Dar es Salaam. Kampuni ya Johnelly TZ (Johnelly TZ Company Limitede) imekwaa kisiki mahakamani katika harakati zake wa malipo ya fidia kutoka Benki ya Equity Tanzania Limited (EBT), kwa madai ya kukiuka mkataba wa mkopo baina yake na benki hiyo.
Mahakama ya Rufani katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo, Lugano Mwandambo (kiongozi wa jopo), Issa Maige na Amour Khamis, mahakama hiyo imeamuru kuwa benki hiyo haikukiuka mkataba huo.
Hii ni mara ya pili kwa kampuni hiyo kushindwa dhidi ya benki hiyo, katika kesi hiyo iliyotokana na mgogoro wa malipo ya mkopo baada ya kampuni hiyo kushindwa kurejesha mkopo huo iliouchukua kutoka benki hiyo ya benki hiyo ya EBT kwa kampuni hiyo.
Hukumu hii ya Mahakama ya Rufani iliyotolewa Agosti 22, 2024 ni mwendelezo wa ushindi wa EBT na pamoja na Equity Bank Kenya Limited (EBK), ambazo zimejikuta katika wakati mgumu kukabiliwa na kesi kadhaa zilizofunguliwa dhidi yake na kampuni mbalimbali.
Kampuni hizo ambazo zilikuwa wateja wa benki hizo zimezifungulia benki hizo kesi baada ya kukopeshwa fedha taslimu ama benki hizo ziliziwekea udhamini kuziwezesha kupata mkopo wa mabilioni ya pesa kutoka kwa wakopeshaji wa nje ya nchi.
Hata hivyo, badala ya kurejesha mkopo huo, kampuni hizo ama zilishindwa au zilipuunza na hivyo benki hizo kama mdhamini zikalazimika kurejesha mikopo hiyo kwa wakopeshaji hao wa nje na zenyewe ndio zikabaki kuzidai kampuni hizo.
Kampuni hizo badala ya kuzilipa benki hizo, zilizigeuzia kibao na kuzifungulia kesi zikipinga kulipa mikopo hiyo kwa madai kuwa ama zilishalipa au kwamba hazikuwahi kukopeshwa wala kudhaminiwa na benki hizo kutoka kwa mkopeshaji wa nje, bali zilipata mkopo huo bila dhamana.
Katika kesi mbili miongoni mwake ambazo Mwananchi limeona hukumu zeke, benki hizo ziliwasilisha mahakamani mikataba ya mikopo hiyo inayoonesha kuwa moja ya masharti ili mkopaji (kampuni) ziweze kupewa mkopo na mkopeshaji wa nje lazima kwanza zipokee kwanza dhamana ya mkopo huo.
Miongoni mwa mashahidi wa benki hizo katika baadhi ya kesi hizo walikuwa ni wawakilishi wa mkopeshaji huyo wa nje ambao waliieleza mahakama kuwa walizikopesha kampuni hizo baada ya kupokea dhamana kutoka kwa benki hizo na waliposhindwa kulipa benki hizo zililazimika kulipa deni hilo.
Hata hivyo, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara katika hukumu yeke ilizipa ushindi kampuni hizo baada ya kukubaliana na madai yake kuwa benki hizo hazina madai yoyote dhidi yake na kwamba mkopo huo ziliupata bila dhamana ya benki hizo.
Hukumu hii inatokana na kesi ya msingi iliyofunguliwa na kampuni ya Johnelly dhidi ya EBT, katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni mwaka 2018, kutokana na mgogoro wa mkopo wa jumla ya Sh290 milioni uliiotolewa na benki hiyo ya EBT kwa kampuni hiyo.
Katika kesi hiyo namba 208/2018, kampuni ya Johnelly ilikuwa ikidai kuwa EBT ilikiuka mikataba mitatu ya mikopo iliyoingiwa na pande hizo mbili, Desemba 10,2016, Machi 29, 2017 na Agosti 28, 2017 kwa ajili kuendeshea shughuli zake za kibiashara.
Kampuni hiyo iliweka dhamana miongoni mwake ikiwa ni mali inayohamishika, gari la kubebea mafuta (Tanker Trailer) namba za usajili T 531 DKE, lenye thamani ya Sh70 milioni.
Lakini kampuni hiyo ya Johnelly haikurejesha mkopo huo baada ya muda wa kurejesha kupita, hivyo EBT iliandikia notisi ya siku 14 ambazo baada ya kuisha, benki hiyo iliamua kukata gari hilo lililowekwa dhamana.
Hata hivyo gari hilo liliachiliwa na baada ya kampuni hiyo kulipa deni lake, ndipo baadaye kampuni hiyo ikaifungulia kesi hiyo EBT, ikidai kuwa kukamata mali hiyo baada ili kufidia deni lake, ilikiuka mkataba, ikidai kuwa haikuwa imewekwa dhamana kwa mkopo huo.
