Huduma za matibabu Zanzibar ziboreshwe

Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) hivi karibuni imeeleza kwamba hospitali kubwa za mikoa na wilaya ziliojengwa karibuni Unguja na Pemba zitasimamiwa na sekta binafsi. Uamuzi huo, kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Nassor Mazrui, unalenga kuzifanya hospitali hizi kuwa na huduma za kiwango cha kimataifa.

Kwa mujibu wa waziri huyo, katika kipindi cha miaka miwili wakati hospitali hizi zikiendeshwa na kampuni za sekta binafsi, wananchi watapata matibabu na huduma nyingine kama za vipimo bila ya malipo na serikali ndio itayolipa.

Waziri alikiri hospitali binafsi zinatoa huduma nzuri na ndio maana serikali imeamua kuipa sekta binafsi kuziendesha na uzoefu umeonyesha wananchi wengi wanakimbilia hospitali binafsi licha ya kutumia fedha nyingi.

Hatua hii Serikali ya Rais Hussein Mwinyi inafaa kupongezwa kwa sababu gharama za matibabu siku hizi ni pasua kichwa na mzigo usiobebeka, hasa kwa watu wenye kipato cha chini na zaidi masikini na fukara.

Lakini tujiulize kwa nini watu wengi wanakimbilia hospitali binasi kupata huduma za matibabu licha ya gharama zake kuwa kubwa na hata zikiwa mbali na makazi yao. Sababu ni nyingi na zipo wazi. Kwa miaka mingi watu wanalalamikia huduma katika hospitali za serikali sio tu haziridhishi, bali zimejaa kero na bughudha zinazomzidishia mgonjwa maradhi badala ya kumpa ahueni.

Watu wanaambiwa matibabu ni bila ya malipo wakati sio kweli kwani malipo yapo na inaweza kuchukua mwezi hujapata vipimo.

Leo utaambiwa kifaa fulani kimeharibika, unakwenda siku nyingine utatakiwa uwe mstahamilivu hula mbivu au tupo mbioni kuuirekebisha hali.

Hiyo huduma bila ya malipo imepakwa vipodozi vya kuitwa mchango na hakuna hata cheti cha kuandikia maelezo ya mgonjwa ambaye hutakiwa akanunue kitabu na akienda kuchukua dawa, anapata zawadi ya cheti kulichochorwa alama ya X kwenye karibu dawa zote.

Kwa hivyo, mgonjwa analazimika kwenda kununua dawa katika duka la mtu binafsi. Sasa hayo majigambo ya huduma za matibabu Zanzibar yana faida gani kama si kuwadanganya wananchi na ulimwengu?

Fikiria mzazi ambaye ni masikini anatakiwa akienda kujifungua aende na mipira ya kinga anayovaa mkunga, dawa za sindano na vifaa vingine kama vile anafungua duka la dawa.

Wakati hali ikiwa hivyo, bado viongozi na watendaji wakuu wa serikali wanaendelea kujitapa kuwa huduma za matibabu Zanzibar ni nzuri na bila ya malipo. Tuache kudanganya watu.

Kama huduma katika hospitali za serikali ni nzuri, inakuwaje hata viongozi na watendaji wakuu wa serikali, wakiwemo wa Wizara ya Afya kutoka nje ya Zanzibar wanapata matibabu na Uingereza, Afrika Kusini, India au nchi za Ghuba kila baada ya miezi michache.

Kila siku boti zinazofanya safari kati ya Zanzibar na Dar es Salaam zinabeba wagonjwa wanne au watano kwenda au kurudi Dar es Salaam.

Kama huduma na gharama za matibabu Zanzibar zinaridhisha, hakuna mwenye akili timamu atayekwenda Dar es Salaam au nchi jirani kupata matibabu. Ukweli ni kwamba hali ya hospitali za serikali Visiwani sio nzuri na ndio maana wapo watu wanaoziita “hospitali majengo”.

Ni vizuri tukajenga utamaduni wa kuueleza umma ukweli na kuacha kudanganya na kuanza kuzitibu hizi hospitali ambazo zinaumwa kwa muda mrefu na zinahitaji matibabu kama hao wagonjwa wanaofika hapo.

Jingine muhimu ni umma kupata maelezo yakinifu ya vigezo na mchakato utakaozifanya hizo kampuni kukabidhiwa hizi hospitali na masharti yaliyomo kwenye mikataba. Watu watafarajika kuona zabuni zinatolewa na uamuzi unafanywa kwa uwazi na sio kuambiwa uamuzi una nia njema. Hio nia njema ni vyema itumike kwa mambo binafsi na sio mali ya umma.

Hata nia njema ikiwa njema, kama hakuna uwazi zitakuwepo mashaka ya rushwa na upendeleo. Tufanye mambo kwa uwazi na sio kulazimisha umma uamini nia njema.

Tumesikia na kuona katika mitandao madai ya zabuni kutolewa kwa mlango wa nyuma na hata kutajwa juu juu kuwa baadhi ya wanaonufaika ni miradi na kutoa huduma serikalini ni wanafamilia na marafiki wa akina fulani.

Vilevile, yapo madai kuwa wakati mwingine zimeundwa kampuni haraka haraka ili kupewa kazi iliyopo mezani.

Tuanze kuweka mambo wazi ili wasiwasi wa rushwa na ufisadi usipate mwanya na watu kurudisha imani juu ya utendaji wa Serikali. Tujirekebishe kwa maslahi za Zanzibar na watu wake. Vitendo vyetu vilingane na kauli zetu.

Related Posts