BAADA ya juzi Jumanne kurejea Zanzibar wakitokea Misri walipokwenda kucheza mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Pyramids, Kocha Mkuu wa JKU, Salum Haji maarufu Kocha Msomi amefichua mambo manne yaliyosababisha kufeli.
JKU iliyokuwa ikiiwakilisha Zanzibar katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ilitolewa hatua ya awali baada ya kufungwa jumla ya mabao 9-1 dhidi ya Pyramids.
Mechi zote mbili baina ya timu hizo zilichezwa nchini Misri ambapo ile ya kwanza JKU waliokuwa wenyeji kikanuni walifungwa 6-0, kisha ya pili wakachapwa 3-1.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema mbali na kuwepo kwa maneno mengi juu ya uamuzi wao wa kwenda Misri kucheza mechi zote, lakini kuna jambo kubwa wamejifunza kupitia michezo hiyo.
Kocha huyo alibainisha kwamba katika mambo manne yaliyosababisha kupoteza mechi kwa idadi kubwa ya mabao ni changamoto ya kuwasilisha majina katika usajili wa CAF.
“Naamini kama mtu anajua kupigana anaweza kukupiga hata mlangoni kwako, kwa hiyo ukiacha hiyo changamoto inayosemwa ya sisi kwenda kuchezea ugenini mechi zote lakini wenzetu wametuzidi vitu vingi na sisi tumechukua kama somo.
“JKU tumepoteza kwa mabao mengi mechi ya kwanza kutokana na mambo makuu manne, jambo la kwanza tumefungwa kwa sababu vijana wetu ni wadogo hawana uzoefu mkubwa, hivyo walikuwa na hofu wakati mechi inachezwa, kilichowatisha zaidi ni jina la wapinzani wetu namna kiwango chao kilivyo na wao wamekuwa wakiiona.
“Jambo la pili ni viwanja vya kuchezea, huku Zanzibar viwanja tunavyochezea karibia vyote ni nyasi bandia, lakini wenzetu hawavitumii hivyo. JKU tulipokuwa kule tumetumia viwanja sita tofauti na hakuna chenye nyasi bandia, kina majani halisi, ukiwa na viatu ambavyo havikamati vizuri unapata shida. Kiukweli viwanja vilikuwepo vingi tu vizuri lakini havikuwa rafiki.
“Tatu, ilitokea changamoto wakati unatumwa usajili CAF, walisahau kutuma cheti changu, kwa hiyo tunafika kwenye mechi kamishna ananiambia siwe
zi kukaa benchi kwa sababu sijathibitishwa na CAF, uongozi ulipambana kuliweka sawa jambo hilo hadi linakamilika mechi ilikuwa imesalia dakika 15 kumalizika, kwa hiyo mpaka napata nafasi ya kukaa benchi timu ilikuwa imefungwa mabao matano, kwa hiyo watoto (wachezaji) walikuwa na mshtuko kwa nini hawamuoni baba (kocha) akiwa karibu yao.
“Jambo la nne ni ukubwa wa Pyramids na uzoefu waliokuwa nao ndiyo ikasababisha tupoteze kwa mabao mengi. Nadhani mambo haya manne yalisababisha tupoteze kwa idadi kubwa ya mabao mechi ya kwanza.
“Mechi ya pili tulipunguza idadi ya mabao kwa sababu tulianza kuzoea viwanja ambavyo wenzetu wamekuwa wakivitumia. Kwa takribani siku kumi tulizokuwa ilibidi tuvizoee lakini pia nilipata nafasi ya kukaa benchi kuanzia dakika ya kwanza hadi mwisho, vitu hivi ilitufanya tupunguze idadi ya magoli,” alisema kocha huyo.”
Zanzibar iliwakilishwa na timu mbili katika michuano ya kimataifa msimu huu. Mbali na JKU, pia Uhamiaji nayo imeishia hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.