Katika kesi hiyo Johnelly ilidai malipo ya Sh80 milioni kama fidia ya hasara halisi iliyodai kuipata kwa benki hiyo kukiuka mkataba, Sh13 milioni ilizodai kuwa alilipwa dalali, kutoka kwenye akaunti yake isivyo halal, hasara ya jumla na gharama za kesi.
Mahakama ya Wilaya katika hukumu yake ilikubaliana na madai ya kampuni ya Johnelly na kuamua EBT ilikiuka mkataba na ikaiamuru kulipa fidia ya Sh60 milioni na Sh13 milioni zilizodaiwa kukatwa isivyo halali kutoka katika akaunti ya kampuni hiyo.
EBT ilikata rufaa Mahakama Kuu Masjala ya Dodoma, rufaa namba 39/2020, ikipinga hukumu hiyo na Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Lameck Mlacha Julai 21, 2021, ilisma kuwa EBT haikukiuka mkataba kwa hatua iliyoichukua.
Hivyo Jaji Mlacha alitengua hukumu na amri za Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na kuiamuru kampuni hiyo iilipe benki hiyo gharama za kesi.
Kampuni ya Johnelly haikukubaliana na hukumu hiyo ndipo ikakata rufaa hii Mahakama ya Rufani, rufaa namba 368/2021, ikipinga hukumu hiyo ya Mahakama Kuu.
Hata hivyo, kampuni hiyo iliitelekeza rufaa yake hiyo kwani siku ya usikilizwaji hakuwepo mahakamani na EBT iliwakilishwa na wakili Godwin Nyaisa.
Kwa kuwa pande zote tayari zilikuwa zimeshawasilisha maelezo yake ya maandishi, mahakama hiyo kwa mamlaka iliyo nayo chini ya Kanuni ya Mahakama hiyo za mwaka 2009, ilikubaliana na maombi ya wakili Nyaisa kumsikiliza upande mmoja hoja zake za mdomo.
Mahakama ya Rufani katika hukumu yake hiyo imekubaliana na hoja A EBT kupitia Wakili wake Nyaisa na imeunga mkono hukumu ya Mahakama Kuu.
“Kwa hiyo, katika kuhitimisha, mjibu rufaa (EBT) hakuvunja mkataba wala sheria yoyote iliyopo, kwa kukamata dhamana (gari lililokuwa lililokuwa na mgogoro) kama hatua ya kurejesha mkopo wake. Hivyo rufaa hii haina mashiko na inafuatwa”, imesema Mahakama baada ya kusikiliza na kuchambua hoja za pande zote.
Julai 23, 2024, benki hizo EBT na EBK zilishinda kesi nyingine ya mgogoro wa malipo ya mkopo wa jumla ya Dola za Marekani 8,064,807.88 (zaidi ya Dola 8.06 milioni) sawa na zaidi ya Sh21 bilioni, iliyokuwa imefunguliwa na kampuni ya ZAS Investment Company Limited
Katika kesi hiyo ya kibiashara namba 103 ya mwaka 2022, kampuni hiyo ya ZAS ilikuwa inapinga kudhaminiwa na benki hizo katika mkopo ilioupata kutoka kampuni ya nje.
Lakini benki hizo zilidai kuwa ziliidhamini kampuni hiyo kupata mkopo huo lakini ilishindwa kuulipa na zenyewe kama.mdhoni zikalazimika kulipa mkopo huo.
Katika hukumu hiyo pia Mahakama iliwaamuru wakurugenzi wa kampuni hiyo kuzilipa benki hizo zaidi ya Dola 7.6 milioni) sawa na zaidi ya Sh19.97 bilioni kama kiasi cha dhamana waliyoitoa kwa ZAS katika mkopo huo kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Pia, Agosti 16, 2024 benki hizo zilipata ushindi mwingine dhidi ya kampuni ya State Oil Tanzania Limited, baada ya kukubali kuzilipa benki hizo Dola za Marekani 13.5 milioni kutokana udhamini ambao benki hizo ziliiwekea na kuiwezesha kupata mkopo kutoka kampuni ya nje.
Awali, kampuni hiyo ilifungua kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara dhidi ya benki hizo ikipinga kudaiwa pesa yoyote na benki hizo.
Benki hizo pia zilifungua madai kinzani zikikdai kampuni hiyo zaidi ya Dola za Marekani 26.47 milioni likia ni deni la mkopo ambao ziliipatia kampuni hiyo Novemba 21, 2018, lakini Mahakama Kuu iliipa kampuini hiyo ushindi.
Benki hizo zilikata rufaa Mahakama ya Rufani ambayo ka Mei 16, 2024 ilibatilisha hukumu hiyo kutokana na kasoro katika mwenendo na ikaamuru isikilizwe upya, lakini baadaye kampuni hiyo ikakubali deni hilo na kukubalima ilipe kiasi hicho cha pesa.