyiwa vitendo hivyo na walinzi wa mwekezaji. Walieleza walikamatwa na kupelekwa katika eneo la majumba mawili ndani ya shamba na kufanyiwa vitendo vya ukatili, ikiwemo kubakwa.

“Hata hivyo, wanawake hao walikiri kutoripoti matukio hayo polisi kutokana na aibu na hofu ya kuachwa na waume zao.

“Kamati ilipata fursa ya kumhoji msimamizi wa kitengo cha ulinzi wa shamba, ambaye alikiri huwakamata watu wanaopita shambani bila ruhusa na kuwahifadhi katika eneo lao maarufu kama Majumba Mawili,” amesema Profesa Manya.

Profesa Manya amesema kamati pia ilibaini kuwa ongezeko la ardhi ya shamba la Malonje kutoka ekari 300 hadi ekari 47,520 kati ya mwaka 1946 na 1974 ilisababisha baadhi ya vijiji kukosa ardhi ya kutosha kwa ajili ya makazi, kilimo, na malisho ya mifugo.

Pia, amesema kamati iligundua mwaka 2007, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ilitangaza kuuza hekta 10,000 za shamba la Malonje bila kushirikisha wadau muhimu kama Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na vijiji husika.

Profesa Manya amesema pia kamati imebaini kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa haikufuata maelekezo ya Baraza la Mawaziri kuhusu ugawaji wa shamba la Malonje.

“Badala yake, ofisi hiyo iliamua kuuza hekta 10,002 kwa mwekezaji na kugawa hekta 3,748 zilizobaki kwa matumizi mengine, jambo lililosababisha migogoro zaidi,” amesema.

Akichangia taarifa hiyo kwa mtizamo tofauti, mbunge wa Mwanga, Anania Thadayo alisema Serikali ilishafikia uamuzi wa kubatilisha umiliki wa shamba hilo, lakini mchakato ulisita.

Amehoji pia kuhusu taasisi ya kidini kumiliki kampuni za ulinzi zenye silaha za moto, jambo linalohitaji uchunguzi zaidi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya amesema mwekezaji amekuwa akivunja taratibu na haki za binadamu na kuongeza kuwa amepatiwa zaidi ya hekta 10,000 ilhali makubaliano yalikuwa ya hekta 3,000 tu kwa ajili ya ufugaji wa kisasa na alisisitiza umiliki wa shamba ubatilishwe.

Mbunge wa Viti Maalum, Stella Manyanya aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, amesisitiza Serikali imewekeza fedha nyingi katika kutatua mgogoro huu na ni muhimu kufikiria jinsi gani wananchi watanufaika na ardhi hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Mayenga amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwabadilisha viongozi wote wa Mkoa wa Rukwa na kufanya uchunguzi kuhusu wale wanaofaidika na mwekezaji wa shamba la Malonje.

Mbunge wa Viti Maalumu, Asia Halamga amesema mwekezaji amekwenda kinyume na makubaliano ya awali kwa kufanya kilimo badala ya ufugaji.

Pia, ametoa wito kwa Jeshi la Polisi la Mkoa wa Rukwa kujitathmini upya kutokana na matukio ya ukandamizaji yanayodaiwa kufanyika dhidi ya wananchi.

Joseph Musukuma, mbunge wa Geita Vijijini amesema suala la Malonje sio geni na linahitaji uamuzi mgumu, ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi wa vijiji vinavyohusika.

Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate amesisitiza kuwa wawekezaji lazima wawe wanaoheshimu taratibu na haki za binadamu.

Alibainisha kuwa kuna mazingira ya rushwa katika upatikanaji wa shamba hilo na uongozi wa mkoa kuhusika katika kudanganya kamati ya Bunge kuhusu hali halisi ya mgogoro huo.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani amesema kuna haja ya kufanya tathmini ya kina ya hali ya shamba la Malonje na kushauri wananchi wapewe elimu kuhusu manufaa ya uwekezaji huo.

