Israel yashambulia kote Gaza, vifaru vyaingia Khan Younis – DW – 28.08.2024

Wakaazi wa Khan Younis wamesema vifaru vimesonga mbele katikati mwa mji huo, huku jeshi likiamuru watu wahame katika upande wa mashariki, na kuzilaazimu familia nyingi kukimbilia usalama wao, huku wengine wakikwama nyumbani.

Maafisa wa afya wa Palestina wamesema mashambulizi ya Israel mjini Khan Younis yameuwa watu wasiopungua 11. Katika mji wa kati wa Deir Al-Balah, ambako watu wasiopungua milioni moja wanajihifadhi, shambulio la Israel limeua Wapalestina wanane karibu na shule inayohifadhi familia zilizokoseshwa makaazi.

Mjini Nuseirat, katikati mwa Ukanda wa Gaza, mwandishi habari Mohammed Abd-Raboo aliuawa pamoja na dada yake katika shambulio la Israel dhidi ya nyumba yao.

Soma pia: Mashambulizi ya Israel yaua 100 katika mmoja ya usiku mbaya zaidi wa vita Gaza

Ofisi ya habari ya serikali ya Gaza ilisema kifo cha Abd-Raboo kimefanya idadi ya waandishi habari wa Kipalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel kufikia 172 tangu Oktoba 7.

“Tunalaani kile kilichofanywa na wakaliaji wa Israel na kuitolea wito jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za kuwalinda waandishi habari katika Ukanda wa Gaza baada ya tukio hili,” alisema Omar Abd Rabboo, ambaye ni kaka yake na Mohammed Abd Raboo.

Ukanda wa Gaza| Mashambulizi dhidi ya Khan Younis
Wapalestina waliohamishwa wakitazama wakati makombora yakishambulia eneo la makaazi mjini Khan Younis.Picha: Bashar Taleb/AFP

Amri za kuhama zazusha malamiko

Katika siku za karibuni, Israel imetoa amri kadhaa za kuhama kote katika Ukanda wa Gaza, ambazo ni nyingi zaidi tangu mwanzoni mwa vita vya karibu miezi 11, na kusababisha malalamiko kutoka kwa Wapaletina, Umoja wa Mataifa na maafisa wa misaada kuhusiana na maeneo ya kiutu yanayozidi kupungua na ukosefu wa maeneo salama.

Jeshi la israel limesema lilitoa amri ya kuhama kartika maeneo ambako Hamas na makundi mengine yalifanya mashambulizi, ikiwemo ufyatuaji wa roketi kuelekea Israel.

Matawi ya kijeshi ya Hamas na Islamic Jihad yamesema wapiganaji wake walipambana na vikosi vya Israel kote katika ukanda wa Gaza, wakifyatua roketi za kuharibu vifaru na mizinga ndani ya Israel.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Soma pia: Israel yafanya mashambulizi makubwa ya kuwalenga Hamas Gaza

Zaidi ya Wapalestina 40,500 wameuawa katika vita vya Gaza kwa mujibu wa wizara ya afya ambavyo pia vimeshuhudia kuangamizwa kabisaa kwa sehemu kubwa ya Ukanda huo.

Idadi kubwa zaidi ya wakaazi milioni 2.3 wamehamishwa mara kadhaa, na wanakabiliwa uhaba mkubwa wa chakula na dawa, yanasema mashirika ya kiutu.

Katika Ukingo wa Magharibi Israel imeendesha uvamizi mkubwa kwa kutumia mamia ya wanajeshi wa miguu na mashambulizi ya ndege katika miji minne, ambamo Wapalestian10 wameuawa, katika kile ilichokiita operesheni ya kupambana na ugaidi.

Wizara ya afya ya Palestina inasema zaidi ya Wapalestina 630 wameua katika operesheni za jeshi la Israel ndani ya Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita vya Gaza.

 

Related Posts