Kwa upande wake mbunge wa Momba, Condester Sichalwe ameonya dhidi ya tabia ya viongozi kulindana na kuwanyamazisha wabunge wanapotoa malalamiko yao.

Amesema changamoto kama hizo zipo maeneo mengi nchini na ni muhimu kusikiliza sauti za wabunge na wananchi.

Mbunge wa Babati, Pauline Gekul amependekeza kamati iendelee kufuatilia matatizo ya ardhi maeneo mengine nchini na kutoa ufumbuzi wa kudumu kwa migogoro kama huu wa shamba la Malonje.

Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo akionyesha msimamo wake wa kumtetea mwekezaji wa ndani, lakini amesema alibadilisha msimamo huo baada ya kushuhudia hali halisi shamba hilo.

Amesema shamba hili lifutwe umiliki wake kwa sababu limekuwa likiwakosesha wananchi ardhi ya kulima.

Akitoa maazimio ya Bunge, Spika Tulia alisema Bunge limeielekeza Serikali kubatilisha umiliki wa shamba na vitalu 51 kwa kufuata sheria na masilahi kwa wananchi.

“Kwa kuzingatia hayo, Bunge linaazimia kwamba mamlaka zinazohusika na uendeshaji wa kesi za jinai nchini zifanye uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kulingana na matokeo ya uchunguzi huo.

“Walinzi wa kampuni ya Funguka Security Co. Ltd wanaolinda shamba la mwekezaji wamekuwa wakituhumiwa kwa vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na kutumia silaha za moto.

“Serikali ifanye tathmini juu ya taratibu zinazotumika kwa sasa kutoa vibali kwa kampuni za ulinzi. Serikali ifanye uchunguzi juu ya uhalali na weledi wa walinzi wa mwekezaji,” amesema.

“Serikali ichukue hatua dhidi ya walinzi wa kampuni ya Funguka waliohusika na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu.”

Wabunge walipotaka Bunge limuagize Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima afungue kesi ya udhalilishaji dhidi ya mwekezaji huyo, Spika Tulia amesema hayo yamo kwenye maazimio kwa kuchunguza na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuhusika na udhalilishaji huo.

Ripoti ya kamati pia imependekeza hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu na taratibu za umiliki wa ardhi.

Pia, imependekeza uchunguzi zaidi ufanyike na vyombo vya dola ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi wa vijiji vinavyohusika na mgogoro huo.

Miongoni mwa malalamiko ni wanawake kudhalilishwa, watu kupigwa risasi, madai ya ubakaji na watu kukodishwa kulima shamba kwa Sh10,000 kwa eka, huku wakilazimishwa kutoa fungu la 10.

Madai mengine ni viongozi wa Serikali kuungana na mwekezaji kwa madai ya kupewa rushwa.

Hata hivyo, Bunge lililazimika kuchukua muda mrefu kujadilia namna ya kuweka vizuri eneo linalohusu kubatilisha umiliki wa shamba ili lisije kutafsiriwa kwamba na vijiji navyo vibatilishwe na kupimwa upya.

“Waheshimiwa wabunge hoja hapa ni shamba na vitalu 51 na si kubatilisha vijiji, tusije kuleta taharuki huko kwa wanakijiji,” ametahadharisha Spika.

Pia, Spika ametahadharisha hoja ya Serikali iandae mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyote vinavyozunguka shamba hilo pamoja na Gereza la Mollo, kwa kuwa suala la matumizi bora ya ardhi linapangwa na vijiji vyenyewe.

Maelekezo ya Bunge ni Serikali ilipime shamba hilo na kuligawa upya kwa wahusika mbalimbali, ikiwemo wanavijiji, gereza la Mollo, mwekezaji (Kanisa la Efatha) na wenye vitalu kwa kuzingatia mahitaji halisi ya ardhi na uwezo wa kila mhusika.

Related Posts